Maagizo matano ya Magufuli kukuza uchumi wa viwanda nchi za SADC

August 5, 2019 10:24 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Amezitaka nchi wanachama kuwekeza zaidi kwenye teknolojia rahisi ya viwanda na kukuza ubunifu wa wananchi. 
  • Amezitaka kuondoa vikwazo vya kibiashara na kuiwezesha sekta binafsi kuwekeza katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameelekeza mambo mbalimbali yanayotakiwa kufanywa na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) yatakayosaidia kujenga uchumi wa viwanda ikiwemo kuhimiza matumizi ya teknolojia rahisi na kuondoa vikwazo vya kibiashara katika nchi za jumuiya hiyo. 

Dk Magufuli, aliyekuwa akizungumza leo (Agosti 5, 2019) jijini Dar es Salaam wakati akifungua rasmi Maonesho ya nne ya Wiki ya Viwanda ya SADC, amesema mapinduzi ya viwanda ni njia ya lazima kuelekea ukombozi na kukuza uchumi wa Afrika. 

Maonesho hayo ni utangulizi wa mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi 16 za SADC utakaofanyika Agosti 17 hadi 18, 2019.

Amesema ili kufikia azma hiyo ya kujenga uchumi imara wa viwanda na kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya Afrika, nchi za SADC zinatakiwa kuwekeza zaidi katika ukuzaji wa teknolojia ya viwanda na matumizi ya malighafi ili kutengeneza bidhaa zenye ubora zitakazouzwa ndani na nje ya Afrika.  

“Sanjari na hili tuuziane bidhaa na malighafi miongoni mwetu ili tukuze mtaji na kuendeleza viwanda ndani ya jumuiya yetu na bara letu…kama Namibia wanahitaji mahindi tuwapelekee mahindi, kama Afrika Kusini wanahitaji korosho tuwapelekee tusiagize mahali pengine,” amesema Rais Magufuli. 

Amesema viwanda hivyo vitafaidika na soko la SADC lenye watu takriban milioni 350 kutoka katika nchi wanachama 16 ambao watakua wanatumia bidhaa hizo. 


Soma zaidi: Tanzania inavyofaidika na mahitaji ya kiuchumi ya SADC


Nchi hizo za SADC pia zimetakiwa kuendeleza ubunifu wa watu na kuhamasisha matumizi ya teknolojia rahisi katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji. 

“Tuna vijana wengi  wenye vipaji vikubwa katika sayansi na teknolojia lakini badala ya kutumia sayansi na teknolojia hii tunakimbilia kwenye mataifa mbalimbali na kununua teknolojia kwa gharama kubwa, wakati mwingine isiyosawili na mazingira yetu,” amesema Rais.

Sambamba na hilo ni kuhimiza zaidi ujenzi wa viwanda vidogo vidogo kwa sababu vinagusa maisha ya watu wengi ambavyo vikiwekewa mikakati vinaweza kuwa viwanda vikubwa. 

Pia ameshauri kuelekeza zaidi nguvu katika kujenga mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza sekta ya viwanda ikiwemo kuongeza miundombinu na upatikanaji wa nishati ya umeme na kuondoa vikwazo vyote kwa wawekezaji.

Aidha, amezitaka kushughulikia vikwazo vyote vinavyochelewesha maendeleo ya viwanda ndani ya SADC na Afrika visivyo na maana ikiwemo utitiri wa taasisi za udhibiti, kodi, tozo, urasimu wa taratibu za uwekezaji, vikwazo vya mipakani. 

Rais Magufuli ambaye ni mwenyekiti mtarajiwa wa SADC, amesema katika uchumi wa viwanda, sekta binafsi haiepukiki hivyo ni jukumu la Serikali za nchi za jumuiya hiyo kuboresha mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Sehemu ya mkutano wa Wiki ya Viwanda unaofanyika Jijini Dar es Salaam. Picha|Mtandao.

Hata hivyo, ameitaka sekta binafsi iache kulalamika badala yake ijikite katika kutatua changamoto za uwekezaji na kuongeza uzalishaji na ajira kwa wananchi wa jumuiya hiyo.

Washiriki wapatao 3,001 kutoka nchi za SADC ikiwemo Tanzania wanashiriki Wiki ya Viwanda kabla ya kufanyika mkutano wa Wakuu wa nchi za jumuiya hiyo Agosti 17 na 18, 2019. 

“Jumla ya waonyeshaji ni 1576 ambapo watanzania ni 1004  waliotoka nje ya Tanzania ni 172. Maeneo yanayotumika katika maonyesha haya; eneo liliko mbele ya ukumbi huu wa mikutano (Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere-JNICC) lakini pia eneo la Karimjee na eneo la viwanja vya Gykhana,” amesema Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa wakati akitoa maelezo ya maonyesho hayo. 

Enable Notifications OK No thanks