Lucy, katuni aliyejizatiti kupunguza mimba za utotoni Morogoro

August 29, 2018 9:49 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Itasaidia kupunguza mimba za utotoni na kuongeza idadi ya wasichana walioelimika.
  • Katuni za 3D zitatumika kutoa elimu ya uzazi wa mpango.
  • Wadau kushirikiana kuwafikia wasichana shule za sekondari.

Dar es Salaam. Mimba za utoto bado ni tatizo kubwa linalowakumba wasichana wengi wa Tanzania na kulazimika kuacha masomo na kwenda kulea watoto au kuolewa katika umri mdogo.  

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) za kati ya mwaka 2010 na 2017, Tanzania ni ya tatu kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni baada ya Sudan Kusini na Uganda. Sudan Kusini kiwango cha watoto wa chini ya miaka 18 wanaoolewa ni asilimia 52 na nchini Uganda ni asilimia 40. Tanzania ni asilimia 31.

Hata hivyo, UNICEF inaeleza kuwa kuna mafanikio makubwa ya kupungua kwa ndoa za utotoni duniani ambazo husababishwa zaidi na mimba za utotoni, ambapo kwa sasa ni msichana mmoja kati ya watano anaolewa chini ya miaka 18 tofauti na miongo iliyopita ambapo ilikuwa msichana mmoja anaolewa kati ya wanne.

Kulingana na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, mtu yeyote aliye chini ya miaka 18 anahesababika kuwa ni mtoto ambaye anahitaji kulindwa na hatari zote zinazoweza kuhatarisha ustawi wa maisha yake. 

Katika kuhakikisha mimba na ndoa za utotoni zinatokomezwa katika jamii, Shirika la TAI Tanzania limeamua kutumia teknolojia ya utengenezaji wa katuni za 3D kutoa elimu ya uzazi wa mpango na kuwajengea uwezo wanafunzi wa kike kukabaliana na mimba na ndoa za utotoni.

Katuni za 3D huwa katika mfumo wa video (Animation Cartoon) ambapo hutengenezwa kwa njia mbalimbali ikiwemo kuchora kwa mkono kila fremu kama katuni za zamani zilijulikana kama ‘Disney’. Wengine hutumia picha mgando (Stop-motion animation) ambapo picha huungwa na kutengeneza video kwa kutumia programu ya ‘Blender’ inayowekwa kwenye kompyuta.

 Elimu hiyo itatolewa chini ya mradi wa “Harakati za Lucy” kwa kushirikiana na wataalamu kutoka taasisi ya Maria Stopes na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) ambapo wanatarajia kuwafikia wanafunzi wa shule za sekondari zilizopo maeneo ya vijijini  mkoani Morogoro.


Inayohusiana: Kutana na shangazi roboti wa Tanzania aliyepania kutokomeza mimba za utotoni.


Kwa mujibu wa Meneja Rasilimali Watu wa Tai Tanzania, Gwamaka Mwabuka anasema wamechagua Morogoro kutokana kuwa na viwango vikubwa vya mimba za utotoni na kupitia mradi huo watapunguza mimba za utotoni na kuongeza idadi ya wasichana wanaoelimika.

‘Harakati za Lucy’ ni jina la katuni zinazomuonyesha msichana Lucy ambaye ameamua kusoma ili kufikia malengo yake kielimu akipinga mimba za utotoni na kuwahamasisha wasichana wengine nchini kukataa vitendo vya ukatili wa kijinsia. 

“Tutaenda kutembelea mashule na kufanya mijadala itakayo husisha wanafunzi, walimu pamoja na wataalamu mbalimbali kama Marie stopes Tanzania na UNFPA,” amesema Mwabuka.

Kwa kutumia katuni ya 3D, “Harakati za lucy” inategemewa kuwa na filamu fupi 12 zisizozidi dakika 10 hivyo kutumia dakika takribani 120 kwa kila shule watakayotembelea kutoa elimu ya uzazi. 

                            Video ya awali ya katuni ya “harakati za Lucy” itakayo tumika kuelimisha juu ya elimu ya uzazi wa mpango na kutokomeza mimba za utotoni. Video| Tai Tanzania.

Katuni hiyo itaweza kuwafikia wasichana wengi mkoani Morogoro hata katika maeneo ambayo hayajapitiwa na umeme wa gridi ya taifa. Teknolojia hiyo itaendeshwa zaidi na umemejua  ambao ni rafiki kwa mazingira.  

“Mtoto wa kike yuko katika hatari ya kukosa masomo hasa pale anapopata ujauzito au anapokuwa kwenye kipindi cha hedhi jambo lililotofauti kwa mtoto kiume,” amesema Mwabuka ambaye kupitia TAI wanakusudia kutoa mchanga wao wa elimu ya uzazi kupunguza mimba za utotoni nchini. 

Mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa Septemba mwaka huu. Katuni za 3D pia zitaonyeshwa katika vituo vya runinga ili kuwafikia wasichana wengi nchini.

Aidha viongozi duniani wamejizatiti katika Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya kutokomeza ndoa za utotoni ifikapo mwaka 2030 na kuzitaka nchi wahisani kubuni njia mpya kukabiliana na vitendo vyote vinavyowadhalilisha wasichana na wanawake.

Enable Notifications OK No thanks