Mambo 10 ya kuyafahamu kabla ya kuanza kufuga kasuku

November 15, 2021 11:14 am · Nasibu
Share
Tweet
Copy Link
  • Kasuku hachagui sana msosi, anakula karibu kila kitu.
  • Anapenda kupiga domo japokuwa yeye hana uwezo wa kuongea.

Baada ya mbwa, paka na samaki basi ni kasuku ndiye kiumbe anayeongoza kwa kufugwa majumbani.

Kwa miaka mingi, ndege kasuku amekuwa kivutio kwa binadamu  kutokana na sifa zake za kipekee.

Miaka hivi ya karibuni, tafiti zimegundua kuwa jumla ya idadi ya ndege millioni 14 wanaishi kama mateka nchini Marekani na ndege hao wanasemekana kutoka mabara tofauti na zaidi ya asilimia 50 ya ndege hao ni kasuku.

Kasuku yupo tofauti na viumbe wengine wa kufugwa na anaweza kukupa changamoto usizozitegemea kwa sababu ndege huyu huishi miaka mingi na ana uwezo mkubwa wa akili. 

Hivyo basi makala hii itakusaidia wewe ambaye una matamanio ya kumfuga ndege huyu mpiga domo.

Kuna aina nyingi za kasuku

Kuna aina takribani 350 za kasuku duniani wenye rangi za tofauti za kuvutia kama bluu, njano, kijani, nyeupe, nyeusi na nyekundu. Barani Afrika, kasuku wa kijivu ndiyo hupatikana kwa wingi.

Kasuku hachagui sana msosi

Kasuku ana mdomo uliyojikunja kuelekea chini kama mundu na anakula chochote anachokutana nacho kuanzia nyasi, matunda, mbegu, majani, maua mpaka nyama. Cha msingi ujue kasuku wako anapendelea nini haswa ili umpe hicho kwa wingi.

Ndege hawa wana akili nyingi huwa na rangi tofauti tofauti ambazo huvutia sana. Picha| Pinterest.

Kasuku wengi hutekwa

Robo tatu ya kasuku wote duniani wapo kwenye hatari ya kupotea kwenye uso wa dunia kwa sababu ya shughuli za binadamu za ukataji miti na biashara haramu ya kusafirisha na kuuza wanyama. 

Kwahiyo, ishi naye vizuri, fanya maisha yake yawe mazuri, muweke kwenye banda kubwa ajiachie kidogo.

Jike au dume?

Ni ngumu sana kutofautisha kasuku dume na jike, wanafanana asilimia 99.9. Pata ushauri wa kitaalamu kabla ya kufungua pochi, usije ukanunua kasuku mtaani ukajikuta una madume mawili yanatazamana humo bandani.

Ulimi wake wa ajabu kidogo

Kasuku ana ulimi ambao hautumii kuonja chakula, kazi ya kuonja chakula hufanywa na upande wa juu wa ndani ya mdomo.


Soma zaidi:


Kasuku hata siyo mzito

Kasuku anaweza kuwa na uzito wa kuanzia gramu 60 mpaka kilo moja na nusu tatu kwa wastani.

Kasuku anakula chumvi!

Kasuku anaweza kuishi hadi miaka hamsini, na kasuku mzee kuliko wote ana miaka 82 na anaishi kwenye zoo iitwayo Brookfield iliyopo mjini Chicago, nchini Marekani. 

Unapoamua kufuga kasuku basi kaa ukifahamu kwamba kuna umuhimu wa kuandika mirathi maana ya Mungu mengi na hiyo miaka 50 ni mingi kweli kweli.

Kasuku anajikinga

Manyoya ya kasuku yana kinga dhidi ya bakteria. Kinga ambayo huwapa manyoya yao rangi nyekundu, kijani na njano.

Kasuku ni mdogo kwa umbo lakini una uwezo wa kukariri sauti za watu na baadaye kuziimba. Picha| East Coast Daily English.

Hachelewi kuhama kambi

Kasuku huhama pale hali ya hewa inapobadilika kutafuta malisho. Hata kama nyumbani kwako kuna vitu asivyovipenda, usishangae siku moja hujafunga banda vizuri, anaondoka na hutomuona tena.

Kasuku anapiga domo!

Kasuku anapenda sana kupiga domo japokuwa yeye hana uwezo wa kuongea bali ana uwezo wa kukariri maneno yanayosemwa na mwanadamu, hivyo basi kuwa mwangalifu na maneno uyasemayo maana ipo siku atayarudia tu mbele ya wageni.

Kasuku anayeshikilia rekodi ya dunia ya kujua maneno mengi alikariri maneno 1,700.

Ushauri: Kama unapenda muziki, basi sikiliza kwa sauti ili na yeye asikie kwa sababu ipo siku atakupa remix na karaoke zake mpaka nafsi yako itafurahi. 

Nikutakie ufugaji mwema. Bye.

Nasibu Mahinya ni mjasiriamali na Afisa Masoko wa soko la mtandaoni la utalii la TenTen Explore nchini Tanzania. Amekuwa mdau muhimu wa shughuli za utalii zinazofanyika ndani na nje ya Hifadhi za Taifa. Unaweza kumpata kupitia tovuti yake ya www.nasibumahinya.com.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks