LHRC yataka hatua za haraka kuwalinda maalbino
- Yashtushwa na matukio ya kuwadhuru yaliyoripotiwa hivi karibuni.
- Yataka walindwe na watuhumiwa wa mauaji wachukuliwe hatua.
Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, (LHRC) kimeonya kuwa hatua za haraka zisipochukuliwa kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), maisha yao yatakua hatarini baada ya vitendo vya ukatili dhidi yao kuanza kuibuka tena.
Kati ya mwaka 2021 hadi kufikia Novemba 7, 2022, matukio matano ya mauaji ya watu wenye ualbino yameripotiwa katika mikoa yaDar es Salaam na Mwanza, hali inayoibua hofu ya usalama kwa kundi hilo.
Mkurugenzi wa LHRC Anna Henga aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 7, 2022 amesema sababu kubwa inayosababisha kuendelea kwa mauaji hayo ni imani za kishirikina.
“Ni wazi kuwa soko haramu la viungo vya watu wenye ualbino (black market) linalohisiwa kuratibiwa na waganga wa kienyeji bado lipo kutokana na uendelevu wa imani za kishirikina katika jamii,” amesema Henga.
Tukio la mwisho la mauaji ya mtu mwenye ualbino limemuhusisha Joseph Mathias (50) aliyevamiwa na wahalifu waliomkata mkono na kusababisha kifo chake usiku wa kuamkia Novemba 2, 2022 mkoani Mwanza.
Kituo cha #Sheria na #Haki za #Binadamu (#LHRC) kushirikiana na chama cha Watu Wenye Ualbino #Tanzania (#TAS) wametoa tamko kulaani #Mauaji ya Bwana Joseph Mathias (50), ambaye alivamiwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia tarehe 2 #Novemba 2022, nyumbani kwake akiwa amelala. pic.twitter.com/5r1KXUFtH9
— LHRC (@humanrightstz) November 7, 2022
Kufutia tukio hilo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ametoa siku saba kwa Jeshi la Polisi mkoani humo kuwasaka wahaifu huku LHRC ikisema taarifa za wazi kuhusu mwenendo wa tukio hilo zitolewe.
“Tunatoa wito kwamba mrejesho utolewe waziwazi ili kuondoa taharuki na hali ya uoga kwa kundi hili la watu wenye ualbino,” amesema Henga.
Kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2015 mpaka 2020 hakukuwa na matukio ya mauaji ya watu wenye ualbino nchini. Matukio yaliyoanza kujitokeza sasa dhidi ya kundi hilo yamewaibua wadau wa haki za binadamu wanaotaka hatua zaidi zichukuliwe.
Soma zaidi:
-
Uchunguzi chanzo ajali ya ndege Ziwa Victoria waanza
-
COP27: Afya iwe kitovu majadiliano ya mabadiliko ya tabianchi
Komesheni mauaji ya albino
Wadau hao wakiwemo LHRC, Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TSA) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) wamependekeza jitihada za pamoja kutoka kwa Serikali, asasi za kiraia, viongozi wa dini na wananchi kupinga mauaji hayo.
“Tunatoa wito kwa Jeshi la polisi na Serikali kuhakikisha kuwa watuhumiwa wa kesi hizi wanakamatwa, upelelezi unafanyika kwa wakati na wanafikishwa mahakamani na kupatiwa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine,” amesema Henga.
Kituo hicho pia kimeiomba Serikali kuridhia Mkataba wa Afrika wa Haki za Watu Wenye Ulemavu uliopitishwa na Umoja wa Afrika (AU) mwaka 2018.
Mkataba huu umetazama haki za watu wenye ulemavu katika mazingira halisia ya Kiafrika ikiwemo kutambua changamoto ya imani potofu zisababishazo madhira dhidi ya watu wenye ualbino.
Kwa upande wa taasisi na viongozi wa dini, LHRC imewataka kuongeza juhudi katika kuwafundisha waumini wao na jamii kwa ujumla kuhusu utu wa watu wenye ualbino na kuwaonya kuachana na imani za kishirikina na tamaa zenye kudhuru binadamu wenzao.
Wananchi nao wametakiwa kuheshimu haki za kila mtu na kuzilinda.
“Haki ya kuishi na haki ya kuwa huru dhidi ukatili ni haki za binadamu ikiwemo watu wenye ualbino ni haki za kikatiba. Hivyo kuua na kukata viungo vya watu wenye ualbino ni makosa ya jinai,” amesema.
Sambamba na hilo jamii imekumbushwa kupuuzia imani potofu za kishirikina za kuwaua na kuuza viungo vya albino na kwamba watu wenye ualbino ni binadamu kama binadamu wengine.
“Ni uongo na upotofu mkubwa kusema kwamba viungo vyao vinaweza kumtajirisha mtu, Hivyo wasiwe wepesi kuwaamini waganga wa kienyeji wanapowaagiza kuwadhuru binadamu wenzao kwa ajili ya viungo hivyo,” amesisitiza Henga.
Latest
