Majaliwa akerwa uchakavu vyoo vya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Tanzania
- Aagiza vyoo hivyo vinavyotumiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Terninal 2 jijini Dar es Salaam vibadilishwe haraka.
- Amesema vyoo hivyo vimechoka.
- Aridhishwa na maandalizi ya mapokezi ya wajumbe wa mkutano SADC uwanjani hapo.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza vyoo vya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Terninal 2 jijini Dar es Salaam vibadilishwe haraka kutokana na uchakavu ili kulinda afya za wasafiri wanaotumia uwanja huo.
Majaliwa aliyekuwa akizungumza leo (Julai 31, 2019) wakati alipotembelea uwanja huo ili kukagua maandalizi ya mapokezi ya wajumbe wa mkutano wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), amesema vyoo hivyo vimechoka na vinatakiwa vibadilishwe haraka sana.
“Nimepita VIP hakuna shida. Pale terminal 2, sehemu ya Uhamiaji iko vizuri, uchunguzi wa afya nayo iko vizuri, lakini vyoo inabidi vibadilishwe haraka sana. Vile vyoo pale nje vimechoka, vibadilishwe mara moja, siyo tu kwa ajili ya ugeni, bali ni kwa faida yetu pia,” amesema Majaliwa wakati akitoa maagizo hayo kwa Meneja wa uwanja huo, Paul Lugasha.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa ameridhishwa na maandalizi ya mapokezi katika uwanja huo isipokuwa baadhi ya kasoro ambazo zinatakiwa zirekebishwe.
Soma zaidi:
- Waziri azungumzia ndege za ATCL kuchelewa, kuahirisha safari
- Shirika la ndege la Ethiopia limesitisha safari zote za ndege aina ya Boeing 737
- ATCL inavyojitanua kimataifa
Pia alipata fursa ya kutembelea jengo jipya la Terminal 3 kwenye uwanja huo, ambalo viongozi wakuu wa nchi za SADC watashukia, watakagua gwaride la heshima na kuangalia vikundi vya ngoma.
Pia amekagua vyumba ambavyo watapumzikia kabla ya kuelekea mjini huku akiwataka wahusika waweke matangazo (banners) za kutosha za aina mbalimbali na picha za wanyama katika kuta za uwanja huo ili kuonyesha kwamba kuna mkutano mkubwa unafanyika hapa nchini.
Amebainisha kuwa usafi wa barabarani katika jiji la Dar es Salaam bado hauridhishi kwa sababu kuna mawe, udongo na michanga kwenye barabara kuu ya kutoka uwanja wa ndege hadi mjini.
“Tulikubaliana kuwa zile bustani ziboreshwe, vyuma vya barabarani vitengenezwe lakini hata leo nimepita kwenye fly-over, bado kuna mawe na michanga, hata sijui vinatokea wapi,” amesema.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kizungumza na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wilson Kantambula (kulia) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Damas Ndumbaro (kushoto) wakati alipokagua maadalizi ya mapokezi ya wajumbe wa mkutano wa SADC kwenye jengo la pili na la tatu katika kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Julai 31, 2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewataka Watanzania watumie fursa ya uwepo wa mkutano huo mkubwa kuendesha biashara zao na ujasiriamali.
“Ziko fursa nyingi za uwepo wa mkutano huu. Kila mmoja atumie nafasi hii kuweza kuongeza na kuboresha kazi yake inayomletea uchumi,” amesema.
Latest