Mambo ya kuzingatia kukabiliana na saratani katika hatua za awali

November 9, 2019 4:46 am · Joshua
Share
Tweet
Copy Link
  • Muone daktari kama unaona au kupata hali isiyo ya kawaida katika mwili wako hasa ngozi, koo, mdomo na matiti.
  • Saratani inaweza kutibika kwa urahisi iwapo dalili zake zitatambulika mapema. 

Mojawapo kati ya changamoto kubwa za kiafya inayosumbua na kuongoza kwa vifo vingi katika dunia ya kisasa ni saratani.

 Mara nyingi unaposikia ndugu ama rafiki ana saratani katika sehemu fulani ya mwili, hofu hutanda na mioyo huvunjika. Hii ni kwa sababu saratani husababisha maumivu makali na uwezekano wa kupona ni mdogo hasa kama imefika katika hatua mbili za mwisho. 

Kiuhalisia hakuna chanzo maalumu cha saratani ila kuna viambata mbalimbali ambavyo huitwa “carcinogens. Na hivi huusishwa na saratani katika mwili wa binadamu. 

Saratani haina dalili maalumu lakini hutegemea imetokea katika eneo gani la mwili. Dalili zilizozoeleka kwa watu ni kama kidonda chochote kisichopona kwenye ngozi kwa mda mrefu, mdomoni na hata kwenye ulimi. Kutokwa damu kusiko kuwa kwa kawaida katika naaeneo tofauti ya mwili.

Pia kupata uvimbe usio wa kawaida na wa muda mrefu katika maeneo ya matiti au sehemu yoyote katika mwili. 

Jinsia ya kutambua saratani mapema

Leo tutaangazia saratani za sehemu mbalimbali na jinsi unavyoweza kugundua mapema. Saratani inaweza kutibika kwa urahisi iwapo dalili zake zitatambulika mapema na kumuwezesha mhanga kupata tiba bora kadiri iwezekanavyo. 

Watu wengi hupata huduma wakati saratani iko katika hatua mbaya za (hatua ya tatu na nne) ambazo ni terminal stages (hatua za mwisho). Katika hali hii inakua ngumu sana kuitibu saratani kwani kiwango cha tatizo kinakuwa kimesambaa sehemu kubwa.

Uonapo dalili hizi katika maeneo mbalimbali ya mwili wako ni vema umuone daktari, huenda inaweza ikawa saratani:

Saratani ya ngozi. Uonapo uvimbe usio wa kawaida chini ya ngozi ambao hubadilika rangi au ukubwa na pembe zilizoinuka. Kidonda kisichopona au vidonda mithili ya upele. Ni vizuri kupata msaada wa kitabibu uonapo ili kupata uhakika wa hali yako ulionayo.

Hata hivyo, siyo kila uonapo dalili hizi unaweza kuwa na saratani. La hasha!, bali ni muhimu kuzingatia dalili hatarishi ambazo iwapo zikipuuzwa huleta madhara. Picha|Mtandao.

Saratani ya mdomo.  uonapo vidonda sugu vya mdomo (chronic ulcers) ambavyo haviponi, kwenye koo ama kwenye ulimi. 

Saratani ya koo la hewa na mapafu. Kikohozi sugu kiambatanacho na sauti ya kukwaruza, maumivu ya kifua pamoja na makohozi yenye damu. 

Saratani  ya matiti. Uvimbe usioopotea, mgumu na hausogezeki. Kuvimba au kuwasha kwa ngozi ya titi. Hii inaweza kuwa dalili ya saratani hiyo. 

Saratani ya damu. Ngozi kuwa nyeupe, kupoteza uzito kusikoelezeka, kuchoka na maambukizi kila mara, kuchubuka kirahisi na kutokwa damu puani.


Soma zaidi: 


Saratani ya kibofu na figo. Damu kwenye mkojo na kukojoa mara kwa mara. Damu kwenye mkojo siyo dalili hasa ya saratani lakini yaweza kuwa. Maumivu upande wa juu wa kushoto au kulia wa tumbo.

Saratani ya tezi dume na korodani. Uvimbe au maumivu kwenye korodani. Maumivi ya nyonga na kushindwa kukojoa vizuri.

Saratani ya shingo ya kizazi. Hii inaweza kuwa kwa kutokwa damu kusikokuwa kwa kawaida katikati ya hedhi. Kutokwa na uchafu usio wa kawaida au majimaji ukeni. Hedhi zenye maumivu kupita kiasi au kutokwa damu kupita kiasi wakati wa hedhi.

Hata hivyo, siyo kila uonapo dalili hizi unaweza kuwa na saratani. La hasha!, bali ni muhimu kuzingatia dalili hatarishi ambazo iwapo zikipuuzwa huleta madhara. 

Ni vyema kufanya vipimo mara kwa mara ili kutambua hali yako halisi ya afya hasa uonapo dalili ambazo unazitilia mashaka.

Enable Notifications OK No thanks