Mambo muhimu unayoweza kufanya ukifika Mwanza
- Ni kutembelea vivutio vya utalii ikiwemo sanamu ya samaki.
- Kituo cha Makumbusho Bujora nacho kitakuvutia.
- Kwa watalii, hifadhi ya Taifa ya Saanane ndiyo habari ya mjini.
Mwanza. Huenda una mpango wa kutembelea Mkoa wa Mwanza hivi karibuni kwa shughuli za kikazi au biashara, lakini unajiuliza wakati wa mapumziko ni maeneo gani unaweza kwenda.
Kwa hilo ondoa shaka, maana nitakusogeza katika maeneo muhimu ambayo yamekuwa yakitumiwa kama vivutio vya utalii kwa wageni wanaotembelea mkoa huo.
Licha ya mkoa huo kujaliwa muonekano mzuri wa kijiografia ikiwemo milima, mawe makubwa na mandhari nzuri ya Ziwa Victoria, usiache kutembelea maeneo haya ukiwa Mwanza:
Jiwe la Bismarck Rocky
Hili ni nembo au ramani inayoutambulisha Mkoa wa Mwanza. Jiwe hili maarufu lipo ndani ya Ziwa Victoria eneo la Kamanga Feri ambapo kwa kulitazama utaona mawe yake yalivyojipanga ni kama kuna mtu aliyapanga na kuufanya mwonekano wa jiwe hilo kuwa wa kupendeza.
Jiwe hilo lililopewa jina la kansela wa kwanza kabisa wa Ujerumani Otto Von Bismarck ndiyo mlango kwa wageni wanaoingia mkoani humo.
Watu hupenda kutembelea eneo hili kupiga picha na hata maharusi hupenda kwenda kupiga picha kwenye eneo hili.
Jiwe hilo ni utambulisho wa kwanza kwa wageni wanaoingia Mwanza. Picha| MwanzaCampusConnect.
Kituo cha Makumbusho cha Bujora
Asilimia kubwa ya wenyeji wa Mkoa wa Mwanza ni wa kabila la Wasukuma. Mila na tamaduni za kabila hili huwavutia wengi hasa kutokana na michezo yao ya kucheza ngoma na nyoka aina ya chatu.
Mbali na michezo hiyo pia wanazo tamaduni nyingi za kupika chakula kama ugali wa mhogo, ufugaji wa ng’ombe na hata wanao machifu ambao ndiyo viongozi wa mila hiyo.
Na katika kulitambua hilo, Serikali ilijenga kituo hicho ambacho kipo barabara ya Musoma eneo la Kisesa ambapo ni mita chache tu kutoka katikati ya kisesa kuelekea Bujora.
Hapo utapata taarifa zote za mila, utaduni na historia ya Mwanza. Utaachaje kufika hapo kujionea utajiri wa mkoa huo?
Sanamu ya samaki
Hii ni sanamu imetengenezwa na kuwekwa katikati ya jiji la Mwanza katika makutano ya barabara za Kenyatta na Stesheni jijini hapa. Sanamu hii imechorwa ili kutambulisha utajiri wa samaki aina ya sangara na sato wanaopatikana ndani ya Ziwa Victoria.
Samaki hawa ni watamu kwa kuwa wanapatikana kwenye maji baridi na ni tofauti na samaki wanaopatikana kwenye maeneo mengine. Watu wanaotoka mikoani kuja Mwanza wanakaribishwa na kitoweo cha samaki.
Mbali na hilo pia kuna utajiri wa dagaa na maji yasiyokuwa na chumvi.
Sanamu ya samaki huyo imekuwa kivutio kikubwa kwa wageni wanaotembelea Mkoa wa Mwanza. Picha| G Sengo.
Hifadhi ya Taifa ya Saanane
Hiki ni kivutio kingine ambacho huwavutia watalii wengi. Ukiacha mbali hifadhi nyingine kama Serengeti na Mikumi, hifadhi hii ni ya aina yake kwanza ni mbuga inayopatikana mjini yaani ndani kabisa ya jiji la Mwanza.
Hifadhi hiyo ina wanyama wakipekee kama vile tumbili weusi ambaye anapatikana pekee hifadhini hapo. Wengine ni swala, pundamilia, chatu, ndege aina mbalimbali, simba, mamba, fisi maji, samaki aina ya sato (tilapia) na samaki wengineo.
Ziwa Victoria ni sehemu ya kivutio cha hifadhi hii huku mtalii akipata fursa ya kutazama mawio ya jua na muda wa jioni ambapo ziwa hilo hutoa nafasi ya pekee kuona mandhari hii.
Shughuli za utalii zinazoweza kufanyika hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane ni kukwea miamba, kutazama ndege, utalii we kutembea kwa miguu, kupiga makasia kwa kutumia mitumbwi, kutalii kwa kutumia boti pamoja na uvuvi wa kimichezo.
Latest