Majaliwa afunga soko, amsimamisha kazi Mweka Hazina Kigoma
- Soko hilo ni lile lililoanzishwa nje ya kambi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo mkoa wa Kigoma ambapo linatajwa kuchochea uharifu.
- Mweka hazina huyo ni Thomas Chogolo anatuhumiwa kwa ubadhilifu wa makusanyo ya mapato ya halmashauri hiyo.
- Amewataka watendaji wa halmashauri huyo kumaliza haraka migogoro yao ya kiutendaji kabla ya Serikali haijawachukulia hatua kwani ni kinyume na maadili ya kazi.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefunga soko la wakimbizi na wananchi lililoanzishwa nje ya kambi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo mkoa wa Kigoma na kumshimamisha kazi Mweka Hazina wa halmashauri hiyo kwa tuhuma za ubadhilifu wa makusanyo ya mapato.
Hatua hiyo imekuja baada ya soko hilo kubainika kuwa chanzo cha wakimbizi kutoka nje ya kambi kiholela na kushiriki katika matukio ya kiharifu.
Majaliwa ametangaza uamuzi huo leo (Februari 19, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma ambapo amesema ni vema halmashauri hiyo ikaandaa utaratibu wa kutoa vibali vitakavyowaruhusu Watanzania kupeleka bidhaa ndani ya kambi hiyo.
“Vitendo vya uhalifu wilayani Kibondo vikiwemo vya utekaji wa watoto vimeongezeka na kusababisha hofu na taharuki miongoni mwa wananchi.
“Nafahamu tunao watendaji wetu ambao wapo kambini kusimamia shughuli mbalimbali za wakimbizi, tekelezeni wajibu wenu ipasavyo na si vinginevyo,” amesema Majaliwa.
Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibondo wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibondo leo (Februari 19, 2019). Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
Katika hatua nyingine, Majaliwa amemsimamisha kazi Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo, Thomas Chogolo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili za ubadhilifu wa makusanyo ya mapato ya halmashauri hiyo.
“Katika Serikali hii suala la ukusanyaji wa mapato ni jambo nyeti na limepewa kipaumbele, hivyo ni lazima fedha inayokusanywa itumike kama ilivyokusudiwa ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.”
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu leo inaeleza kuwa wananchi wa halmashauri hiyo wanalipa kodi kupitia kwa watendaji wa kata katika maeneo yao lakini Mweka Hazina huyo amekuwa siyo mwaminifu katika mapato.
Imebainika kuwa mbali na fedha za makusanyo ya kodi pia matumizi ya fedha mbalimbali zinazopelekwa na Serikali katika halmashauri hiyo nayo hayaridhizishi.
Akitolea mfano wa fedha za sekta ya Afya, amesema zaidi ya bilioni mbili zimepelekwa na lakini dawa hazipatikani katika vituo vya afya.
Soma zaidi:
- Majaliwa: Nawaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii waache
- Majaliwa aagiza elimu itolewe upangaji madaraja ya korosho.
Amesisitiza kuwa uaminifu na uadilifu ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele na watumishi wa umma, hivyo amewataka watumishi hao wasijiingize kwenye mambo ambayo hayana tija katika utumishi wao.
“Serikali haitawapa nafasi ya kuendeleza migogoro yenu kila mmoja lazima atambue majukumu yake na kuyatekeleza. Serikali haiitaji mtumishi mvivu, asiyekua muadilifu na wala anayejihusisha na vitendo vya rushwa,” amesema Majaliwa.
Akihitimisha maagizo yake, amewataka watendaji wa halmashauri huyo kumaliza haraka migogoro yao ya kiutendaji kabla ya Serikali haijawachukulia hatua kwani wanachokifanya ni kinyume na maelekezo yake.