Maonyesho ya ‘Expo 2020’ yazivalisha ndege za Emirates ‘nguo mpya’
- Uamuzi huo umefikiwa na Shirika la ndege la Emirates ikiwa ni maandalizi ya kutangaza maonyesho ya kimataifa ya ‘Expo 2020’ yatakayofanyika Dubai mwaka 2020.
- Ndege hizo zimepakwa rangi ya bluu, machungwa na kijani.
- Maonyesho hayo yanalenga kuonyesha kazi za ubunifu, ujasiriamali na teknolojia mbalimbali ili kuifanya dunia kuwa mahali salama poa kuishi.
Dar es Salaam. Shirika la ndege la Emirates limekamilisha upakaji rangi mpya ndege zake 40 ikiwa ni maandalizi ya kutangaza maonyesho ya kimataifa ya “Expo 2020” yanayotarajiwa kufanyika katika Jiji la kibiashara la Dubai lililopo katika nchi za Falme za Kiarabu za Emirates (UAE).
Maonyesho hayo ya “Expo 2020” yatafanyika kwa miezi sita kuanzia Oktoba 20, 2020 hadi Aprili 10, 2021 ambapo yanatoa fursa kwa wafanyabiashara na watu mbalimbali kutoka duniani kutangaza huduma na bidhaa zao.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya shirika hilo, hadi sasa ndege 40 za shirika hilo zimepambwa kwa rangi tofauti huku ndege ya kwanza kupambwa tayari imetua katika nchi 134 ulimwenguni na imekamilisha takribani safari 15,000.
Shirika hilo ambalo hufanya safari zake pia Tanzania limepamba ndege zake kwa rangi za bluu, kijani na machungwa zikiashiria fursa endelevu zinazohamishika zitakazopatikana katika maonyesho hayo.
“Ndege za Emirates zinabeba zaidi ya rangi zenye dhima ya fursa, uendelevu na uhamaji. Zinabeba pia ujumbe wa nguvu ya ushirikiano wa kimataifa kuonyesha wakati ujao uliobora kwa wote unaoletwa na maonyesho yanayoziunganisha zaidi ya nchi 190 kote ulimwenguni na mamilioni ya wageni hapa Dubai,” amesema Waziri wa Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa na Mkurugenzi wa Dubai Expo 2020, Reem Al Hashimy katika taarifa hiyo.
Maonyesho hayo yaliyobeba kauli mbiu ya “Ili kujenga ulimwengu bora tunatakiwa kutumia akili na mioyo yetu” yameandaliwa na Shirika la kimataifa linalosimamia maonyesho ya kimataifa la Bureau International des Expositions (BIE) yakiwa na lengo la kuonyesha ubunifu na teknolojia inayofaidisha sekta mbalimbali zikiwemo elimu, biashara na viwanda.
Pia yanalenga kudumisha mshikamano na ushirikiano baina ya nchi na nchi pamoja na kufurahia vumbuzi mbalimbali kutoka mamia ya nchi tofauti duniani.
Moja ya ndege ya Shirika la ndege ya Emirates ikiwa imepakwa rangi ya chungwa kuelekea maonyesho ya kimataifa ya Expo 2020.
Mwenyekiti Mtendaji wa BIE, Sheikh Ahmed bin Saeed Al Maktoum amesema lengo la kufikia uamuzi huo wa kuzibadilisha rangi ndege za Emirates ni kusambaza ujumbe wa maonyesho ya Expo 2020 ulimwenguni kote na Emirates ni fursa ya kuwafikia watu wengi na kuhakikisha wageni wanapata fursa ya kuhudhuria maonyesho hayo.
“Muunganiko hukutanisha mawazo mapya, mazungumzo ya ulimwengu na pia husaidia kufikia mabadiliko. Emirates inatoa huduma ya usafiri wa anga usiokoma kwa nchi nyingi zinazoshiriki maonyesho hayo na ambapo watu milioni 25 sawa na asilimia 70 watakaohudhuria maonyesho hayo wanatarajiwa kutumia usafiri wa anga,” amesema Maktoum.
Zinazohusiana:
- Airbus yatundika daruga kutengeneza ndege za kifahari za Airbus A380 Superjumbo
- Mambo unayotakiwa kufanya ukifika mapema ‘Airport’
- Shirika la ndege la Ethiopia limesitisha safari zote za ndege aina ya Boeing 737
- Shirika la ndege la Emirates lawapa ahueni wafanyabiashara Dar
Fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania
Maonyesho hayo ambayo pia yatakuwa na mahema ya kuhamishika ni fursa nyingine kwa watanzania wenye ndoto za kuifikia dunia kwa ubunifu na ujasiriamali wa teknolojia kukutana na wawezekaji, wabia wa maendeleo na wateja wa kimataifa.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara wa Tanzania wameiambia www.nukta.co.tz kuwa wangependa kuona maonyesho hayo yanafika Afrika ikiwezekana Tanzania kwasabau siyo watu wote wanaweza kufika Dubai.
“Natamani maonyesho hayo siku moja yafanyikie Tanzania au hata Afrika kwani tuna teknolojia na wavumbuzi wengi tu ambao hawajapata nafasi ya kuonekana,” amesema Kitulla ambaye hununua bidhaa zake Dubai.
Rangi ya kijani pia imetumika kutambulisha maonyesho ya Expo 2020 yatakayofanyika kwa miezi sita kuanzia Oktoba 20, 2020 hadi Aprili 10, 2020. Picha|Mtandao.
Kwa mara ya kwanza maonyesho ya kimataifa yalifanyika miaka 168 iliyopita kwenye mji wa Crystal Palace, Uingereza yakionyesha kazi mbalimbali za ubunifu na uvumbuzi za viwanda ambapo takribani vumbuzi 10,000 zilionyeshwa. Maonyesho hayo yalileta kwa mara ya kwanza teknolojia ya ‘Telegraph’ na ‘Typewriter’.
Tangu wakati huo maonyesho hayo yamekuwa yakifanyika kila baada ya miaka mitano ambapo mara ya mwisho yalifanyika katika Jiji la Milan, Italia mwaka 2015 ambapo yalitambulisha rasmi teknolojia ya miti ya sola na lifti zenye kutumia umemejua ambazo zimenufaisha wamiliki wa majengo marefu ulimwenguni.
Latest
