Mapato vituo makumbusho ya Taifa yapaa Tanzania
- Mapato yaongezeka hadi kufikia Sh443.2 milioni mwaka 2021/22.
- Kijiji cha Makumbusho Dar chaongoza kutembelewa.
Dar es salaam. Mapato yatokanayo na utalii wa vituo vya makumbusho ya Taifa yamezidi kuongezeka hadi kufikia Sh443.2 milioni mwaka 2021/22 huku idadi ya watalii nayo ikiongezeka kwa miaka miwili mfululizo, jambo linalosaidia kuimarisha sekta utalii nchini.
Mapato hayo ya mwaka 2021/22 ni hadi Aprili mwaka huu.
Vituo vya Makumbusho ya Taifa vilivyopo nchini, ni pamoja na Nyumba ya Utamaduni na Kijiji cha Makumbusho, vilivyopo jijini Dar es Salaam, Azimio la Arusha (Arusha) na Vita vya Maji Maji na kituo cha Dk Rashid Kawawa (Ruvuma).
Kingine ni kituo cha Mwalimu J.K Nyerere kilichopo Butiama mkoani Mara, kituo cha Elimu Viumbe (Arusha) na Mji Mkongwe Mikindani uliopo Mtwara.
Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2022/23 iliyowasilishwa hivi karibuni Bungeni na Waziri Balozi Pindi Chana, mapato yanayotokana na watalii kutembelea vituo hivyo yameongezeka kutoka Sh338.2 milioni mwaka 2020/21 hadi Sh443,2 mwaka huu.
Licha ya kuwa mwaka 2019/20 Serikali ilikusanya Sh356.2 milioni ambacho ni kiasi kikubwa ukilinganisha na mapato ya 2020/21, lakini ilipokea watalii 54,920 waliotembelea Makumbusho hayo.
Mwaka 2021/22, makumbusho hayo ya Taifa yalitembelewa na watalii 543,178 ambapo 537,655 kati yao walikuwa watalii wa ndani.
Ongezeko la idadi ya watalii nchini Tanzania huenda limechangiwa na kupungua kwa kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa Uviko-19 na hivyo watalii kupata fursa ya kusafiri.
Soma zaidi:
Vituo vilivyotembelewa na watalii wengi
Kijiji cha Makumbusho cha jijini Dar es Salaam ndiyo kiliongoza kwa kutembelewa na watalii wengi mwaka huu unaoisha Juni 30. Watalii 482,315, wengi wao wakiwa ndani walitembelea kijiji hicho na kuliingizia Taifa Sh148.3 milioni.
Kijiji hicho kilifuatiwa kwa mbali na Nyumba ya Utamduni iliyotembelewa na watalii 43,652, licha ya kuwa ndiyo imeongoza kuchangia mapato mengi yanayofikia Sh192.5 milioni.
Vituo vya makumbusho ya Taifa vilivyopokea idadi ndogo ya watalii ikiwemo ni Dk Rashid Kawawa, Mji mkongwe Mikindani na Elimu Viumbe.
Vituo hivyo havikupokea zaidi ya watalii 500 hadi kufikia April 2022.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa akiwasilisha mapendekezo ya bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 ilisema Tanzania inatarajia kuendelea kupokea watalii wengi hasa baada ya uzinduzi wa filamu ya “Royal Tour”.
“Kupitia Bunge hili, napenda kuendelea kuwakaribisha diaspora wa Tanzania na wawekezaji kutoka kona zote za dunia kuja kutalii na kuwekeza katika fursa za uwekezaji zilizopo nchini,” alisema Waziri Nchemba.
Latest
