Makalla atatua mgogoro wa kituo cha hijja Kageye, Mwanza
- Ni mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka mitano
- Sasa waumini waruhusiwa kuandelea na ibada taratibu za umiliki zikiendelea kufanyiwa kazi
Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla ameutatua mgogoro wa kituo cha hija cha Kageye, uliokuwepo kati ya Kanisa Katoliki Parokia ya Kagaye na Halmashauri ya Wilaya ya Magu ambapo kwa sasa waumini wa kanisa hilo wanaruhusiwa kuhiji kwenye kituo hicho.
Mgogoro huo uliodumu kwa miaka mitano ulikuwa ukihusisha zuio la kuhiji katika kituo hicho ambalo liliwekwa na Halmashauri ya Magu baada ya kukitangaza kituo cha Kageye kuwa Makumbusho ya Taifa.
Juni 13, 2023 Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Renatus Nkwande alimuomba Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa mkoni Mwanza kuhudhiria ufunguzi wa tamasha la Bulabo kutatua mgogoro huo ambao umekwamisha baadhi ya shughuli za kanisa hilo ikiwemo ibada.
“Serikali ilitangaza kituo cha Kageye kuwa makumbusho lakini haitunyimi sisi wamiliki kukitumia kwa shughuli zetu za kidini. Tunagombana na kwa kitu ambacho kiko wazi, Kanisa Katoliki tulikijenga ili watu wakifika pale wafanye ibada zao,” alisema Askofu Nkwande.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Renatus Nkwande.PichalMwananchi
Kufuatia ombi hilo Amos Makalla, aliahidi kulifuatilia suala hilo na hii leo Julai 12 amewatangazia waumini wa kanisa hilo kuwa sasa wanaweza kuendelea na ibada zao kituoni hapo wakati taratibu za umiliki zikiendelea kufuatiliwa.
“Nimetumwa na Rais kuja hapa na kabla ya hapo nimewasiliana na Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na yule wa Ardhi…kwa sasa nimeruhusu eneo hilo lianze kutumika kwa ajili ya ibada, masuala mengine ya umilikishwaji yatashughulikiwa na wizara husika,” amesema Makalla wilayani Magu.
Mkuu huyo wa Mkoa amewaomba waumini wa kanisa hilo kongwe duniani kutoa ushirikiano kwa wizara husika ili kukamilisha taratibu zilizosalia kwa wakati.
Paroko anena
Father John Makungu ambaye ni Paroko wa Parokia ya Kayenze amesema kwao ni faraja kubwa kuona serikali imewarejeshea eneo hilo ambalo kwao ni la kihistoria.
Makungu ameongeza kuwa nia ya kituo hicho ni kuviunganisha na kuviendeleza vituo vya hijja vya Malya, Kageye na Bukumbi ambavyo ni muhimu katika kutunza na kuenzi historia ya ukristo katika maeneo hayo.
“Tutaendelea kuenzi eneo hili kwakuwa kwetu ni eneo takatifu ni mahali ambapo ndugu zetu wamishonari walimwaga damu wakazikwa mahali hapa, kama moja ya mbegu ilizikwa na kuchipua hivyo sisi tutaendelea kuenzi,” amebainisha Father Makungu
Kituo hicho ni moja ya vituo vitatu vya hija vikiwamo Bukumbi na Malya ambavyo ni sehemu ya historia ya kanisa katoliki Kanda ya Ziwa na vinatumika kwa shughuli za hijja kwa waumini wa kanisa hilo.
Latest