Maisha ni siasa: Nani mwingine anasema haimhusu?
- Uwe ni mtoto mchanga, kijana au kikongwe wa miaka 100, siasa itakugusa tu.
- Miaka ya nyuma nilidhani siasa hainihusu, wapi? Nilikuwa najidanganya.
Siasa, vyovyote vile unavyoijua au unavyoichukulia ina athari chanya na hasi katika maisha yetu ya kila siku.
Iwe kiumbe kilichopo ndani ya mama yake, mtoto mchanga wa miezi miwili, kijana wa miaka 20 au mzee wa miaka 100. Huwezi kukwepa mkono wa siasa katika maisha yako. Lazima utaguswa tu.
Miaka mingi iliyopita niliwahi kuongea kwa kejeli kuwa sifuatilii siasa na kuwa ilikuwa hainihusu. Nilidhani kufuatilia wanasiasa wanasema nini na wanafanya nini ni kupoteza muda tu.
Sababu kubwa iliyonifanya nifikie uamuzi huo ni mawazo kwamba “wanasiasa hawa hawanisaidii chochote hivyo sina haja ya kufuatilia wanachokifanya”. Natamani hii ndio ingekuwa hali halisi. Haikuwa.
Taa za kejeli zangu zilianza kufifia kwa mara ya kwanza wakati Kanuni za maudhui ya mtandaoni chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta zilipoanzishwa mwaka 2018.
Kipindi hicho nilikuwa na blogu na chaneli ya YouTube nilizokuwa nazitumia kuwashirikisha watu mambo mbalimbali kuhusu vitabu ninavyovisoma nilivyokuwa najifunza mahali nilipotembelea au watu niliokutana nao katika kazi zangu.
Kanuni hizi za maudhui mtandaoni zilikuja na utaratibu wa namna ambavyo wazalishaji maudhui mitandaoni kama blogu, YouTube na mitandao mengine walitakiwa kujisajili ili kupata leseni ya kuendelea kutoa huduma hizo za kimaudhui.
Kubwa kwangu ilikuwa ni sharti la kulipa Sh1.1 milioni ili kuweza kupata leseni hii ikijumuisha Sh100,000 ya maombi ya leseni. Inakuwaje kijana ambaye nimeamua kushirikisha watu uzoefu wangu kwenye mitandao nilipe pesa kufanya hivyo wakati hakuna kipato ninachoiingiza kutokana na maudhui hayo? Kwa faida gani?
Kutokana na mkanganyiko uliokuwepo wa nani anatakiwa kulipa na nani hatakiwi kulipa, pamoja na mazingira ya kisiasa ya wakati huo, nililazimika kusitisha kwa uchungu mkubwa ushirikishaji wa maudhui mtandaoni.
Taa hii ilipoteza mwangaza kabisa pale ambapo Sheria ya Bodi ya Mikopo ya mwaka 2016 ilipowataka wanufaika kurejesha mkopo kutoka asilimia 8 mpaka asilimia 15 ikiwa ni ongezeko la takriban mara mbili. Ongezeko hilo, lilioanza kutekelezwa Februari 2017, ni kubwa hasa kwa mfanyakazi ambaye kipato chake cha kukidhi maisha ni mshahara pekee yake. Hili wanasiasa hawakuliona wanavyopitisha sheria hiyo ambayo imeendelea kuwa mwiba kwa watu wengi wenye mishahara midogo
Sheria hii na nyingine nyingi ambazo zinagusa maisha ya wananchi ya kila siku zinapitishwa na Bunge na wabunge ambao ni wawakilishi wetu. Kwa akili ya kawaida hawa walitakiwa kuwa mstari wa mbele kutupigania na kutupunguzia maumivu.
Lakini si wote wanaona wanawajibu wa kutupigania si mijini wala vijijini. Kutokana na kazi ninayoifanya, huwa napata bahati ya kutembelea maeneo mengi, hasa ya vijijini. Ukiwa huko, unaona namna siasa inavyogusa maisha ya kila siku ya wananchi.
