Wananchi zaidi ya 2,000 kupisha upanuzi wa kiwanja cha ndege Mwanza

September 14, 2023 7:33 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Wananchi hao ni wakazi wa mitaa ya Mhonze, Kihili na Bulyanhulu wilayani Ilemela.
  • Hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha ulinzi na usalama katika kiwanja hicho.

Mwanza.Wananchi zaidi ya 2,000 wanaodaiwa kuvamia kwenye eneo la kiwanja cha ndege kilichopo wilayani Ilemela mkoani Mwanza wanatarajia kuhamishwa kupisha upanuzi wa kiwanja hicho ifikapo Disemba mwaka huu.

Wananchi hao wanaotarajia kuhamishwa ni kutoka nyumba 800 zilizojengwa katika mitaa ya Mhonze, Kihili na Bulyanhulu iliyopo wilaya ya Ilemela jijini humo.

Akizungumzia suala hilo leo Septemba 13, 2023 jijini Mwanza, mkuu wa mkoa huo Amos Makalla amesema Serikali inaandaa utaratibu wa kuwaondoa wananchi waliovamia eneo la kiwanja hicho.

Hatua hiyo inaelezwa kutoa fursa kwa shughuli za kiwanja hicho kinachoshika nafasi ya tatu kwa ukubwa Tanzania kufanyika kwa usalama.

“Kwa kuwa Mwanza tunaanza Safari ya kuubadilisha uwanja wa ndege kuwa wa kimataifa… jeshi la anga wanalihitaji eneo hilo pia kwa usalama wa ndege zao za abiria na kwa wananchi wetu pia,” amesema Makalla

Aidha, Makalla ameagiza Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TAA) kuandaa michoro ya jengo la abiria, upanuzi wa hoteli na ‘shopping mall’ ili kuleta unadhifu kwenye huduma.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Amos Makalla akizungumza na wafanyakazi wa uwanja wa Ndege mkoani Mwanza.Picha|Mariam John.

Kazi hiyo imetakiwa kufanyika kwa haraka ili kuwezesha utolewaji wa huduma bora zitakazotokana na miundombinu ya kimataifa na kisasa itakayojengwa katika uwanja huo. 

“Nilikuja hapa nikiwa na siku tatu tu Mwanza na nlielekeza muanze ujenzi mara moja tena kwa bahati mna fedha za kuanzia tena ni Sh11 Bilioni na kazi ya kwanza mliyotakiwa kuanza nayo ni kusanifu namna bora ya ujenzi wa Jengo ambalo litakua la kimataifa kwa ajili ya kuubadilisha uwanja wetu kuwa wa kimataifa,” amesema Makalla.


Soma zaidi


Serikali yafanya maboresho uwanja wa ndege Mwanza

Wakati TAA ikihamasisha kuongeza kasi ya uchoraji ramani meneja wa uwanja huo Mussa Mchola amesema tayari Serikali imefanya maboresho mbalimbali katika uwanja huo hatua itakayowezesha mazingira bora kwa usafiri wa anga nchini.

“Serikali imefanya maboresho ya kimkakati kama urefushaji wa wa barabara ya kutua na kupaa, upanuzi na ujenzi wa tabaka la mwisho la lami pamoja na ujenzi wa jengo jipya la mizigo na barabara za maungio ya ndani kwa ajili ya magari na mfumo wa maji taka,” ameongeza Mchola.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW