Serikali yazindua kampeni ya ‘sitapeliki’ kukabiliana na utapeli, wizi mtandaoni
- Yazindua jumbe sita zitakazosaidia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu utapeli mtandaoni.
- Ushirikiano na mashirika yasiyo ya serikali, taasisi kuongeza nguvu ya kukabiliana na utapeli.
Arusha. Serikali ya Tanzania imezindua kampeni mpya iliyopewa jina la ‘sitapeliki’ kukabiliana na vitendo vya utapeli na ulaghai mtandaoni vinavyoendelea kushika kasi nchini.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika jijini Arusha leo Februari 20, 2025 amesema kuwa kampeni hiyo imelenga kupunguza wimbi la utapeli kwa kuongeza uelewa kwa wananchi.
“Kampeni hii inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mbinu zinazotumiwa na matapeli wa mtandaoni na kuwapa maarifa sahihi ya jinsi ya kujikinga dhidi ya majaribio mbalimbali ya ulaghai,” amesema Silaa.
Uzinduzi wa kampeni hiyo ni muendelezo wa jitihada za kukabiliana na utapeli mtandaoni wakati huu ambapo Tanzania inaendelea kupiga hatua katika maendeleo ya Teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).
Jitihada hizo ziliwezesha kupungua kwa utapeli kwa njia ya mtanda kwa asilimia 19 kutoka matukio 16,069 yaliyoripotiwa katika robo ya mwaka inayoishia Septemba hadi matukio 12,896 kwa mujibu wa ripoti za mawasiliano zinazotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Silaa amewaambia wahudhuriaji wa uzinduzi huo kuwa watumia njia mbalimbali kufikisha elimu hiyo ya kujilinda dhidi ya utapeli kwa wananchi kwa kutumia ujumbe wa simu (sms) utakaosambazwa na watoa huduma, matangazo ya televisheni, redio na njia nyingine za mawasiliano.
Miongoni mwa jumbe zitakazotumika kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu utapeli ni pamoja na ‘linda tarifa zako kwa kutunia nywila thabiti na tofauti kwa kila akaunti yenye mchanganyiko wa maneno, namba, alama, herufi kubwa, na ndogo.
“Jumbe nyigine, nasema usifuate maelekezo na kutoa nywila yani neno la siri au namba yako ya utibitisho kwa kifupi ‘OTP’ kwa mtu yoyote. Usifuate maelekezo na kutoa nywila yani neno la siri au namba yako ya uthibitisho kwa kifupi ‘OTP’ kwa mtu yoyote,” amesema Silaa.
Aidha, Silaa amesema kuwa kampeni hiyo itafanikiwa endapo wizara yake itashirikiana na sekta mbalimbali mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya habari, na jamii kwa ujumla.
Pamoja na hayo amewataka wananchi kutokutoa ushirikiano kwa watoa huduma wasio rasmi wasiotumia namba 100 ambayo ndiyo iliyosajiliwa kwa ajili ya kuwasiliana na wanchi pamoja na kutokujibu jumbe wasizozielewa au kuwa na viashria vya kitapeli.
“Hatuna mtu yoyote aliyedukuliwa kwenye mtandao bila kutoa ushirikiano…Lazima watanzania wafahumu watoa huduma wote mawasiliano yao wao yanafanyika kwa kutumia namba 100 pekee ukipata simu yoyote ambayo haitokani na namba 100 hiyo ni namba ya ulaghai,” amesema Silaa.
Latest



