Majaliwa aondoa sintofahamu ya bei ya pamba, sasa kuuzwa Sh1,200 kwa kilo
- Amesema baada ya kupitisha bei hiyo pamba ianze kuuzwa mara moja katika maeneo yote.
- Amesema jukumu la kutoa leseni za ununuzi wa zao hilo ni la Bodi ya Pamba na siyo Wakurugenzi wa Halmashauri.
- Atoa maagizo mazito kwa wakulima, vyama vya ushirika na wakala wa vipimo.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameondoa sintofahamu ya bei ya pamba, baada ya kutangaza bei elekezi ya Sh1,200 kwa kilo itakayotumika katika msimu wa manunuzi katika mikoa yote inayozalisha zao hilo Tanzania.
Sintofahamu ya bei ya zao hilo imedumu kwa takriban wiki nne tangu bei elekezi ilipotangazwa Aprili 30, 2019 mkoani Shinyanga ambapo ilitarajiwa kuanza kutumika Mei 2, 2019.
Waziri Mkuu amefikia uamuzi huo wakati akizungumza na wadau wa sekta ndogo ya pamba kwenye kikao kilichofanyika leo (Mei 29, 2019) kwenye ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu leo, baada ya muafaka huo, ununuzi wa zao la pamba utaanza mara moja kwa bei ya Sh1,200 kwa kilo moja katika mikoa yote inayozalisha zao hilo.
Amesema kwa sasa Bodi ya Pamba (TCB) iachiwe jukumu la kutoa leseni za ununuzi wa zao hilo na kwamba Wakurugenzi wa Halmashauri waliokuwa wakifanya kazi hiyo waache mara moja.
“Kuna baadhi ya Wakurugenzi wanatoa leseni za ununuzi, lakini wenye Mamlaka ni Bodi ya Pamba. Mnunuzi nenda Bodi ukapate leseni yako,” amesema Waziri Mkuu na kubainisha kuwa,
“Wakurugenzi baadhi yenu mnazuia wanunuzi wapya, mnamtaka fulani tu. Kwa kufanya hivyo, unapunguza kiwango cha kilo ambacho wakulima wako wangeuza.”
Soma zaidi: Wakulima kuuza pamba kwa bei wanayoitaka
Maagizo kwa wakulima, vyama vya ushirika na wakala wa vipimo
Kuhusu ubora wa pamba, Waziri Mkuu ameagiza wananchi waelimishwe ili waache kuweka maji au mchanga kwenye pamba kwa minajili ya kuongeza uzito kwani kwa kufanya hivyo wanachafua jina la Tanzania pindi inapopelekwa kuuzwa nje ya nchi.
Pia amevitaka vyama vikuu vya ushirika vijiridhishe kuhusu ubora wa maghala ya kuhifadhia pamba kwenye vyama vya msingi (AMCOS) ili kuwasaidia wakulima wauze mapema pamba yao mara baada ya kuivuna.
Wakala wa vipimo nchini (WMA) wameagizwa waende wakakague mizani zilizopo AMCOS na vinu vya kuchambulia pamba (ginneries) kwa sbabu ya kuwepo kwa tofauti kubwa ya uzito inayojitokeza na kuwalazimisha wakulima kulipia upotevu wa kilo hizo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe atume wakaguzi kwenye Bodi ya Pamba ili wabainishe matumizi ya Sh100 kwa kila kilo ambazo zimekuwa zikilipwa kwenye bodi hiyo.
“Katibu Mkuu Kilimo lete wakaguzi ndani ya bodi ya pamba, waangalie kwa kipindi cha miaka mitatu toka tulipoanza kukusanya Sh100 kwa kilo, zimekusanywa shilingi ngapi, na zimetumika kulipia nini.
“Na Mrajisi wa Ushirika nchini ufanye ukaguzi kwenye vyama vikuu vya Ushirika na AMCOS. Uangalie ziko ngapi na zinafanya nini. Kuna AMCOS zina hela, je fedha hiyo imetumika kufanya nini ili kuendeleza zao la pamba. Je zimenunua matrekta au zimelipia posho za vikao,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya zinazolima zao la pamba katika mkutano wa dharura wa baadhi ya wadau wa zao la pamba kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza, Mei 29, 2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi Binafsi wa Pamba (TCA), Christopher Gachuma amemshukuru Waziri Mkuu kwa maelekezo aliyoyatoa kuhusu utoaji wa leseni kwani yalikuwa ni kikwazo kikubwa kwa baadhi ya wanunuzi wa zao hilo.
“Suala la utoaji leseni linapaswa lianze mapema lakini kuna wengine hadi sasa bado hawajapata leseni zao,” Amesema Gachuma
Kikao hicho kilichoitishwa na Majaliwa kilihudhuriwa na Manaibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa wizara za Kilimo na Viwanda, Ofisi ya Rais-Tamisemi na Wakuu wa Mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu na Geita ambayo inalima zao hilo.
Pia kilihudhuriwa na wanunuzi wa pamba, wakulima na maafisa wa benki kadhaa.