Mambo yanayochangia kupata matatizo ya meno

April 11, 2023 1:30 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Huanza kwa kutengeneza utando wa bakteria kwenye jino (plaque)
  • Vyakula  vyenye asili ya sukari pamoja na asidi huchochea mchakato wa jino kuharibika.
  • Kupata tiba mapema kunaweza kuokoa jino lako.

Dar es Salaam. Meno ni kiungo muhimu katika mwili wa binadamu. Siyo tu katika shughuli za kurahisisha mmeng’enyo wa chakula bali hutusaidia kutoa matamshi fasaha lakini pia hutuongezea mvuto.

Kuna wakati kiungo hiki hugeuka kero hususan pale yanapoharibika kwa kutengeneza mashimo au kuvunjika jambo ambalo husababisha maumivu makali na kufanya mhusika kushindwa kufurahia mlo au kuzungumza kwa uhuru.

Wakati takwimu za Wizara ya Afya zikionesha mwaka 2020 kulikuwa na wagonjwa wa kinywa na meno 662,341 huku wagonjwa waliotoboka meno wakitajwa kuwa 507,508 ni muhimu kufahamu mchakato wa jino kuharibika.

Katika makala haya ya afya, Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imezungumza na mtaalamu wa meno anayeelezea mchakato wa jino kuharibika ambao utakusaidia jinsi ya kulinda jino lako na hivyo kuepuka gharama unazoweza kuingia ili kutibu meno yako pale yatakapoharibika.

Kwa mujibu wa Dk Benard Raymond kutoka kliniki ya meno ya Ndovu iliyopo jijini Dar es Salaam, mchakato wa jino kuharibika huhusisha vitu viwili ambavyo ni bakteria waliopo kinywani pamoja na asidi ambayo huzalishwa kutokana na vyakula tunavyokula au wakati wa mchakato wa mmeng’enyo unapoanza.

“Jino kuoza ni mchakato ambao husababishwa na utengenezaji wa asidi kwenye mdomo kutokana na bakteria ambao hukaa kwenye utando laini wa meno (plaque) na chakula tunachokula. 

Asidi hii husababisha kuharibika kwa enamel (tabaka la nje la jino) na hivyo kuanza kuoza,” amesema Dk Raymond.

Mchakato wa kuoza jino unaweza kuwa kama ifuatavyo:


Soma zaidi


Utengenezaji wa Plaque

Kwa mujibu wa Dk Raymond, katika  mchakato huu, bakteria hukusanyika kwenye meno na kujenga utando laini wa bakteria inayoitwa plaque na kisha asidi huanza kuzalishwa.

Asidi hiyo huzalishwa pale bakteria waliopo katika plaque wanapovunja sukari na wanga ndani ya chakula tunachokula. 

Majarida mbalimbali ya kitabibu ikiwemo Kituo cha Utafiti wa Afya ya Meno Marekani (NIH) yanavitaja vyakula vyenye sukari kama sababu ya kutengeneza asidi nyingi zaidi wakati wa mmeng’enyo hivyo ni muhimu kuviepuka.

Uharibifu wa enamel

“Enamel ni tabaka la juu la jino ambalo hufanya kazi ya kulinda jino lisiharibike kiurahisi. Asidi ikishazalishwa kwa wingi husababisha kuharibika kwa enamel na hivyo taratibu asidi huendelea kuharibu jino na kisha kutengeneza ufa ambao baadaye hugeuka kuwa shimo,” amesema daktari huyo.

Kuoza kwa jino

Ikiwa jino halitatibiwa mara baada ya kutoboka au kuwa na nyufa,  basi huoza na lisipotibiwa husababisha kuvunjika kwa jino amba[o dalili zake huwa ni kupata maumivu ya jino, uvimbe wa fizi, na kubadilika kwa rangi ya jino.

Jino lililooza husababisha maumivu makali au kuvimba kwa fizi matibabu yake ni kuling’oa au kuziba sehemu iliyoharibika. Picha| Kyrylo Glivin/Shutterstock

Gharama za matibabu ya meno

Usipoziba ufa utajenga ukuta. Ikiwa ulishindwa kujizuia kula vyakula vilivyosababisha jino kuharibika na ukashindwa kudhibiti na kutibu dalili mapema basi jiandae kutoboa mfuko kwa gharama utakazotakiwa kulipa ukienda katika kliniki ya meno.

Kwa mujibu wa daktari huyo, gharama za matibabu ya meno nchini Tanzania hutofautiana sana kulingana na eneo, huduma inayotolewa na hali ya jino lilivyooza. 

Mathalan, kutoa meno yanayovunjika au kusagwa kunaweza kugharimu kati ya Sh 50,000 hadi Sh200,000 kwa jino moja, huku gharama za kupata tiba ya kujaza jino zikiwa kati ya Sh30,000 hadi Sh100,000 kwa jino moja. 

“Kulingana na hali ya jino lilivyooza, huenda ukahitaji matibabu mengine kama vile upasuaji wa kutoa jino, kuweka meno ya bandia au kusafisha mizizi ya jino. Gharama za matibabu haya hutofautiana sana, lakini kwa ujumla zinaweza kugharimu zaidi ya Sh200,000,” amesema.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: RAIS SAMIA AKIHITIMISHA MAFUNZO YA UONGOZI NGAZI YA JUU, UONGOZI DARAJA LA PILI KOZI 2025/26

🔴LIVE: RAIS SAMIA AKIHITIMISHA MAFUNZO YA UONGOZI NGAZI YA JUU, UONGOZI DARAJA LA PILI KOZI 2025/26

Nukta TV

Rais Samia: Anzisheni mfuko  kuwasaidia wafungwa wenye ujuzi wanapotoka gerezani

Rais Samia: Anzisheni mfuko kuwasaidia wafungwa wenye ujuzi wanapotoka gerezani

Nukta TV

🔴LIVE: RAIS SAMIA AKIHITIMISHA MAFUNZO YA UONGOZI NGAZI YA JUU, UONGOZI DARAJA LA PILI KOZI 2025/26

🔴LIVE: RAIS SAMIA AKIHITIMISHA MAFUNZO YA UONGOZI NGAZI YA JUU, UONGOZI DARAJA LA PILI KOZI 2025/26

Nukta TV