Magufuli awaachia ‘home work’ vigogo wa Tazara
- Awataka kupeleka mapendekezo ya namna ya kuboresha reli hiyo yenye uwezo wa kubeba tani zaidi ya milioni tano.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesafiri kwa treni ya Shirika la reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) akielekea Rufiji mkoani Pwani leo huku akiwaachia kibarua vigogo wa shirika hilo kupeleka mapendekezo yatakayosaidia kuboresha usafirishaji wa abiria na mizigo.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu iliyotolewa leo imeeleza kuwa Dk Magufuli amesema Serikali inatambua umuhimu wa Tazara na haiwezi kuiacha ikajiendesha kwa ufanisi mdogo usiokuwa na tija kwa Watanzania.
Tazara, moja ya miradi ya kwanza ya China barani Afrika, ina uwezo wa kubeba tani milioni tano kwa mwaka lakini Ikulu imeeleza kuwa kwa sasa inasafirisha tani 300,000 pekee kwa mwaka, kiwango ambacho ni pungufu mara 17 ya uwezo wake.
Tangazo

Mkurugenzi Mkuu wa Tazara Bruno Chingandu na Meneja wa Tazara Tanzania, Fuad Abdallah wamemweleza Rais Magufuli kuwa mapendekezo ya maboresho ya sheria zinazozihusu shirika hilo yameshawasilishwa serikalini ili kuiwezesha kila nchi mbia kuwekeza ili kuboresha usafiri wa abiria na mizigo.
Rais Magufuli, aliyeambatana na mkewe Janet Magufuli katika safari ya kwenda kuzindua mradi wa maporomoko ya maji wa Rufiji, amewaambia vigogo hao kuharakisha mchakato wa maboresho ya sheria hiyo ili kuruhusu ununuzi wa mabehewa na injini za treni ufanyike kwa haraka.
Reli ya Tazara, yenye urefu wa kilomita 1,860, imekuwa ikikabiliwa na changamoto lukuki za kiutendaji jambo lililofanya usafirishaji wake wa mizigo na abiria uwe chini ya kiwango kinachotakiwa kwa mwaka.
Latest
