Kutana na shangazi roboti wa Tanzania aliyepania kutokomeza mimba za utotoni
- Wamiliki wa shangazi roboti wanaeleza kuwa anawahudumia wanawake wengi zaidi kuliko wanaume.
- Eshangazi anapatikani kwenye Facebook Messenger.
- Ana mhakikishia kijana faragha ya mazungumzo baina yake.
- Kuna wakati shangazi huyo huzidiwa na maswali na kumfanya ashindwe kuwajibu watoto wake kwa wakati.
Dar es salam. Utaweza kumpiga chenga shangazi kwa muda mrefu lakini kuna wakati kutokana na mila nyingi za kitanzania hutaweza kumkwepa. Hakuna namna tena mazingira na tamaduni zitakufanya tu ukutane naye.
‘’Mila zetu nyingi mtu akitaka kuoa au kama akipata mchumba anawajibika kumueleza shangazi kwanza alfu shangazi ndio anaongea na wazazi,’’ anasema Meneja Mradi wa eshangazi, Dorah Ndazi.
Ndazi na timu yake ya kampuni inayochipukia ya Index Lab wameubeba mtazamo huo wa shangazi na kuuleta kwenye teknolojia. Kama utamkwepa shangazi wa nyumbani basi utakutana naye wa mtandaoni. eshangazi imetokana na tafsiri ya Kiingereza ya ‘elentronic shangazi’ yaani shangazi wa kielektroniki.
“Eshangazi amebuniwa ili afanye kazi kama za shangazi kwenye jamii lakini sasa kwa kutoa habari, elimu na ushauri kuhusu afya ya uzazi na jinsia kwa vijana kuhusu mimba za utotoni kupitia Facebook Messanger ,’’ anasema Ndazi.
Tofauti na shangazi wa familia ambaye mtu anaweza kuonana naye ana kwa ana ama kwa kumpigia simu, eshangazi anapatikana kupitia Facebook Messenger ambapo mtumiaji akishajiunga anaweza kuteta naye moja kwa moja kwa kumuuliza maswali ya wakati wa kuchati. Katika mazungumzo hayo eshangazi hujibu maswali yote yote kuhusu haki yake ya afya ya uzazi, uzazi wa mpango.
Yeye siyo binadamu kama ambavyo wengi wangedhani. Ni roboti aliyefundishwa kung’amua maswali ya watu juu ya afya ya uzazi na kuna wakati anaweza hata kukutajia vituo ambapo unaweza kupata huduma za masuala hayo. Lengo la roboti huyo ni kupunguza mimba za utotoni na kuhakikisha vijana wanapata taarifa sahihi za masuala yanayowahusu.
Shangazi huyo roboti anapatikana kupitia Facebook Messenger kwa wale wanaomiliki simu janja (smartphones) na hujibu maswali papo kwa papo. Picha|eshangazi.
Kwa mujibu wa Index Lab, shangazi huyo wa mtandaoni mwenye kaulimbiu ya “Njoo tutete” au tuzungumze ana mhakikishia kijana faragha baina yake kwenye mazungumzo hayo ambayo vilevile yameizinishwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za afya.
Ndazi anasema mwanzoni haikuwa rahisi eshangazi kueleweka kwa watu maana yeye yupo katika mfumo wa roboti na wakati huo kilikuwa kitu kipya ndani ya jamii ukilinganisha na sasa ambapo wamepata mafanikio.
“Wakati mfumo wa eshangazi unaanza ulikuwa na wafuasi 900 tu katika Facebook sasa kuna wafuasi 18,000 huku takwimu zikituonyesha watumiaji wengi ni wanawake kuliko wanaume,” anasema Ndazi.
Ndazi anasema eshangazi ilianza kama wazo tu mwaka 2017 na kuchepua hasa baada ya Sahara Ventures wakishirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) kuanzisha shindano la Amua Acceletor lenye lengo la kutatua changamoto zinawakabili vijana na jinsia.
“Tulifanikwa kuwa miongoni mwa washindi nne kati ya sita na kupata hela kukuzia wazo (seedfund) ya dola za kimarekani 6,000 zaidi ya milioni 13 za kitanzania kutoka shirika la watu dunia ili kufanya wazo letu kutekelezeka,” anaeleza.
Tofauti na ilivyokuwa awali, mfumo huo sasa umeongezewa majukumu kuliko ilivyokuwa hapo awali baada ya kuwekwa kipengele cha wataalamu (experts referral) ambapo mtumiaji anaweza kushauriwa na wataalamu kwa njia ya simu kama eshangazi atashindwa kumsaidia.
Vile vile kuna mchezo wa maswali na majibu mtu anaweza kujifunza kuhusu afya ya uzazi na mimba za utotoni huku akijiburudisha kwa michezo hiyo.
eshangazi huyo anaweza kukujibu maswali yote unayouliza kuhusu afya ya uzazi. Picha|eshangazi.
Hata hivyo, shangazi kuna wakati anazidiwa na maswali ya mashangazi zake. Changamoto kubwa inayokabili mfumo wake eshangazi wakati mwingine kuchelewa kujibu maswali kwa muda mwafaka kutokana na kuzidiwa na maulizo.
“Utakuta ameulizwa maswali zaidi ya 300 au 400 kwa wakati mmoja hiyo kupelekea majibu kuchelewa na muda mwingine inawezekana mfumo umepata hitilafu,’’ anaeleza Ndazi na kwamba kwa “sasa tunafanya jitahada za kurekebisha jambo hilo”anasema Ndazi
Pamoja na kuwa msaada kwa vijana wengi nchini, eshangazi hajaanza kutengeza hela ila Ndazi anasema wanategemea kuingiza mapato kupitia matangazo kutoka kwa kampuni mbalimbali zitakazovutiwa kutangaza nao.
Ndazi anasema ili kuhakikisha eshangazi anaishi miaka mingi zaidi, lengo lao ni kuona mwaka huu wanaanza kutengeza mapato.
Shangazi huyo wa kimtandao ana ongea lugha ya Kiswahili na ania ya kufika katika nchi zote wanazozungumza lugha hiyo na kwa sasa ametimiza mwaka mmoja toka kuanzishwa kwake Agosti 2017.
Ukimkosa shangazi wa kwenye familia yenu, roboti huyu anaweza kuwa shangazi wako wa karibu wakati wote kwa kukushauri masuala ya afya ya uzazi. Picha|eshangazi.