Makosa ya uhalifu wa kifedha yaliyotikisa mwaka 2018

August 27, 2019 8:07 am · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Makosa hayo ni pamoja na kughushi, kutengeneza fedha bandia na wizi wa fedha kwenye benki na mashirika ya umma.
  • Hata hivyo, makosa  ya uhalifu wa kifedha yamepungua kutoka makosa 1,640 mwaka 2017 hadi makosa 1,303 mwaka jana.

Dar es Salaam. Licha ya takwimu kuonyesha matukio ya uhalifu wa kifedha kupungua Tanzania katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, yapo baadhi ya matukio hayo likiwemo la utengenezaji wa fedha bandia yaliyotikisa mwaka 2018.

Uhalifu wa kifedha unahusisha makosa mbalimbali ya kijipatia fedha kwa njia isiyo halali ikiwemo ya kugushi, utengenezaji fedha bandia na wizi fedha kwa njia ya mtandao ambao ni kinyume cha sheria.

Baadhi ya makosa hayo yanashughulikiwa na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka 2015. 

Kwa mujibu wa ripoti ya Takwimu muhimu za mwaka 2018 (Tanzanian Figures 2018) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha kuwa makosa  ya uhalifu wa kifedha yamepungua kutoka makosa 1,640 mwaka 2017 hadi makosa 1,303 mwaka jana.

Hiyo ni sawa na kusema makosa hayo yamepungua kwa asilimia 20.5 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Haya ni baadhi ya makosa yaliyohusisha uhalifu wa kifedha yaliyotikisa kwa mwaka 2018:

Makosa ya Kugushi

Makosa ya kugushi nyaraka ili kujipatia fedha isivyo halali pesa ni miongoni mwa makosa yaliyoshuhudiwa katika katika sekta ya fedha mwaka jana.  

Makosa ya kughushi yalipungua kwa asilimia 9.4 kutoka 1,114 mwaka 2017 hadi 843 mwaka jana. 

Hata hivyo, ndiyo aina ya uhalifu wa kifedha ambao ulirekodiwa kuwa na kiwango cha juu ukilinganisha na makosa mengine yaliyotajwa katika ripoti ya NBS. 


Soma zaidi: 


Utengenezaji wa fedha bandia

Utengenezaji fedha bandia ni uhalifu mwingine ambao umekua ukijitokeza katika jamii unaohusisha kutengeneza fedha zenye muonekano sawa na zile halali lakini zikiwa na mapungufu mbalimbali. 

Mwaka jana pekee kulikuwa na makosa 340 ikiwa yamepungua kutoka makosa 405 yaliyorekodiwa mwaka 2017.

Wizi fedha kwenye mashirika ya umma

Makosa ya wizi wa fedha ambao ripoti hiyo imeutaja ni yale yaliyojitokeza katika mashirika ya umma (Parastatals) ambapo mwaka jana kulikuwa na makosa 83 ukilinganishwa na 54 yaliyorekodiwa mwaka 2017. 

Hata hivyo, takwimu hizo zinaonyesha kuwa makosa hayo yamekuwa yakipungua kila mwaka katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Mathalani, mwaka 2016 kulikuwa na makosa 90 kabla hayashuka hadi 54 mwaka 2017.

Wizi wa fedha Serikali za mtaa

Ripoti hiyo inaeleza kuwa makosa ya wizi wa fedha Serikali za mitaa ambayo huusisha mamlaka zilizopo Halmashauri za Wilaya, vijjiji, kata na tarafa yaliongezeka kidogo kwa mwaka mmoja uliopita. 

Mwaka 2017 kulikuwa na makosa 19 lakini mwaka uliofuata wa 2018 makosa 20 yalirekodiwa.

Wizi wa fedha Serikali Kuu

Makosa ya wizi wa fedha yaliyohusisha Serikali Kuu, kwa mwaka jana yalikua 10 ambapo yameongezeka kutoka 6 mwaka 2017. 

Makosa mengine ya wizi wa fedha yaliyotajwa kwenye ripoti hiyo ni pamoja na wizi uliotokea kwenye vyama vya siasa na wafanyakazi na uvamizi wa taasisi za fedha kama benki.  

Makosa ya fedha zilizoibwa kwenye vyama vya wafanyakazi kwa mwaka jana yalikuwa saba yakiwa yameporomoka kutoka 40 yaliyorekodiwa mwaka 2017. 

Hiyo ni sawa na kusema ndani ya kipindi cha mwaka mmoja makosa ya wizi wa fedha katika vyama hivyo, vinavyotetea haki za wafanyakazi yamepungua kwa zaidi ya mara tano. 

Enable Notifications OK No thanks