Majaliwa atoa tena maagizo mazito matumizi ya vyoo bora, utunzaji wa mazingira.

November 23, 2018 8:55 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Awaagiza watendaji Serikalini kuhakikisha lengo la kila kaya nchini kupata choo bora kabla ya Desemba 31, 2018 linafikiwa. 
  • Wananchi wapewe elimu ya matumizi ya vyoo bora pamoja na umuhimu wa usafi wa mazingira ili kuwaepusha na maradhi.
  • Huduma za vyoo bora na sehemu za kunawa mikono zifike katika taasisi zote za umma na binafsi zikiwemo shule, vituo vya afya na nyumba za ibada.
  • Ameonya jamii dhidi ya tabia ya kuchimba dawa wakati wa safari kuwa atakayekamatwa atachukuliwa hatua za kisheria.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi na Ajira kufanya ukaguzi wa vyoo na mifumo ya kutiririsha maji katika viwanda vyote nchini na vitakavyobainika na makosa hatua kali zichukuliwe.

 Pia amewaagiza maafisa afya na mazingira katika mikoa yote nchini badala ya kuzingatia maeneo ya hoteli, mabucha na migahawa waende kwa wananchi kutoa elimu ya matumizi ya vyoo bora pamoja na umuhimu wa usafi wa mazingira ili kuwaepusha na maradhi.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hay leo (Novemba 23, 2018) katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya usafi wa mazingira kitaifa na mkutano wa Maafisa afya wa mikoa, halmashauri na wadau wa afya na mazingira Tanzania, uliofanyika Jijini Dodoma.

Amesema viwanda vina jukumu la kuhakikisha vinatunza afya za wafanyakazi wake kwa kufuata taratibu na sheria za afya kazini. 

“Ni jukumu la kila kiwanda kuhakikisha kwamba kinadhibiti uchafuzi wa hewa ili tuweze kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Majaliwa.

Amesema kwamba hivi sasa, madhara ya mabadiliko ya tabianchi yameanza kushuhudiwa  nchini na endapo jitihada za makusudi zisipochukuliwa ipo hatari ya kufifisha matarajio ya vizazi vijavyo. 

Kufuatia hatua hiyo, Majaliwa amewaelekeza wakuu wote wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na maafisa watendaji wa kata, mitaa na vijiji nchini wasimamie vizuri na kwa ukaribu kampeni ya usafi wa mazingira na matumizi ya vyoo bora.

“Hakikisheni kuwa lengo la kila kaya nchini kupata choo bora kabla ya tarehe 31 Desemba, 2018 linafikiwa. Waziri mwenye dhamana, tambua kwamba baada ya tarehe husika kupita nitahitaji kupata taarifa kuhusu utekelezaji wa agizo hilo kutoka kwa kila mkoa na halmashauri nchini,” amesema Majaliwa.


Zinazohusiana: 


Amebainisha kuwa ameelezwa kuwa hadi kufikia Septemba 30, 2018 kaya zenye vyoo bora zimefikia asilimia 51.4 kutoka asilimia 46.6 Julai, 2017 na katika kipindi hicho kaya zisizokuwa na vyoo kabisa imepungua kutoa asilimia 5.4 hadi asilimia 3.8. 

Iwapo watendaji Serikalini watazidisha kasi katika utoaji wa elimu, usimamizi wa sheria na kuongeza ufuatiliaji, kaya zote zitakuwa na vyoo bora ndani ya muda mfupi ujao. 

“Nimedokezwa hapa kwamba, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika hilo. Sasa nitashangaa sana kwa nini wengine mshindwe?,” amehoji Majaliwa na kuongeza kuwa,

“Ninaagiza shule zote, vituo vyote vya tiba, vituo vya abiria, masoko na nyumba zote za ibada ziwe na miundombinu bora ya vyoo na sehemu za kunawa mikono.” 

Wakurugenzi wa halmashauri nao waagizwa kuhakikisha maeneo yote hayo yanakuwa na huduma hizo muhimu kabla ya Aprili 30, 2019 itasaidia kuondokana na aibu ya kukosa miundombinu ya usafi katika taasisi zao. Usafi wa mazingira ni sehemu muhimu ya kuhifadhi mazingira. Picha| wisemantanzania

Katika hatua nyingine, Majaliwa ameonya jamii dhidi ya tabia ya ya kuchimba dawa wakati wa safari, “tabia hii imeota mizizi, imekuwa kama ni desturi ya baadhi ya watu licha ya Serikali pamoja na sekta binafsi imeweza kuweka huduma za vyoo kwenye stendi za mabasi, vituo vya kuuzia mafuta, pamoja na hoteli zinazotumiwa na wasafiri.” 

Amesema haiingii akilini kuona basi la abiria linasimama porini ili watu wajisaidie wakati muda mfupi uliopita basi hilo lilisimama kwenye kituo kikubwa cha abiria au sehemu zinazotoa huduma ya chakula.

Maagizo hayo pia yanawahusu watendaji Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia kikosi cha usalama barabarani, SUMATRA na kuandaa mikakati ya kuondokana kabisa na tabia hii hatarishi kiafya. “

Waziri Mkuu amewaagiza maafisa afya na mazingira kote nchini watekeleze wajibu wao kwa kuwachukulia hatua za kisheria madereva na makondakta wote watakaobainika kusimamisha magari porini kwa lengo la kuchimba dawa.

Katika mkutano huo halmashauri ya wilaya ya Njombe imeibuka kidedea kwenye kundi la utekelezaji wa kampeni ya Taifa ya usafi wa mazingira, ambapo imepewa zawadi ya gari aina ya Ford Ranger lenye thamani ya Dola za Marekani 35,700.

Mbali na halmashauri hiyo kuibuka mshindi na kupata zawadi ya gari jipya pamoja na tuzo, ndiyo Halmashauri pekee nchini ambayo kaya zake zote zina vyoo bora na kwamba hakuna kabisa tabia ya kujisaidia vichakani. 

“Ni dhahiri kuwa endapo halmashauri zote zitafikia hadhi ya Njombe tutaokoa fedha nyingi ambazo zinatumika kugharamia matibabu ya wagonjwa pamoja na kuokoa muda mwingi unaohitajika kwenye shughuli za uzalishaji ambao unapotea kila siku kwa kuuguza watu wanaopata magonjwa yanayoenezwa kwa njia ya uchafu,” amesema Majaliwa.

Enable Notifications OK No thanks