Mambo yatakayosaidia kuongeza ufaulu darasa la nne, kidato cha pili
- Ni kushughulikia changamoto ya lugha pamoja na uhaba wa walimu.
Dar es Salaam. Kufuatia kushuka kwa ufaulu kwenye mitihani ya kidato cha pili na darasa la nne kwa mwaka 2022, wadau wa elimu wamesema kuna haja ya kutafuta suluhu ya kudumu ya uhaba wa walimu lugha ya kufundishia ili kuokoa elimu nchini.
Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) lilitangaza matokeo ya kidato cha pili na darasa la nne Januari 4, 2022 huku ufaulu ukishuka kwa asilimia 3.35 kwa darasa la nne na asilimia 7.4 kwa kidato cha pili.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athuman Amasi aliyekuwa akitangaza matokeo hayo alisema asilmia 82.9 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa majaribio wa darasa la nne wamefaulu.
“Watahiniwa milioni 1.3 kati ya milioni 1.5 wenye matokeo wamefaulu mtihani kwa kupata madaraja A, B,C na D,” alisema Amasi mbele ya wanahabari kwenye ofisi za baraza hilo zilizopo jijini Dar es Salaam.
Wakati ufaulu ukishuka, idadi ya watahiniwa walioshika mkia kwa kupata daraja E imeongezeka kwa asilimia 3.35 ukilinganisha na idadi ya waliofeli mwaka 2021.
“Wataniwa 271,535 wamepata alama E sawa na asilimia 17.05,” ilisema Amasi.
Hiyo ni sawa kusema takriban watahiniwa wawili kati ya 10 wamefeli mtihani wa majaribio wa darasa la nne.

Mbali na somo la lugha ya kingereza somo la hesabati pia limewapa changamoto watahiniwa wengi kwenye mtihani wa majaribio wa darasa la nne. Picha EATV.
Ufaulu wa kidato cha pili nao waporomoka
Si ufaulu wa darasa la nne tu ulioporoka kwa mwaka huu, hata ufaulu wa kidato cha pili umeshuka kwa asilimia 7.4 ukilinganisha na ule wa mwaka 2021.
Akizungumza na wanahabari Amasi amesema kwa kidato cha pili ni asilimia 85 ya wanafunzi waliofaulu mtihani huo, huku wasichana wakiongoza.
“Kati ya watahiniwa 539,645 waliofaulu wasichana ni 283,541 sawa na 52.5 na wavulana ni 256,104 sawa na asilimia 47.5,” alisema Amasi.
Hata wakati matokeo ya ufaulu wa jumla yakishuka hali ni mbaya zaidi kwenye ufaulu wa madaraja ya masomo.
Kwa mujibu wa Necta, ni asilimia 7.65 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo wamepata daraja la kwanza. Hiyo ni sawa na kusema wanafunzi takriban nane kwa kila 100 waliofanya mtihani huo ndiyo wamepata daraja la kwanza.
Ufaulu wa wanafunzi waliopata daraja la kwanza umeshuka kwa asilimia 5.2 ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2021 ambapo wanafunzi 75,770 sawa na asilimia 12.58 ya wanafunzi waliofanya mtihani walipata daraja hilo la dhahabu.
Watahiniwa 45,288 sawa na silimia 7.15 wamepata daraja la pili huku zaidi ya nusu (asilimia 58.74) ya watahiniwa wakiangukia daraja la nne.
Watahiniwa 93,892 sawa na asilimia 14.82 wameshika mkia kwenye matokeo hayo kwa kupata daraja sifuri.
Zinazohusiana
-
Ufaulu ya darasa la nne washuka kwa asilimia 3.35
- Watahiniwa zaidi ya 270 wafutiwa matokeo darasa la nne, kidato cha pili
Nini sababu ya wanafunzi kufeli?
Wadau wa elimu nchini wanaeleza kuwa lugha ya kufundishia ndiyo mzizi wa kuporomoka kwa matokeo ya kidato cha pili na baadhi ya masomo kama Kiingereza kwa darasa la nne.
