Kutana na baiskeli ya kuuzia ‘ice cream’ inayotumia umemejua
- Ni teknolojia inayokuja kuboresha kuuza bidhaa baridi kwa kutumia deli dogo linalotunza ubaridi kwa muda mfupi.
- Wameanzisha teknolojia hiyo kwa lengo kuu la kuwasaidia wafanyabiashara kutunza bidhaa hiyo kwa muda mrefu isiharibike wakiwa barabarani.
- Itawasaidia wafanyabiashara kupata faida na kuepuka hasara ya ice cream kuharibika kwa kukosa barafu.
Dar es Salaam. Kama wewe ni muuzaji wa “ice cream” barabarani kwa kutumia baiskeli ya magurudumu matatu au deli, basi teknolojia imekukumbuka kwa sababu hutaweza tena kutumia barafu kugandisha vinywaji huwapo njiani ili zisiyeyuke na kukuletea hasara.
Wabunifu wamebuni baiskeli ya magurudumu matatu yenye jokofu la kutunzia vinywaji baridi na ice cream inayotumia umemejua kuhakikisha zinakuwa katika hali ya barafu wakati wote wa kuuza.
Taasisi ya Elico Foundation kwa kushirikiana na kampuni ya teknolojia ya Juka Solar wameleta teknolojia hiyo nchini Tanzania ikiwa na lengo la kusaidia wafanyabiashara wadogo wadogo hasa wanaouza ice-cream pamoja na vinywaji baridi kupata faida wanayokusudia kutokana na bidhaa zao.
Teknolojia hiyo inatatua changamoto ya baiskeli zinazotumia deli kwa ajili ya kupoza ice cream ambayo uhifadhi wake wa baridi umekuwa haudumu kwa muda mrefu.
Mtaalamu Nishati Endelevu kutoka taasisi hiyo, Fredrick Mushi amesema teknolojia hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa wafanyabiashara kwa sababu ya mfumo wake wa uendeshaji unatumia umemejua ambao ni endelevu na haihitaji gharama kubwa.
“Itasaidia sana wafanyabishara wadogo na wengine wanaokusudia kuanza biashara kwa sababu itawapa uwezo mkubwa wa kuendesha biashara kwa kutumia teknolojia ya kisasa,” amesema Mushi.
Teknolojia hiyo ambayo kwa lugha ya kitaalamu inajulikana kama “Cooling Tricycle” imetengenezwa kwa mfumo wa baiskeli ambayo wakati huo huo imeunganishwa na jokofu (freezer) linalotumia umemejua kupoza vitu vilivyopo ndani ya jokofu hilo.
Wakati wabunifu wakifanya kila liwezekanalo kuwafikishia Watanzania teknolojia hiyo, baada ya wafanyabiashara wanaotembeza ice cream barabarani, wameiambia www.nukta.co.tz kuwa ujio wa teknolojia hiyo utawasaidia na kuwapunguzia changamoto ya ice cream zao kuyeyuka kabla hawajauza, jambo linalowaletea hasara wakati mwingine.
Teknolojia hiyo, imeipiku teknolojia iliyokuwepo awali ya baiskeli ya miguu mitatu inayotumia deli kwa ajili ya kupoza bidhaa. Picha | Elico Foundation.
Mashauri Razack, mmoja wa wauza ice-cream katika eneo la Victoria jijini Dar es Salaam amesema teknolojia hiyo itakuwa yenye manufaa makubwa kwani changamoto ya bidhaa zao kuharibika imekuwa inasumbua sana.
“Aisee! hiyo teknolojia itasaidia sana, Mimi nimeshagawa ice-cream sana (baada ya barafu kuyeyuka) hiyo ni hasara kwangu. Ikija hiyo teknolojia itakuwa rahisi sana,”amesema Razack.
- Toolboksi: Teknolojia inayowaunganisha vijana na fursa za ufundi stadi Tanzania
- Teknolojia inavyotumika kuokoa mazingira
- Huyu ndiye muuza biriani kidijitali Dar
Kwa sasa, baiskeli hizo zimeanza kupatikana nchini katika maeneo na taasisi mbalimbali zinazohusika na vifaa vya umemejua.
Matarajio ya Elico Foundation ni kuifanya teknolojia hiyo ya majokofu kuwafikia Watanzania wengi. Lakini kuingia ubia na makampuni makubwa ya vinywaji ya Tanzania kama ya Azam, Coca-Cola, Pepsi ili kuangalia namna ya kuendeleza teknolojia hiyo.
Latest