Zinazohusiana:
- Makosa dhidi ya binadamu yaongezeka kwa asilimia 26 Tanzania
- Rais Samia asisitiza siasa za maridhiano kongamano la Bawacha
Baadhi ya masuala ambayo ni matokeo ya kisiasa ni kama pale wanawake wajawazito wanapokosa huduma bora za afya na ubovu wa barabara za kuwafikisha zahanati zilizo mbali na maeneo wanayoishi. Hii haihatarishi afya ya mama peke yake bali hadi maisha ya kiumbe ambacho hakijazaliwa bado.
Kunapokosekana shule katika maeneo mbalimbali, hakunyimi tu haki ya watoto kupata elimu lakini pia kuna nyima haki hii kwa vizazi vijavyo pia.
Kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa Uwezo (2019), mama anapokuwa na elimu ya sekondari au zaidi ana uwezekano mkubwa wa kuwalea watoto vizuri lakini pia kuweza kuhakikisha wanapatiwa elimu.
Kwa wastani, watoto 7 kati ya 10 (72%) wanaosoma madarasa ya 3 hadi 7 ambao mama zao wana elimu ya sekondari au zaidi walipita vipimo vya ustadi wa kusoma na kuhesabu vya Uwezo ikilinganishwa na 54% ya wenzao ambao mama zao hawakuwa na elimu rasmi.
Kukosekana kwa vyote hivi kunatokana na kutokuwa na sera nzuri ambazo zinamuweka mwanachi mbele katika kuleta maendeleo. Hii inasababishwa na wanasiasa na siasa ambazo zipo kunufaisha wachache.
Wiki chache zilizopita kulikuwa na mjadala wa kina ulioandaliwa na Jamii Forums kupitia X (zamani Twitter) juu ya athari za mgao wa umeme.
Mwanaharakati maarufu nchini Tanzania, Ananilea Nkya akihojiwa na wanahabari wakati wa maandamano yaliyoandaliwa na chama cha Chadema Januari 24, 2024 ambapo miongoni mambo mengine yalikuwa yakihimiza Serikali kutatua kupanda kwa gharama za maisha. Picha|Nuzulack Dausen/Nukta.
Mmoja wa wazungumzaji, Martin Mbwana ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo aliiomba Serikali kutoa taarifa juu ukataji wa umeme ili waweze kujiandaa kutafuta njia nyingine za kupata umeme.
“Kama tatizo ni umeme tuambiwe mapema. Tutaarifiwe litakuwa kwa muda wa miezi miwili au mitatu tujipange. Hiyo kuwasha na kuzima tunaomba hayo mambo yasiwepo…tunapata hasara kubwa sana inapotokea umeme wa kukata na kuwasha leo Kariakoo muda fulani mpaka fulani hakutakuwa na umeme,” alisema.
Inasikitisha kuona wananchi wanaona kupatiwa huduma nzuri za kijamii kama msaada kutoka serikalini.
Inasikitisha kuona ahadi zinazotolewa na wanasiasa na viongozi mbalimbali zinavunjwa kila uchwao.
Je, tunajenga mahusiano gani kati ya Serikali na wananchi ikiwa ahadi zinazowekwa hazimitimizwi? Je, tunatarajia wananchi kuwa na imani na viongozi waliowadhamini kuwawakilisha kama hawawajibiki wala kutimiza majukumu yao?
Je, wananchi wataendelea kushiriki katika shughuli za kidemokrasia kama kupiga kura na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwa hawaoni serikali na viongozi waliowapa dhamana ya kuwawakilisha wakifanya kazi na kuwajibika kwa ajili yao?
Maswali haya na mengine ambayo nayatafutia majibu ni miongoni mwa maswali mengi yaliyonifanya nikaanza kufuatilia siasa. Siasa ni maisha yetu ya kila siku. Aidha unafuatilia masuala haya au la, bado mkono wake utakugusa.
Jane Shussa ni Ofisa Mwandamizi wa Mawasiliano ya Kidijitali wa Shirika lisilo la kiserikali la Twaweza. Haya ni maoni yake binafsi na wala si msimamo rasmi wa Nukta Habari.