Lindi, Mtwara zinavyochuana kidato cha sita
- Mikoa ya Lindi na Mtwara toka mwaka 2017 hazijawi kushuka nafasi ya tatu.
- Mkoa wa Lindi mwaka huu 2019 umefaulisha wanafunzi wote kwa asilimia 100 kama ilivyofanya Mtwara mwaka 2018.
Dar es Salaam.Katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) wiki hii, yameuweka mkoa wa Lindi katika nafasi ya kwanza kitaifa kwa mpangilio wa ufaulu wa mikoa 29 iliyoshiriki mtihani huo.
Lindi imeshika nafasi ya kwanza baada ya kupanda kutoka nafasi ya pili iliyoshikilia mwaka 2018 na kuushusha mkoa jirani wa Mtwara kwa nafasi mbili kutoka namba mmoja mwaka 2018 hadi nafasi ya tatu mwaka huu.
Mafanikio iliyopata Lindi, siyo tu ni somo kwa mikoa mingine bali kwa wadau wa elimu kuwekeza zaidi katika elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa sahihi kuwawezesha kujibu mtihani.
Uchambuzi uliofanywa na www.nukta.co.tz wa mpangilio wa mikoa kwa ubora wa ufaulu katika mtihani wa kidato cha sita uliotolewa na Necta mwaka 2019 unaonyesha kuwa siyo tu Lindi imeongaza kitaifa bali wanafunzi wake wote wamefaulu kwa asilimia 100.
Wanafunzi wote 953 waliofanya mtihani huo kutoka katika shule tisa za mkoa huo wamefaulu kwa kupata kati ya daraja la I hadi IV na hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyepata daraja sifuri.
Hali imekuwa ni tofauti na mwaka uliopita (2018) ambapo mkoa huo ulishika nafasi ya pili kitaifa huku ukifaulisha kwa asilimia 99.59 ambapo wanafunzi 733 kutoka shule nane walifaulu kwa kupata kati ya daraja la I hadi IV.Wanafunzi watatu tu walipata daraja sifuri kati yao wawili walitoka Shule ya Sekondari Mahiwa na mmoja alitoka Seminari ya Namupa.
Shule ya Sekondari Lindi iliyopo mkoa wa Lindi ambayo nayo imefanya vizuri katika mkoa huo. Picha|Mtandao.
Kwa mujibu wa viwango vya ufaulu vya Necta wanafunzi wanaopata daraja la I hadi la IV wanahesabika wamefaulu na wana sifa ya kupata cheti na kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
Katika matokeo hayo yalitangazwa alhamisi (11 julai 2019) yanaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya wanafunzi wamepata daraja la pili, sawa na asilimia 57 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani huo mkoani humo.
Kwa upande wa daraja IV ni wanafunzi sita tu walifaulu katika daraja hilo sawa na asilimi 0.6 huku daraja la III wakiwa wanafunzi 175.
Wakati Mkoa wa Mtwara ukipigwa kikumbo na Lindi, nao bado uko katika nafasi nzuri ambapo mwaka huu umeshika nafasi ya tatu kitaifa nyuma ya Mkoa wa Singida uliopanda kutoka nafasi ya saba mwaka 2018.
Huku pia asilimia ya wanafunzi waliopata daraja II ikishuka hadi kufikia asilimia 48.3 mwaka 2019 kutoka asilimia 56 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani huo. Lakini wanafunzi waliopata daraja IV mwaka 2019 wameongezeka kutoka wanafunzi 11 mwaka 2018 hadi 18 mwaka huu ambapo waliopata sifuri ni sita.
Zinazohusiana:
- 10 bora kidato cha nne, sita shule za Serikali inavyofikirisha
- Shule zinavyochuana kubaki katika 10 bora kidato cha sita.
Matokeo hayo ni ya kubahatisha?
Historia ya ufaulu wa elimu katika ya mikoa hiyo ya Lindi na Mtwara siyo ya kubahatisha ni ya muda kidogo na nyakati zote wanafunzi wake wamekuwa wakifaulu.
Takwimu za Necta zinaonyesha kuwa kwa miaka mitatu iliyopita, mikoa hiyo imekuwa ikishikilia nafasi tatu za juu katika ubora wa ufaulu kwa mikoa.
Mwaka 2017 mkoa wa Lindi ulishika nafasi ya pili sawa sawa na mwaka jana kabla ya kupanda hadi katika nafasi ya kwanza mwaka huu.
Kwa upande wa Mtwara, mwaka 2017 ulishika nafasi ya tatu kitaifa na mwaka uliofuatia ikawa ya kwanza kabla ya kushuka hadi nafasi ya tatu mwaka huu.
Matokeo hayo yameibua shangwe kwa viongozi wa mkoa huo, akiwemo Mbunge wa Mtama mkoani Lindi, Nape Nnauye ambaye katika ukurasa wake wa Twitter ameandika,
“Mwenyezi Mungu hakunyimi kila kitu! Mkoa wa Lindi umekuwa wa Kwanza kitaifa matokeo ya kidato cha sita. Na kati ya wanafunzi kumi bora kitaifa mmoja katoka jimbo la Mtama, Shule ya Sekondari Nyangao!.”
Siku chache kabla ya kufanyika kwa mtihani wa kidato cha sita mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara aliambia www.nukta.co.tz kuwa ufaulu mzuri katika mkoa wake unachangiwa na ushirikiano baina ya walimu, wanafunzi na viongozi wa mkoa huo kufuatilia masomo darasani.