Mambo muhimu ya kuzingatia katika mfungo wa Ramadhan

March 23, 2023 5:33 am · Zakia
Share
Tweet
Copy Link
  • Kipindi cha mfungo wa Ramadhan kunakuwa na mabadiliko mengi katika mfumo wa maisha na matendo ya watu.
  • Katika kipindi hicho watu hufanya zaidi ibada na kujiepusha na matendo maovu.
  • Mfungo wa Ramadhan mwaka huu umeanza leo Machi 23. 

Dar es Salaam. Kwa kufuata kalenda ya Kiislamu, Ramadhan ni mwezi wa tisa na Waislamu duniani kote huutukuza mwezi huo kwa kufunga na kufanya ibada. Na ndiyo mwezi ambao Quran tukufu iliteremshwa.

Waislamu Tanzania na ulimwenguni kote wanategemea kuanza mfungo wao wa mwezi mtukufu wa Ramadhan rasmi Alhamisi, Machi 23, 2023.

Kufunga wakati wa mwezi huu mtukufu ni mojawapo wa nguzo tano za Kiislamu ambazo kila muumini hutakiwa kuzitimiza katika maisha yake.

Katika mwezi huu, Waislamu hufunga kati ya siku 29 au 30 kulingana na kuandama kwa mwezi kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu.

Kipindi cha mfungo wa Ramadhan kunakuwa na mabadiliko mengi katika mfumo wa maisha na matendo ya watu.

Dhamira siyo tu kuacha kula chakula na maji, lakini kutumia muda huo kujikumbusha manufaa ya kujiepusha na mambo yanayokatazwa, mfano hasira, kugombana, vita, kijicho, matamanio na zinaa, masimango, kusengenya na kusema uongo.


Ni lazima kufunga?

Wakati waumini wote wanajizuia kula na kunywa katika kipindi hiki, wapo wanaoruhusiwa au wasioshurutishwa kufunga kwa sababu tofauti.

Wazee wasiojiweza wameruhusiwa kutofunga au hata wale wanaofunga kwa tabu pia wana hiari ya kuacha kufunga katika mwezi wa Ramadhan.

Pia kwa mwanamke wa Kiislamu anayefunga anatakiwa kuvunja swaum yake punde anapoingia katika hedhi au anapovuja damu ya uzazi (Nifas).

Wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wanaweza kutofunga katika Ramadhan, iwapo wanahisi watakuwa wanahatarisha afya zao au za watoto wao.

Hata hivyo, iwapo mwanamke mjamzito anajihisi kuwa na afya nzuri na nguvu na kwa ushauri wa daktari wake anaweza kuendelea na swaum yake.

Kufunga wakati wa mwezi huu mtukufu ni mojawapo wa nguzo tano za Kiislamu ambazo kila muumini hutakiwa kuzitimiza katika maisha yake. Picha | istock.

Wagonjwa wazingatie hili

Wakati mtu anapokuwa katika hali ya afya isiyo nzuri ikiwemo magonjwa ya kudumu na ya muda mrefu naye haruhusiwi kufunga. Hata hivyo, atatakiwa kulipia fidia ya kila siku ambayo hawakufunga maarufu ‘kibaba’.


Ukifanya haya, swaum yako inatenguliwa

Wakati watu wanaendelea na mfungo kuna baadhi ya mambo yakifanyika yanaweza kutengua swaum zao hivyo kutoendelea kufunga.

Mambo hayo ni kama kula na kunywa kwa makusudi. Na sio kwa kusahau wala kwa bahati mbaya au kwa kulazimishwa, katika mchana wa swaum.

Kujitapisha kwa makusudi. Kuwe kujitapisha huko kwa kutia kidole mdomoni au kunusa kitu kitachosababisah kutapika.

Pia mume akimwingilia mke wake ama kumkumbatia au kumchezea hadi “yakamtoka manii” mchana wa mwezi wa Ramadhani, huyo funga yake itakua haina maana. 

Mwenye kutia nia ya kula wakati amefunga, kwa sharti kuwa kaazimia tendo hilo hata kama hakulitekeleza, na kudhania kuwa jua limezama Magharibi au bado hakujapambazuka (yaani haujaanza wakati wa kufunga), kisha anayefunga akala, akanywa au akamuingilia mke wake. 


Soma zaidi:


Vipi kuhusu uongo kwenye swaum? 

Kauli maarufu ya Mtume juu ya hilo inasema “yeyote ambaye hawezi kuacha maneno ya uongo na kuufanyia kazi uzushi, basi Mwenyezi Mungu hana haja naye yeyote ya kuacha chakula chake na maji yake.”

Wasomi wa Kiislamu wanatafsiri kauli hiyo kuwa uongo na uzushi haubatilishi swaum bali unapunguza thamani ya funga ya mtu.

Imezoeleka watu hupeana hamasa kutenda mambo mema wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, baada ya hapo wengi hurejea kwenye maisha ya kawaida ya kutenda yale yanayozuiwa kidini na hata kiutamaduni. Wewe ni miongoni mwa hao? 

Enable Notifications OK No thanks