Kombe la Dunia: Qatar ilivyojipanga kudhibiti Uviko-19

October 1, 2022 5:49 am · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Tahadhari zote kuzingatiwa ikiwemo wachezaji, mashabiki kuvaa barakoa.
  • Wachezaji na viongozi wao kupimwa kila baada ya siku mbili.

Dar es Salaam. Muda unazidi kusogea kwa mataifa kukutana Qatar kwa ajili ya mashindano ya kombe la dunia. 

Mashindano hayo yanaweza kuwa miongoni mwa matukio makubwa ya kumalizia mwaka 2022 baada ya kifo cha Malkia Elizabeth II.

Ni hatua gani zinachukuliwa kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa hasa kulinda afya za watu dhidi ya Uviko-19?

Juhudi za kuhakikisha usalama wa afya za wachezaji, viongozi, mashabiki na wakazi wa Qatar ambapo mashindano ya Kombe la Dunia yatafanyika mwaka huu, unazidi kuimarishwa ili kuhakikisha yanafanyika kwa ufanisi.

Wizara ya Afya ya Umma ya Qatar na WHO zinashirikiana kutekeleza hatua za usalama za afya ya umma kwa kipindi hiki ambapo mashindano hayo yanapokaribia.

“Sasa mpango wetu ni kuendeleza mbinu na mapendekezo bora kutoka kwa FIFA Arab Cup  mwishoni mwa 2021, na kuimarisha utayari wa dharura wa kiafya.

“Tunahakikisha tahadhari za kudhibiti magonjwa ya kuambukiza, pamoja na Uviko-19 ili kuwaweka watu salama na wenye afya,” amesema Dk Rayana Ahmad Bou Haka, Mwakilishi wa WHO nchini Qatar.

Takriban mashabiki milioni 1.5 wanatarajiwa kwenda Qatar kuhudhuria kombe la dunia linasimamiwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kati ya Novemba, 20 hadi Desemba,18, 2022 kushuhudia mchuano mkali wa timu za mataifa 32.

Moja ya uwanja wa mpira utakaotumika kwa mashindano ya Kombe la Dunia mwezi ujao nchini Qatar. Picha| InsideTheGames.

Jinsi Uviko-19 utakavyodhibitiwa

Kwa mujibu wa mamlaka za afya za Qatar, mashabiki watakaohudhuria mashindano hayo hawatawekwa karantini ila ni lazima waonyeshe uthibitisho kuwa hawana Uviko-19, japokuwa chanjo hazitakuwa za lazima.

Wageni wenye umri zaidi ya miaka sita lazima wawasilishe matokeo hasi ya kipimo cha Uviko-19 (Polymerase Chain Reaction (PCR)) kitakachopimwa ndani ya saa 48 kabla ya kuondoka nchini zao.

Pia watawasilisha majibu hasi ya kipimo cha Rapid Antigen (RAT) kitakachochukuliwa ndani ya saa 24 kabla ya kuwasili Qatar.

Kila mtu aliye na umri wa miaka 18 na zaidi pia ataombwa kupakua programu ya ufuatiliaji kupitia simu inayoitwa EHTERAZ itakayotumika kuthibitisha hali ya Uviko-19. 

Matumizi ya barakoa yanapendekezwa kuwa lazima katika viwanja vinane ambapo mechi zitaandaliwa, kama ilivyo lazima kwenye usafiri wa umma nchini humo.

Pia yeyote ambaye atapatikana na Uviko-19 akiwa Qatar atalazimika kujitenga kwa mujibu wa miongozo ya Wizara ya Afya ya Umma.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Qatar, nchi hiyo imerekodi zaidi ya kesi 440,000 zilizothibitishwa za Uviko-19 na vifo 682 huku asilimia 97 ya watu wake wamechanjwa chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

FIFA ilisema wachezaji wote kutoka timu 32 za Kombe la Dunia watalazimika kufanya vipimo haraka vya Uviko-19 kila baada ya siku mbili wakaiwa nchini Qatar.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW