Makosa unayotakiwa kuepuka wakati unatumia simu yako
- Makosa hayo ni pamoja na kuchaji simu usiku kucha na kutumia chaja isiyokuwa ya simu yako.
- Makosa mengi hupelekea kuharibika kwa betri na hata vifaa vingine vya simu.
- Ni muhimu kukubali kuingia gharama kununua vitu thabiti kuliko kununua vitu feki na kupata gharama ya matengenzo.
Dar es Salaam. Kila kitu kinapotengenezwa kinaambatana na maelezo muhimu ya kuzingatia ili kitumike kwa usahihi.
Hata hivyo, kutokana na haraka, mazoea na wakati mwingine kutokufahamu, watu wengi wamekuwa wakifanya makosa katika matumizi ya simu zao ikiwemo kuchaji simu na hata uhifadhi wa chaja za simu zao isivyotakiwa.
Unafahamu kuwa utunzaji wa simu yako ndio kitu pekee kinachoweza kuifanya idumu kwa muda mrefu?
Kama wewe ni mtumiaji wa simu, basi hivi ni baadhi ya vitu ambavyo umekuwa ukikosea kuvifanya wakati ukitumia simu yako na huenda meingia gharama zisizo za lazima na kukupunguzia unene wa mfuko wako:
Kuchaji simu yako
Ni mara ngapi umechomeka simu yako kwenye chaji na kisha ukavuta shuka lako kulala?
Watu wengi husahau kuwa simu nyingi hujaa ndani ya saa mbili hadi tatu na hivyo kwa mtu anayelala saa nne usiku na kuamka saa 11 asubuhi basi huchaji simu yake kwa saa tano zaidi.
Kwa mujibu wa tovuti ya Battery University, hali hiyo huchangia kulichosha betri lako kwani baada kufikia asilimia 100 na kutochomolewa ni sawa na mtu anapokuwa ameshiba lakini akaendelea kupewa chakula.
Siyo dhambi kuichaji simu yako ikiwa na asilimia 50 au hata ikiwa na asilimia 30 lakini ni dhambi kwa simu kuitumia hadi ifike asilimia sifuri bila sababu maalumu. Picha|Steve Johnson/Unsplash
Kutumia simu yako hadi izime
Huenda ulidhani ni vizuri kuchaji betri lako hadi asilimia 100 na kutumia chaji yako hadi pale iishapo kabisa yaani hadi asilimia sifuri. Wataalamu wanasema kwa mabetri ya “Li-ion” ambayo yanatumika kwenye simu nyingi, hayafurahii kuwekwa kwenye chaji kwa msimu mrefu baada ya kuishiwa chaji kabisa.
Mtandao wa xfinit unaeleza kuwa kila simu ina maisha yake. Kwa simu za iPhone unaweza kuichaji mara 500 tu endapo utakuwa ukiitumia hadi kufikia asilimia sifuri.
Hivyo, watumiaji wanashauriwa kuichaji simu pale wanapoweza ili kuepuka kuishi na simu zao kwa siku 500 tu.
Mabetri haya ni kama alivyo mtoto mdogo yaani kwa kipindi cha mchana, unatakiwa kumpa uji kidogo, maziwa kidogo, sharubati kidogo na siyo kusubiria hadi asikiapo njaa.
Siyo dhambi kuichaji simu yako ikiwa na asilimia 50 au hata ikiwa na asilimia 30 lakini ni dhambi kwa simu kuitumia hadi ifike asilimia sifuri bila sababu maalumu.
Unapokuwa ofisini, ni vyema ukaiweka simu yako kwenye chaji mara kwa mara na kwa mujibu wa Battery University haitaua betri lako kama ambavyo unaiweka simu yako kwenye chaji ikiwa na asilimia sifuri na kisha kuiwasha na kuendelea kuitumia.
Soma zaidi:
- Jinsi ya kufanya mitandao ya kijamii isikuharibie mahusiano yako
- Mbinu tano za kudhibiti matumizi makubwa ya intaneti kwenye ‘smartphones’
Kuacha intaneti wazi endapo huitumii
Kila kitu kilichowekewa uwezo wa kuzimwa na kuwashwa kina sababu yake. Basi ni kwanini uache intaneti ikiwa imewashwa usiku kucha na hauitumii?
Wadau wa teknolojia wanashauri kuzima intaneti kwani kwa kuiacha unafupisha maisha ya betri yako na huenda simu yako ikapata hitilafu ya kuanza kuchemka kutokana na kutumika kwa muda mrefu.
Unapoacha intaneti ikiwa imewashwa, unatoa ruksa kwa programu mbalimbali zikiwemo za “location” na programu tumishi kama WhatsApp kuendelea kufanya kazi hata kama huzitumii.
Programu hizo hutafuna kifurushi cha intaneti na kukufanya uvunje kibubu kila siku bila kujua. Njia rahisi ya kuzuia matumizi hayo yasiyo ya lazima ni kuzima data wakati unalala au huna matumizi nayo hata kama ni mchana.
Kuchaji simu yako baada ya kuinunua
Wakati uvumi wa kwamba ni lazima unaponunua simu uichaji bila kuitumia ukiendelea kusambaa kwa wadau wa teknolojia hiyo, Mhandisi na mdau wa matengenezo ya simu na bidhaa za kielektroniki, Brad Nichols amefafanua zaidi.
Amesema ushauri huo hutolewa ili kumpatia mtumiaji “experience” (mtazamo) nzuri na simu yake mpya kwani kila mtu anayenunua simu hutarajia walau simu idumu na chaji kwa muda wa saa nane.
Kwa simu mpya, nusu ya chaji yake huishia kwenye majaribio wakati wa matengenezo. Hivyo wengi wanashauri hivyo ili mtu anunuapo simu apate “experience” mzuri wa simu yake lakini siyo kuchaji simu mara baada ya kuitumia.
Kila kitu kilichowekewa uwezo wa kuzimwa na kuwashwa kina sababu yake. Basi ni kwanini uache intaneti ikiwa imewashwa usiku kucha na hauitumii?. Picha|Laura Highgrace/Unsplash.
Kutumia chaji feki
Ili kukwepa gharama, watu wengi hupotezea kununua chaja halisi za simu zao pale zinapoharibika ama kupotea. Wengi hujikuta wakinunua chaja za bei rahisi ambazo matokeo yake ni uharibifu wa betri unaosababishwa na kutokuwepo na uwiano wa betri na chaja.
Wadau wa teknolojia wanashauri pale chaja yako inapoharibika, ni vema ukatafute chaja ya simu hiyo. Unaweza kuagizia matandaoni au kutembelea duka rasmi la simu yako.
Kwa kufanya hivyo, utaweza ongezea maisha ya betrii la simu lako.
Makala hii ni mfululizo wa dondoo ya mambo ambayo umekuwa ukikosea kuyafanya. Leo umepata dondoo kwenye nyanja ya teknolojia ya simu, endelea kusoma tovuti hii kwa dondoo zijazo.