Majaliwa: Serikali haitawafumbia macho watumishi wa ‘hovyo’
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mwabakima wilayani Igunga akiwa katika ziara ya siku moja wilayani humo ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa zao la pamba, Julai 15, 2019. Kushoto ni Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Amewataka kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wala kupokea rushwa.
- Amesisitiza kuwa vita dhidi ya rushwa ni endelevu.
- Ripoti mpya ya Shirika la Kimataifa la Transparency International yakiri kiwango cha rushwa Tanzania kimeshuka.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watumishi wote wa umma kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi bila ubaguzi na Serikali haitomvumilia mtumishi atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Kauli ya Majaliwa inakuja siku chache tangu ripoti mpya ya Shirika la Kimataifa la Transparency International kubainisha kuwa kiwango cha rushwa Tanzania kimeshuka kutoka asilimia 25 mwaka 2015 hadi asilimia 18 mwaka 2019.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa takriban robo tatu ama asilimia 72 ya waliohojiwa katika utafiti huo nchini walieleza kuwa kiwango cha rushwa kimeshuka huku asilimia 13 au mmoja kati ya watu 10 akieleza kuwa kimeongezeka ndani ya kipindi cha miezi 12 iliyopita.
Majaliwa aliyekuwa akizungumza mwishoni mwa wiki katika mkutano na viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma, amesisitiza kuwa vita dhidi ya rushwa ni endelevu.
“Watumishi wa umma wanatakiwa kutambua kwamba jukumu lao kubwa ni kuwatumikia wananchi kwa kuzingatia maadili na kanuni za utumishi wa umma zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni na si vinginevyo.
“Serikali hii kamwe haitowaonea haya au kuwafumbia macho watumishi wa hovyo,” amesema Majaliwa.
Soma zaidi: Rushwa yapungua Tanzania-Transparency International
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali imejipanga vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa, hivyo amewataka wananchi wasisite wakati wote kutoa taarifa kwa vyombo husika pale watakapobaini uwepo wa watumishi wanaojihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.
Amesema kuwa suala la kuwaondoa kazini watumishi wazembe, wasiotimiza wajibu wao ipasavyo pamoja na wale wasiozingatia maadili ya utumishi wa umma ni endelevu kwa sababu Serikali inahitaji watumishi wa umma wenye heshima na nidhamu ya kazi.
“Suala la kuwapokea, kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma kwa wananchi zikiwemo ofisi za Serikali kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo watumishi wa umma wanapaswa kuzingatia jambo hilo,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Ripoti hiyo mpya iliyotolewa Julai 11, 2019 inaonyesha kuwa kwa sasa Tanzania inaongoza katika nchi 35 za Afrika baada ya kupungua kwa vitendo vya rushwa katika sekta mbalimbali, rushwa katika ofisi ya Rais, Waziri Mkuu, viongozi wa dini, wabunge na viongozi wa kimila ikipomoroka kwa kasi.