Watoto hatarini, chakula kisichokuwa salama

June 10, 2026 2:40 pm · Method Allen
Share
Tweet
Copy Link
  • Chakula kisicho salama husababisha takribani visa milioni 866 vya magonjwa.

Dar es Salaam. Kila siku maelfu ya watoto huanza siku zao kwa kula chakula ambacho wazazi wao wanaamini ni salama. 

Hata hivyo, nyuma ya mlo huo kunaweza kujificha vimelea na kemikali hatarishi zinazoweza kusababisha magonjwa makubwa, kudhoofisha ukuaji wao na hata kuhatarisha maisha yao. 

Wakati dunia ikiendelea kupambana na changamoto za lishe na afya ya watoto, tatizo la chakula kisicho salama limeibuka kuwa adui wa kimya anayewaathiri mamilioni ya watoto, hususan wale walio chini ya miaka mitano. 

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inakadiriwa kuwa chakula kisicho salama husababisha takribani visa milioni 866 vya magonjwa na vifo milioni 1.5 kila mwaka, ambapo bara la Afrika na Asia ya Kusini Mashariki ndiko kuna athirika zaidi.

Ripoti hiyo ya WHO inabainisha kuwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ndio kundi lililo katika hatari kubwa zaidi ikiwa ni wanauwezo wa kupata magonjwa yanayotokana na chakula kisichokuwa salama mara tatu zaidi ukilinganisha na rika nyingine. 

Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dk. Ladislaus Kasankala, amesema kuwa uelewa wa wananchi kuhusu elimu ya chakula salama bado ni changamoto kubwa katika jamii, hali inayochangia vyakula vinavyo andaliwa kutokuwa salama kwa waandaaji na walaji.

“Vyakula vingi vinavyoandaliwa kwa sasa hutayarishwa na wajasiriamali wadogo. Endapo hawatazingatia kanuni za usalama wa chakula, watoto na wananchi wengine wanaweza kula vyakula visivyo salama, jambo ambalo linaweza kusababisha madhara mbalimbali kiafya,” amesema Kasankala

Dk Kasankala ameongeza kuwa wakati wa kuandaa chakula cha mtoto, ni muhimu kuzingatia viwango vya juu vya usalama na usafi, mazingira ya kuandalia chakula, ikiwemo jikoni, vyombo vinavyotumika ni safi wakati wote.

Aidha, WHO imeongeza kuwa vihatarishi vya kibaolojia, ikiwemo bakteria na virusi vinavyosababisha magonjwa yatokanayo na chakula pamoja na maambukizi ya vimelea, kulichangia idadi kubwa ya wagonjwa wa magonjwa yatokanayo na chakula, takribani watu milioni 860 mwaka 2021.

Kwa upande mwingine, vihatarishi vya kemikali vilichangia kwa kiwango kikubwa zaidi vifo vinavyotokana na chakula kilichochafuliwa.

Mwaka 2021, vihatarishi vya kemikali vilihusika na asilimia 73 ya vifo vyote vilivyosababishwa na chakula kisicho salama, aseniki isiyohai (inorganic arsenic) (asilimia 42) na risasi (asilimia 31). 

Ili afya ya mtoto iendelee kuimarika ni muhimu kwa mzazi/mlezi kuhakikisha anampatia mtoto chakula kilicho salama. Picha| Canva.

Hali hii ilitokana na ukweli kwamba kemikali hizo huongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo pamoja na saratani mbalimbali. 

Mtaalamu wa Lishe na Afya kutoka Hospitali ya Besta, Kokushubira Bijana, amesema hata maziwa ya mama yaliyokamuliwa yanaweza kuwa chanzo cha magonjwa kwa mtoto endapo hayatahifadhiwa na kushughulikiwa kwa usalama unaotakiwa. 

Aidha, amewashauri wazazi kuwaandalia watoto vitafunwa vyenye afya kama matunda na karanga badala ya vyakula visivyo na lishe ya kutosha, ili kuwakinga dhidi ya utapiamlo na ongezeko la uzito kupita kiasi.

Ameeleza kuwa ulaji wa chakula kisicho salama au kilichochafuliwa unaweza kuwaweka watoto katika hatari ya kupata matatizo ya afya kama utapiamlo, kuhara na kudumaa kwa ukuaji, hali ambayo inaweza kuathiri maendeleo yao na wakati mwingine kusababisha vifo.

Ingawa watoto wadogo wanachangia takribani asilimia tisa tu ya idadi ya watu duniani, wanabeba karibu theluthi moja ya visa vyote vya magonjwa yatokanayo na chakula. 

Kwa ujumla, usalama wa chakula si suala la uchaguzi binafsi pekee, bali ni jukumu la pamoja linalohitaji elimu, uangalizi na hatua madhubuti ili kulinda kizazi kijacho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Sin

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Sin

Nukta TV

Mizinga ya heshima, Rais Samia akimpokea Rais wa Singapore, Ikulu Dar es Salaam

Mizinga ya heshima, Rais Samia akimpokea Rais wa Singapore, Ikulu Dar es Salaam

Nukta TV

Mikakati ya Serikali kuhakikisha walimu wa VETA wanapata ajira na mikopo

Mikakati ya Serikali kuhakikisha walimu wa VETA wanapata ajira na mikopo

Nukta TV