Wagonjwa wa kisukari wanavyoweza kushiriki mfungo wa Ramadhan

April 19, 2021 6:19 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuhakikisha wanapima kiwango cha sukari kabla ya kufunga. 
  • Wakati wa kufuturu, wanashauriwa kutokula vya matunda na mboga mboga.
  • Wasioweza kufunga, wanatakiwa kufanya matendo mema.

Dar es Salaam. Ni siku kadhaa zimepita tangu kuanza kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa waamini wa dini ya kiislamu. Waumini hufunga ili kutimiza nguzo muhimu ya dini hiyo.

Hata hivyo, wapo baadhi ya waumini wanashindwa kukamilisha kikamilifu funga kutokana na changamoto za kiafya na hivyo kubaki katika sintofahamu wafanye nini. Lakini suluhuhisho limepatikana kwa ajili yao. 

Mfungo wa Ramadhan,  kwa mujibu wa muumini wa dini ya Kiislamu, Mikidadi Mchau ni kipindi ambacho Waislamu hukitumia kusogea karibu na Mungu na kutenda yaliyo mema. Katika kipindi hicho muamini wa dini hiyo hufunga kwa siku 30.

“Swaumu inaanza kabla ya swala ya asubuhi mpaka muda wa swala ya magharibi (jioni). Ni muda ambao jua limezama,” amesema Mchau, mkazi wa jijini Dar es Salaam akielezea kuwa mfungo huo hudumu kwa takriban saa 15 kwa siku.

Hata hivyo, kwa waumini ambao wanakabiliwa na changamoto za kiafya ikiwemo ugonjwa wa kisukari, wanaweza kuogopa kushiriki katika mfungo huo ambao kwa mkazi wa Dar es Salaam, Abdul Makai  anasema ni “mwezi wa toba, mwezi wa kushukuru na kusamehe.”

Inashauriwa kuonana na daktariili kupata vipimo vya afya yako na hali ya kisukari kabla ya kuamua kuingia katika mfungo. Picha| Dawn.

Mtaalamu wa masuala ya afya kutoka Hospitali ya Shree Hindu Mandal ya Dar es Salaam, Dk Frank John ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz)  kuwa mgonjwa wa kisukari anatakiwa kuzingatia mambo matatu muhimu ambayo ni lishe, mazoezi na kunywa dawa.

Mtaalamu huyo amesema, kabla ya kuamua kushiriki katika mfungo, inashauriwa mgonjwa aonane na daktari kwa ajili ya vipimo vya kutambua hali ya afya yake. 

Majibu ya vipimo vyake yataamua kama kwa hali yake ya kiafya, anaruhusiwa au haruhusiwi kufunga.

Kwa ambao wataruhusiwa na daktari wao kufunga, Dk John amesema lishe yao huhitaji kuwa na mboga mboga kwa wingi, vyakula vilivyo na protini na wanga kidogo sana. 

“Mgonjwa anatakiwa afanye mazoezi walau kwa nusu saa kwa siku atoke jasho ili kusaidia shughuli za uendeshaji mwili. Pia, anatakiwa kutumia dawa kulingana na dozi husika ya mtu,” amesema Dk John.

Licha ya kuwa kuruhusiwa kufunga wanatakiwa kupima mara kwa mara kiwango cha sukari mwilini kama imeshuka au la! . Hii itawasaidia kuepuka mashara ya kiafya. 

“Ni muhimu kuwa makini unapofunga na kujua dalili za sukari kushuka zaidi na kua na kipimo cha kucheki sukari unapohisi imeshuka,” amesema daktari huyo.


Soma zaidi:


Wakati wa kufungua ufanye nini?

Tovuti ya masuala ya afya ya TanzMed imeandika, mgonjwa wa kisukari hashauriwi kufuturu vyakula vya wanga kwa wakati mmoja bali anashauriwa kula matunda ikiwemo tende kila anapofuturu.

Zaidi, inashauriwa kabla ya kula futari au daku, mgonjwa ajipime kiwango cha sukari saa mbili kabla ya chakula na pia asitumie chakula kizito.

Kama hali yako ya afya siyo njema unaruhusiwa kutokufunga lakini unatakiwa kuzidisha kufanya matendo mema kwenya jamii.

Enable Notifications OK No thanks