Magufuli kuzikwa Chato, ratiba ya kuagwa ikibadilishwa

March 20, 2021 8:24 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link

Mwili wa Hayati Rais Magufuli umefanyiwa ibada katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Peter Jijini Dar es Salaam. Picha| Mtandao.


  • Kabla ya kuzikwa Chato wananchi wa mikoa mbalimbali watapata nafasi ya kuaga mwili wa Hayati Magufuli.
  • Mwili utaanza kuagwa Dar es Salaam kwa siku mbili, Dodoma, Zanzibar, Mwanza na kisha Geita.
  • Mazishi ya mwili wa Hayati Rais Magufuli yatafanyika Machi 26, 2021 nyumbani kwake Chato.

Dar es Salaam. Ratiba ya mazishi ya aliyekua Rais wa Tanzania, John Magufuli imebadilishwa ambapo badala ya kuzikwa Machi 25 kama ilivyotangazwa awali, atazikwa Machi 26 mwaka huu wilayani Chato, Mkoa wa Geita.

Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali katika taarifa yake imeeleza kuwa viongozi wa Serikali na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam watashiriki ibada ya kuaga leo Jumamosi Machi 20, 2021 katika uwanja wa Uhuru. Ratiba ya kuaga mwili wa Dk Magufuli itaendelea kesho Machi 21 jijini humo kabla ya kusafirisha hadi jijini Dodoma.

Machi 22 mwaka huu wakazi na viongozi wengine wa Serikali watapata fursa ya kumuaga Dk Magufuli katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Siku hiyo kwa mujibu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan itakuwa ni siku ya mapumziko.

Siku inayofuata ya Machi 23 itakiwa ni zamu ya wananchi wa Zanzibar ambapo wataaga mwili wa Rais Magufuli na kisha utasafirishwa kuelekea Mwanza ambapo wakazi wa Mwanza na maeneo ya jirani watapata nafasi ya kuuaga mwili huo Machi 24, 2021.

Alhamisi ya Machi 25 itakuwa ni zamu ya wanafamilia na wananchi wa Chato na mikoa ya jirani. 

Safari ya mwisho ya Magufuli itahitimishwa Ijumaa Machi 26 katika nyumba yake ya milele nyumbani kwake Chato, mkoani Geita.

Enable Notifications OK No thanks