Mahakama Tanzania ni mwendo wa kidijitali utoaji wa huduma
- Imeanza kutumia mifumo ya kielektroniki katika usajili na kuratibu mwenendo wa mashauri, Mawakili, makusanyo na utambuzi wa mahitaji ya mahakama nchini.
- Matumizi hayo yatasaidia kuharakisha utoaji wa haki kwa wakati na pia yanasogeza huduma za mahakama karibu zaidi na wananchi.
- Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma amuomba mpiga chapa mkuu wa Serikali kuchapisha sheria zote mtandaoni kurahisisha upatikanaji wake.
Dar es Salaam. Mhimili wa Mahakama nchini umeanza kutumia mifumo mbalimbali ya Tehama ili kutekeleza mpango wake wa kuwa mahakama mtandao (E-Justice) ili kuongeza wigo wa utoaji na upatikanaji wa haki Tanzania.
Mbali na kujiboresha katika uwekezaji wa Tehama, uongozi wa mhimili huo umemuomba mpiga chapa mkuu wa Serikali kuzichapisha sheria zote nchini katika mtandao ili wananchi wazipate kirahisi na kuzitumia kwa maslahi yao.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma aliyekuwa akizungumza leo (Februari 6,2019) katika maadhimisho ya wiki ya sheria yanayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini hapa amesema matumizi ya Tehama yana msaada mkubwa wa kuharakisha utoaji wa haki kwa wakati na pia yanasogeza huduma za mahakama karibu zaidi na wananchi.
“Tehama italeta mapinduzi ya haki pale tu mahakama itakaposhirikiana na wadau pamoja na wananchi,” amesema Profesa Juma.
Amebainisha kuwa mahakama ya Tanzania imetoka katika nadharia na sasa inajiendesha kwa vitendo kupitia mifumo mbalimbali ya Tehama inayo rahisisha utendaji wa shughuli za taasisi hiyo.
Mfumo wa kielektroniki wa usajili mashauri
Katika maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na Rais John Magufuli kama mgeni rasmi, Profesa Juma amesema mfumo huo wa kielektroniki wa kusajili mashauri umeanza kufanya kazi katika maeneo mbalimbali.
“Mfumo huu unawezesha kufanyika kwa urahisi kwa mambo mbalimbali ya mashauri kwa mfano kufungua shauri kieletroniki, kuitwa shaurini na hata kupata taarifa za shauri kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu au SMS,” amesema.
Kupitia mfumo huo unawezesha kuwa na benki ya kutunza nyaraka na hukumu zinazotolewa mahakamani na kuwa rahisishia wananchi kusoma hukumu zinazotolewa wakati wowote na popote walipo.
Tehama ikitumika vizuri inaweza kupunguza changamoto za ucheleweshaji wa kesi mahakamani na kuharakisha utoaji wa hukumu. Picha| Stock.
Mfumo huo unaosaidia pia ukusanyaji wa takwimu za mashauri, umeanza kutumika katika mahakama za Dar es Salaam, Mbeya, Dodoma na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo haita mlazimu mtu wa maeneo hayo kusafiri umbali mrefu kufungua shauri lake.
“Hata hivyo, baada ya muda mfupi mahakama zetu zote zitafikiwa na mfumo huu. Huu ni wakati wakujitayarisha tunatoka katika mfumo wa zamani tunaingia katika mfumo mpya,” amesema Profesa Juma.
Zaidi utawezesha kujua kila mahakama imefanya nini kila siku, kila Jaji na kila Hakimu amefanya nini kila siku, jambo likalosaidia kuwa na takwimu sahihi za ufanisi wa watumishi wa mahakama.
Mfumo wa kielektoniki wa utambuzi wa mahitaji ya mahakama
Mfumo huo ambao unatambulika kama ‘Court Maping’ ni hatua nyingine ya kuboresha mazingira ya utoaji haki, ambapo unawezesha kupata taarifa zote zinazohusu mahakama yoyote, watumishi, hali ya majengo na umbali wa mahakama husika.
Mfumo huo uliotayarishwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya mahakama na Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) utasaidia kudhibiti nidhamu na vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikishamiri katika taasisi hiyo muhimu inayotegemewa na wananchi kutoa haki.
“Waheshimiwa Majaji wa mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu na Wafawidhi kutoka kanda zote za Mahakama Kuu na divisheni pamoja watumishi wa kada zote hapa Tanzania wamepata semina elekezi kuhusu maboresho na mabadiliko hayo makubwa ya Tehama,” amesisitiza Profesa Juma.
Zinazohusiana:
- Tanzania yatajwa kwenye nchi 10 za mwisho matumizi ya Tehama
- Emanuel Feruz: Mtalaam wa Tehama aliyegeukia ujasiriamali wa kupiga picha
Mfumo wa kielektroniki wa makusanyo na ada
Kama ilivyo kwa taasisi nyingine, mahakama nayo imeanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa makusanyo na ada ambao tayari umeunganishwa na mfumo wa makusanya maarufu kama ‘Government Electronic Payment Gateway’.
Kwa mujibu wa Profesa Juma, mfumo huo ambao umeanza kutumika katika mkoa wa Dar es Salaam umeunganishwa na mfumo wa mashauri (case management system).
Pia unasaidia kudhibiti upotevu wa mapato kwa sababu kesi haiwezi kusajiliwa bila malipo kufanyika katika mfumo huo.
Mfumo wa usajili na kuratibu Mawakili
Matumizi ya Tehama kwa vitendo ya mahakama pia yanaoneka kwenye mfumo wa usajili na kuratibu mawakili unaoitwa TAMSI ambapo sasa wananchi wanaweza kuwafahamu mawakili wenye sifa na mahali walipo kupitia mtandaoni.
Mahakama inayotembea (Mobile Court)
Mahakama hiyo imezinduliwa leo na Rais John Magufuli itasaidia kuwaondolea changamoto wananchi ambao hawapati huduma za mahakama kwa wakati hasa katika maeneo ambayo hayana majengo.
Itaanza kufanya kazi katika mahakama za mwanzo za Bunju, Chanika, Buza na Kibamba mkoani Dar es Saam na katika Halmashauri za Wilaya za Ilemela na Nyamagana ambazo zinakabiliwa na upungufu wa majengo ya mahakama.
Rais John Pombe Magufuli akikata utepe kuzindua rasmi gari maalumu litakalotumika kama Mahakama inayotembea akiwa na Spika wa Bunge Job Ndugai (kulia) Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi. Wengine ni Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma, Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia nchini Bella Bird na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Sophia Mjema wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria leo Februari 6, 2019.
Utengenezaji wa mahakama hiyo inayoendeshwa kwa nguvu ya umemejua umegharimu zaidi ya Sh470 milioni kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na Serikali.
Mahakama hiyo inayotembea ni ya kwanza Afrika na ya tatu duniani ukiachilia mbali zilizopo Brazili na Guantemala, itakuwa na vifaa muhimu kama kabati la kutunzia nyaraka, printa, viyoyozi na kifaa cha kuwabeba watu kuingia ndani.
Mkurugenzi Mkazi wa Benki wa Dunia nchini Tanzania, Bella Bird amesema mahakama hiyo itarahisisha upatikanaji wa haraka wa haki kwa wananchi, mchakato wa kufungua kesi na kutunza kumbukumbu za mahakama.
Utekelezaji na usimamizi mzuri wa mifumo hiyo unaweza kusaidia kuifikisha mahakama katika mpango mkubwa wa kuwa mahakama mtandao au E-justice.