Kwanini ukague usafi wa chumba cha hoteli kabla ya kutumia?
- Usafi wa chumba unachotumia ni muhimu kulinda afya yako isidhurike unapokuwa safarini.
- Hakikisha kitanda na vifaa vingine ni visafi.
- Wakati mwingine fungua madirisha ya chumba chako kuruhusu hewa safi kuingia.
Kusafiri ni njia mojawapo ya kujifunza mambo mbalimbali kwa kuona na hata kusikia. Lakini safari yenye mafanikio hutegemea zaidi usalama wa eneo unalofikia ikiwemo afya na mazingira yanayokuzunguka.
Wasafiri wengi wamekuwa wakifikia katika hoteli na nyumba za kulala wageni (lodges). Lakini unahakikishaje chumba cha hoteli unacholala ni kisafi kwa ajili ya kukufanya ufurahie safari yako?
Fanya haya wakati ukiwa katika chumba cha hoteli ili kukifanya kiwe nadhifu na kukuhakikishia usalama wa mwili na akili yako:
Kagua chumba kabla ya kuanza kutumia
Ukiingia kwenye chumba cha hoteli ni vema ukafanya ukaguzi mdogo hasa kitanda, makochi na sehemu kuogea ili kufahamu kama mazingira ni salama kwako.
Licha ya kuwa hoteli nyingi huzingatia viwango vya usafi, lakini una wajibu wa kuhakikisha hali ya chumba chako inakuruhusu kukaa na kutimiza majukumu yako bila vikwazo vyovyote.
Wakati mwingine vyumba vya hoteli vinakaa muda mrefu bila kutumika, jambo linaloweza kuibua changamoto za usafi, ambazo ni muhimu kuzishughulikia mapema kuilinda afya yako.
Soma zaidi:
- Waziri Kanyasu ataka tathmini ifanyike ajira hoteli za kitalii Tanzania
- Hizi ndizo sababu kwanini hoteli zinatumia mashuka meupe
Beba shuka lako wakati wa safari
Kitanda unacholalia ni muhimu kiwe kisafi kwa sababu kinatumika zaidi ukiwa katika hoteli. Ni kweli mashuka ya hotelini yanasafishwa mara kwa mara lakini ni vema na wewe ubebe lako ili ikitokea dharura unaweza kutumia.
Hili pia linaambatana taulo la kujifutia baada ya kuoga. Wapo baadhi ya watu ambao wanapendelea kutumia mataulo yao. Basi ni vema ukabeba ili uwe huru kutumia vyako.
Beba dawa za kuua wadudu (Anti-bacterials)
Unashauriwa kubeba dawa za kuua wadudu kama mbu, bakteria ili kuhakikisha unapokua kwenye chumba cha hoteli unajihamu na hatari yoyote inayoweza kutokea kwa mwili wako.
Hata hivyo, unatakiwa kuwa makini wakati ukitumia dawa hizo hasa unapopulizia kwenye simu, vitasa vya mlango, swichi za taa,rimoti za runinga na radio.
Ukaguzi wa chumba cha hoteli ni muhimu kabla hujaanza kutumia ili kujihakikishia usalama wako. Picha|Mtandao.
Hakikisha kuna mwanga wa kutosha chumbani
Mwanga wa kutosha kutoka nje ni muhimu kwani unasaidia katika kuhakikisha mahali ni salama na kuleta hewa nzuri katika chumba kwajili ya afya.
Wakati mwingine fungua madirisha ya chumba chako ili kuruhusu hewa iingie ili kupata utlivu na upepo mwanana kwa ajili ya afya yako.
Lakini unapaswa kuwa na tahadhari kwa sababu madirisha yakikaa muda mrefu, wadudu wanaweza kuingia na hewa chafu ikakudhuru.