Mwandishi wa vitabu na mdau wa elimu, Richard Mabala anasema matokeo ya mwaka huu hayaridhishi na ufinyu wa uelewa wa lugha ya Kiingereza unawakwamisha wanafunzi kujifunza hali inayochangia kuporomoka kwa ufaulu
“Walio wengi wanaingia sekondari wakiwa na Kiingereza kidogo alafu unataka wajifunze kwa Kiingereza na wafaulu,” anasema Mabala na kusisitiza kuwa,
“Hali inakuwa mbaya zaidi wanapotakiwa kujifunza kwa Kiingereza masomo ya sayansi, ugumu wanaokutana nao kuanzia kwenye kujifunza darasani husababisha matokeo mabovu tunayoyaona.”
Kumekuwa na mjadala miongoni mwa wadau wa elimu kuhusu lugha ya kufundishia huku baadhi wakipendekeza Kiswahili kitumike kama lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu ili kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa na ujuzi kwa lugha wanayoimudu.
Hata hivyo, wengine wamekuwa wakisema lugha siyo tatizo bali kuimarisha mifumo ya ufundishaji na kuhakikisha wanafunzi wanaelewa Kiingereza ambacho kimekuwa kikitumika kama lugha ya kufundishia katika shule za sekondari.
ukaribu kati ya wazazi au walezi na wanafunzi ni njia bora ya kuwezesha matokeo mazuri kwenye masomo.Picha|Shutterstock.
Wingi wa wanafunzi, uhaba wa walimu chanzo kushuka kwa ufaulu
Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk Godfrey Kimaro anasema wingi wa wanafunzi darasani na uhaba wa walimu ni chanzo kingine cha kushuka kwa ufaulu huo wa wanafunzi wa kidato cha pili na darasa la nne.
“Ukiangalia uwiano wa walimu na wanafunzi hasa kwa ngazi ya chini kama shule za msingi na sekondari kwa kweli hali ni mbaya,” anasema Dk Kimaro.
Wingi wa wanafunzi humkosesha mwalimu fursa ya kumfikia kila mwanafunzi ili kumpatia maarifa.
Dk Kimaro anasema baadhi ya shule za sekondari hasa za kata zilizoanzishwa hivi karibuni zikabiliwa na changamoto ya vifaa vya kufundishia hasa katika masomo ya sayansi.
“Uhaba wa walimu wa sayansi ni mkubwa kuliko masomo mengine kuna shule ukienda utakuta mwalimu mmoja wa sayansi na bado wanafunzi hao watatatikiwa kujibu mitihani ya masomo hayo,” anasema Kimaro.
Tangazo
Serikali, wazazi fanyeni haya kuongeza ufaulu
Wadau hao walimu wanapendekeza suala la elimu liangaliwe kwa jicho la tatu na kuja na mbinu shirikishi zitakazosaidia kuongeza ubora wa elimu.
Akizungumza na Nukta habari (www.nukta.co.tz), Mabala anasema ni vyema Serikali ikaongeza kasi kwenye mabadiliko ya sera ya kujifunzia ili kunusuru taaluma za wanafunzi nchini.
“Serikali itengeneze mitaala ambayo itafanya watoto wafurahie kujifunza kwa ngazi zote,” anasema Mabala.
Sambamba na hilo mdau huyo anaishauri Serikali kuboresha miundombinu ya ufundishaji kuhakikisha vitabu vya kiada na ziada vinapatikana shuleni pamoja na kuwapa motisha walimu kwa kuwaongezea mishahara.
Kwa upande wa wazazi, mdau huyo wa elimu anasema ni wakati wao wa kuzingatia ubora wa elimu inayotolewa kwenye shule wanazowapeeleka watoto wao na kuhamasisha usomaji wa vitabu tangu watoto wakiwa wadogo.
“Ili mtoto aanze vizuri ni vyema kuanza tangu akiwa mdogo kwa kumnunulia vitabu vya kiada na ziada ikiwemo vitabu vya hadithi vitakavyochochea upatikanaji wa maarifa,” anasisitiza Mabala.
Latest
