Kiswahili chapendekezwa kuwa lugha rasmi ya SADC
- Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) lapendekeza Kiswahili kuwa lugha ya nne ya mawasiliano.
- Itaungana na lugha za Kifaransa, Kiingereza na Kireno zinazotumika katika jumuiya hiyo.
- Uamuzi wa kutumia lugha hiyo unasubiri kupitishwa na wakuu wa nchi wa jumuiyo mwishoni mwa wiki hii.
Dar es Salaam. Lugha ya Kiswahili imependekezwa na Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuwa lugha ya nne itakayotumiwa katika shughuli za mawasiliano katika jumuiya hiyo.
Iwapo kitapitishwa mwishoni mwa wiki hii na Wakuu wa nchi za SADC, Kiswahili kitaungana na lugha za Kifaransa, Kiengereza na Kireno zinazotumika katika shughuli rasmi za jumuiya hiyo.
Mwenyekiti wa baraza Mawaziri wa SADC, Prof Palamagamba Kabudi amesema mapendekezo hayo yatafikishwa kwenye mkutano wa wakuu wa nchi utakaofanyika Agosti 17 na 18, 2019 jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maamuzi.
Prof Kabudi amesema mapendekezo hayo ni heshima kubwa kwa Tanzania kwa sababu kimekuwa kikitumika katika shughuli za ukombozi wa bara la Afrika.
“Kwetu ni heshima kubwa kwamba Kiswahili ambayo ni lugha ya ukombozi, kama itakubaliwa na wakuu wa nchi za SADC kama lugha ya nne rasmi,” amesema Kabudi.
Soma zaidi:
- Kiswahili ndiyo mpango mzima wa kusaka wateja Tanzania: Ripoti
- Wageni kufunzwa Kiswahili katika Chuo cha Diplomasia
Hiyo itakuwa hatua kubwa ya kuongeza wigo wa Kiswahili duniani ikizingatiwa kuwa kinatumiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki kama lugha rasmi ya mawasiliano.
Mbali na hatua hiyo, iwapo kitaridhiwa, lugha hiyo sasa itatoa fursa nyingi za ajira kwa Watanzania kwenda kufundisha katika nchi wanachama wa jumuiya miaka ijayo.
Tayari Afrika Kusini imeingia makubaliano na Serikali kupeleka walimu katika taifa hilo kubwa Afrika.