Mambo muhimu yatakayozisaidia kampuni zinazochipukia Tanzania kukua
- Kuwa na mawazo ya kibunifu yanayolenga kutatua changamoto za wananchi wa kawaida katika jamii ili kuwatengenezea tija ya maisha.
- Kuwa wavumilivu na kutokukata tamaa ya kufanya mambo makubwa yanakusudia kuleta matokeo chanya katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Dar es Salaam. Washiriki wa kongamano la ujasirimali la Seedstars Africa Summit wameeleza mambo mbalimbali yatakayosaidia kampuni zinazochipukia (Startups) za Tanzania kukua na kuimarika ikiwemo kuwa na mawazo ya kibunifu na kutumia teknolojia rahisi katika kutatua changamoto za jamii.
Kongamano hilo la siku tano limehitimishwa juzi (Desemba 13, 208) jijini Dar es Salaam ambapo liliwakutanisha wajasiriamali, wabunifu na wawekezaji kutoka nchi za Afrika kubadilishana uzoefu katika kutumia teknolojia na rasirimali zilizopo kuleta matokeo chanya katika jamii na kuboresha maisha ya wananchi.
Katika kuhakikisha vijana wabunifu wanaoanzisha startups wanaifikia jamii kwa upana, wamepewa changamoto mbalimbali zitakazowasaidia kukuza shughuli zao ikiwemo;
Mawazo ya kibunifu yanayolenga kutatua changamoto za jamii
Kongamano hilo ambalo kwa sehemu kubwa lilijikita katika kubadilishana uzoefu wa jinsi ya kutengeneza mifumo ya teknolojia, vijana wametakia kuongeza ubunifu na mawazo chanya yanayolenga moja kwa moja kutatua changamoto za kijamii za wananchi wa kawaida.
Mkurugenzi Mtendaji wa jukwaa la GovChat.Org, Eldrid Jordaan ambaye alikuwa mzungumzaji katika kongamano hilo, amesema vijana wanapaswa kuwa programu zinazolenga kuwaunganisha viongozi na wananchi kama wanavyotumia jukwaa lao kuwakutanisha viongozi na wananchi jambo linaloondoa pengo la upatikanaji wa taarifa muhimu za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Ni platform (jukwaa) muhimu linalowakutanisha wananchi na viongozi wa Serikali kujadiliana mambo ya msingi katika jamii lakini ni sehemu muhimu ya watu kubadilishana mawazo,” amesema Jordaan.
Zinahusiana:
- Apple yaingiza sokoni simu mpya zinazotumia mfumo wa ‘eSIM’
- Vodacom, Google wazindua manunuzi ya ‘Apps’ kwa njia ya simu
- Usiyoyajua kuhusu mtandao wa 5G
Uvumilivu na kutokukata tamaa ya kufanya mambo makubwa
Akielezea safari yake wakati anaanzisha jukwaa la elimu la Ubongo Kids, Doreen Kessy amesema haikuwa rahisi kubuni na kuhakikisha ndoto yake ya kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa kutumia njia rahisi ili kutatua changamoto ya uhaba wa walimu na vitabu shuleni.
Changamoto aliyokutana nayo ni kukatishwa tamaa na watu kuwa App hiyo isingeweza kukua kutokana na mazingira ya elimu ya Tanzania ambapo wanafunzi wengi bado hawajafikiwa na teknolojia ya mawasiliano na habari hasa matumizi ya intaneti.
Lakini alipiga moyo konde, na sasa amesimama na anasonga mbele katika kutenegeneza katuni za 3D zinazowasaidia wanafunzi kujifunza haraka na kupata maarifa popote walipo wakati wakisubiri kuboreshewa mazingira ya kujifunzia shuleni.
“Somo tunalojifunza katika mazingira magumu ni kuwa wa kweli. Sio jambo ambalo mara nyingi linakuja tu; kuwa wewe na fuata njia yako ya mafanikio,” amesema Doreen.
Washiriki wa Kongamano la ujasirimali la Seedstars Africa Summit walikuwa na bashasha la aina yake baada ya kujumika pamoja. Picha|K15.
Uwazi na maamuzi magumu
Wakati mwingine startups zinashindwa kukua kwasababu ya kukosa uwazi wa majukumu wanayotekeleza kwa jamii. Uwazi unasaidia kuongeza uwajibikaji miongoni mwa waanzilishi na hata kuvutia wawekezaji ambao wanaweza kuwekeza fedha ili kuifikia jamii kwa upana zaidi.
Akizungumza katika kongamano hilo, mshiriki Marcello Scherme kutoka Afrika Kusini amesema uwazi unafungua fursa mbalimbali za kupata msaada wa kuboresha kazi na kukutana na watu wenye uzoefu wa kutatua changamoto za teknolojia na uvumbuzi wa fursa za kibiashara.
Sambamba na hilo ni kufanya maamuzi magumu (Risk taking) ya kutumia rasimali zinazowazunguka katika jamii ili kufanya vitu visivyo kawaida na kuleta matokeo chanya katika shughuli za maendeleo.
Wawekezaji na watu wa kushirikiana nao
Startup yoyote ili ukue inahitaji watu wenye ujuzi na maarifa ya kutumia teknolojia rahisi inayoeleweka na watu wanaokusudiwa. Hili linaenda sambamba na kujenga timu imara yenye uwezo wa kuvutia wawekezaji kufadhili miradi mbalimbali inayobuniwa.
“Katika makosa ambayo waanzilishi wanafanya katika bara hili (Afrika) ni kutokuandaa mikakati ya harambee, kutokuwepo kwa mipango ya fedha na kutokuelewa lugha ya wawekezaji,” amesema Eveline Buchatskiy kutoka kampuni ya One Way Venture ya nchini Uturuki.
Awali akitoa ufafanuzi wa shughuli za taasisi ya Seedstars World ambao ni waandaaji wa kongamano hilo, Meneja wa taasisi hiyo kanda ya Afrika, Claudio Makadristo amesema wataendelea kuziwezesha na kuzijengea uwezo startups za Africa ili ziwe sehemu ya kuboresha maisha wananchi wa bara hilo wanaokabiliwa na tatizo la umaskini.
“Tunafadhili na kuendeleza startups zinazoibukia kwenye soko kwa kuziunganisha na wawekezaji na makocha waliobobea katika ujasiriamali,” amesema Makadristo.
Katika kongamano hilo, kampuni inayochipukia ya NALA imechaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia yatakayozikutanisha startups zaidi ya 80 kutoka nchi mbalimbali nchini Uholanzi mapema Aprili 2019.