Matrilioni ya fedha yanavyozunguka kwenye simu za mkononi Tanzania
Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Takwimu za Mawasiliano ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonyesha kuwa miamala inayofanywa kupitia huduma za kifedha za simu za mkononi imeongezeka kwa zaidi ya Sh1 trilioni ndani ya mwezi mmoja.
Ripoti hiyo ya robo ya kwanza ya mwaka 2019, inabainisha kuwa mwezi Machi pekee thamani ya miamala ya fedha iliyofanywa katika simu za mkononi ilifikia Sh7.82 trilioni kutoka Sh6.7 trilioni iliyorekodiwa Februari mwaka huu.
Katika mwezi huo wa Machi watumiaji wa huduma hiyo walifanya miamala milioni 243.5 ikiwa ni juu kidogo kutoka miamala milioni 215 ya Februari.
Huduma za kifedha za kwenye simu zinasaidia kuongeza mzunguko wa fedha nchini na kutatua changamoto mbalimbali za kibenki ikiwemo kuweka fedha, kukopa na kulipia huduma na bidhaa mbalimbali.