Madeni tarajiwa ya Sh52.6 bilioni yazitesa wizara, idara za Serikali
- Madeni hayo tarajiwa yanatoka katika taasisi 11 ikiwemo Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo yanasubiri uamuzi wa mahakama.
- Madeni tarajiwa ni moja ya vyanzo vikuu vya vihatarishi vya kifedha kutokana na matarajio ya wajibu wa kulipa utakaotokana na matokeo tarajiwa.
- CAG amependekeza Serikali ihamasishe kila taasisi ya serikali iwe na mikakati thabiti ya usimamizi wa madeni kulingana na mazingira yao.
Dar es Salaam. Wakati mjadala wa Spika wa Bunge, Job Ndugai kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Juma Assad ajiuzuru kutokana na kuliita Bunge ‘dhaifu’ ukiendelea kwenye mitandao ya kijamii, ripoti yake imefichua Sh52.6 bilioni za madeni tarajiwa kutoka taasisi 11 za Serikali ikiwemo Wizara ya Maliasili na Utalii.
Madeni tarajiwa ni moja ya vyanzo vikuu vya vihatarishi vya kifedha kutokana na matarajio ya wajibu wa kulipa utakaotokana na matokeo tarajiwa.
Katika ripoti hiyo ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2017/18 kuhusu Serikali Kuu, CAG anasema amebaini taasisi 11 ambazo zina madeni tarajiwa yanayofikia kiasi cha Sh52.6 billioni zikisubiria maamuzi ya mahakama dhidi ya makampuni na watu binafsi.
Amesema kuna viashiria vya hatari katika kuongezeka kwa madeni tarajiwa kwenye wizara na idara za Serikali ambapo taasisi hazitengi bajeti kwa ajili ya madeni tarajiwa.
“Ikiwa inatokea madeni tarajiwa yanakuwa madeni itabidi yalipwe kutoka kwenye bajeti ya taasisi badala ya kutoa huduma na pia kuifanya taasisi isiwe na uwezo wa kifedha,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Soma zaidi:
- Bunge lamtenga rasmi CAG Assad
- CAG hajaiacha salama sekta ya utalii, aibua utofauti wa takwimu za watalii
- CAG: HESLB imeshindwa kuwapata wadaiwa wa Sh1.46 trilioni
Kiasi kikubwa cha madeni tarajiwa kipo katika Wizara ya Maliasili na Utalii kikiwa ni Sh23.4 bilioni sawa na asilimia 44 ya kiasi chote cha madeni tarajiwa ikifuatiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sh6.84 bilioni) na Wizara ya Kilimo yenye madeni tarajiwa Sh5.67 bilioni sawa na asilimia 11 ya madeni tarajiwa yote.
Taasisi nyingine ni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Sh2.6 bilioni), Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (Sh3.5 bilioni), Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi (Sh42 milioni) na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu (Sh21.8milioni).
Hali hiyo isipodhibitiwa, CAG anasema kuna hatari ya kuingia katika matumizi yasiyo na manufaa kwa wizara kutokana na faini au adhabu ambayo inaweza kuamriwa na mahakama kama wizara zitashindwa kesi hizi.
“Kama nilivyopendekeza katika taarifa zangu zilizopita, naendelea kupendekeza Serikali ihamasishe kila taasisi ya serikali iwe na mikakati thabiti ya usimamizi wa madeni kulingana na mazingira yao kwa ajili ya kuhakikisha hatari zilizopo katika taasisi zao zinasimamiwa na kupunguzwa mpaka kufikia kiwango cha kudhibitiwa,” inapendekeza ripoti hiyo ya CAG ambayo ilitolewa kwa umma Aprili 10, 2019.
Latest