Majaliwa ashikilia hatma ya DED Lindi

August 23, 2019 12:06 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga ametakiwa kuwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Waryoba Gunza.
  • Hatua hiyo imekuja baada ya  kushindwa kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi wa maji kata ya Rutamba.
  • Waziri Mkuu, Majaliwa amesema hawatamvumilia mtumishi yeyote asiyetekeleza majukumu yake ipasavyo.  

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga ampelekee taarifa ya utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Waryoba Gunza baada ya kushindwa kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi wa maji kata ya Rutamba.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo (Agosti 23, 2019) wakati akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Rutamba akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo na huduma za jamii mkoani Lindi.

Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu inaeleza kuwa Majaliwa ametoa agizo hilo baada ya kumtaka Mkurugenzi huyo atoe maelezo ya namna gani walivyojipanga katika kutekeleza mradi wa maji kwenye kata hiyo ambayo wakazi wake wanakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji na kushindwa kutoa maelezo.

 Mradi wa maji wa kata hiyo unakabiliwa na tatizo la uchakavu wa miundombinu na ukarabati wake unahitaji bajeti ya Sh75 milioni ambazo zimeombwa kutoka Wizara ya Maji.

Waziri Mkuu amesema miradi yote ambayo gharama zake ziko chini ya Sh100 milioni  inatakiwa itekelezwe kwa kutumia fedha za ndani ya halmashauri husika. 

 “Miundombinu hiyo ilitakiwa iwe imebadilishwa. Mradi wa Sh75 milioni  unaomba fedha wizarani ni uvivu,” amesema Majaliwa.


Soma zaidi: 


Waziri Mkuu amesema suala la huduma ya maji limewekewa msisitizo na Rais John Magufuli kwa kuanzisha kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani, inayolenga kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama karibu na makazi yao.

Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi hao kwamba licha ya kuagiza mradi huo wa ukarabati wa miundombinu ya kusambazia maji ufanyike kwa haraka, pia Serikali inatekeleza mradi mwingine wa maji wa Milola ambao ukikamilika maji yatafikishwa hadi Rutamba.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwahutibia wananchi wa Kata ya Rutamba, kwenye mkutano wa hadhara, akiwa mkoani Lindi katika ziara ya kikazi ya siku mbili, Agosti 23.2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Wilaya nchini wahakikishe wanawasimia vizuri watumishi wa umma na kuwachukulia hatua wote watakaobainika kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Watumishi fanyeni kazi kwa bidii na msitarajie kuundiwa tume pale mnapofanya vibaya, ukiharibu kazi tunakushughulikia hapo hapo na huu ndiyo msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk  John Magufuli,”  amesisitiza Majaliwa.

Awali, akizungumza kwa niaba ya wabunge wa mkoa wa Lindi, Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Lulida amesema wakazi wa kata ya Rutamba wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji licha ya kuwepo kwa vyanzo, hivyo aliiomba Serikali iwasaidie.

Hata hivyo alilalamikia kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira katika maeneo hayo ikiwemo uvamizi katika vyanzo vya maji pamoja na ukataji hovyo wa misitu unaohatarisha kuibuka kwa jangwa, ambapo Waziri Mkuu ameagiza viongozi wa wilaya hiyo kuzishughulikia suala hilo.

Enable Notifications OK No thanks