Kipandauso: Ugonjwa unaowatesa Watanzania kimya kimya
- Ni ugonjwa wa maumivu ya kichwa yanayosababishwa na mwanga, sauti za ghafla na uchovu
- Wahanga wa ugonjwa huo hupoteza marafiki, ndugu na kuingia gharama kubwa za kiuchumi kujitibu.
- Wataalam wa afya washauri Serikali kuwekeza katika matibabu ili kuokoa wahanga wengi wa ugonjwa huo.
Dar es Salaam. “Katika ukuaji wangu, sikuwahi kusikia juu ya neno kipandauso au kama wataalamu waiitavyo migraine, ninajua kichwa kuuma inahitaji kuonana na daktari ambaye mara nyingi atakupima malaria na kukupa dawa unywe na siku moja, mbili unakuwa sawa,” ni maneno ya Witness Sosoma, mkazi wa Jijini Dodoma.
Yapo magonjwa mengi ambayo yanaongelewa mara nyingi na wataalamu wa afya lakini ni mara chache kusikia kuhusu ugonjwa wa kipandauso ambao ni miongoni mwa magonjwa yanayowatesa pia watu.
Kipandauso kimekuwa kikichukuliwa kama “maumivu ya kichwa yaliyochangamka” huku ukweli wa kuwa ugonjwa huo unasababisha wahanga wake kushindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu.
Balozi Togolani Mavura, msaidizi binafsi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema tunaishi katika jamii ambayo kuumwa kichwa ni kitu cha kawada huku wanaopata maumivu makali ya kichwa wanachukuliwa kama watoa visingizio wanaoshindwa kukamilisha majukumu yao kwa wakati na watu wa kudeka.
“Wasichokijua wengi ni kuwa ugonjwa wa kipandauso siyo maumivu ya kichwa yaliyochangamka bali ni ugonjwa ambao baadhi ya watu huwapeleka hospitalini kulazwa kwa wiki, wiki mbili na wengine zaidi ya mwezi.” amesema Balozi Mavura leo Juni 25, 2021 katika uzinduzi wa kitabu cha “The Wave” kilichaondikwa na mbunifu wa mavazi na mwandishi wa vitabu, Rahma Bajun.
Kitabu hicho kinaelezea kwa undani Rahma anavyokabiliana na ugonjwa huo na hamasa iliyopo kwa wadau kuupa kipaumbele ili kuokoa maisha ya Watanzania ambao wanapata maradhi hayo.
Mbunifu wa mavazi na Mwandishi wa kitabu cha “The Wave” Rahma Bajun wakati akizindua kitabu chake. Picha| Jalilu ZaidKipandauso ni nini?
Kipandauso ni maumivu ya kichwani yanasababishwa (triggered) na mambo mbalimbali ikiwemo mwanga, sauti za ghafla na uchovu na kumsababishia mtu athari za kiafya mwilini.
Mtaalam wa afya kutoka kituo cha afya cha TMH kilichopo Mwenge jijini Dar es Salaam, Dk Isaac Maro amesema asilimia 90 ya wagonjwa wa kipandauso hushindwa kutimiza majukumu yao baada ya kulazimika “kujifungia gizani kwa hadi wiki nzima” ili kurejea katika hali ya kawaida.
Dk Maro amesema kipandauso huwa katika mifumo mingi na siyo maumivu ya kichwa upande wa mbele peke yake.
Amesema hali hiyo huambatana na upofu wa muda na wa kudumu, maumivu ya macho na kichwa na kujihisi kutapika ama kukosa hamu ya chakula.
Changamoto zinazoambatana na kipandauso
Kwa ajili ya kuelewa zaidi ugonjwa huu, Dk Maro amesema unaweza kumpata mtu yeyote katika umri wowote na ni katika hatua hiyo ambayo mtindo maisha wa mhanga wake hubadilika kabisa.
Amesema wapo ambao ugonjwa huo umewasababishia kupata hadi kiharusi na magonjwa mengine na ndiyo maana “unatakiwa kuzungumziwa kwa uwazi kama magonjwa mengine ili watu waelewe uzito wake”.
Ugonjwa wa kipandauso umeendelea kuwatesa wahanga wake kwa kukwamisha shughuli zao za kuingiza kipato na kutimiza ndoto zao.
Rahm Baijun aliyezindua kitabu chake cha “The Wave” kinachoelezea safari yake ya maisha kama mhanga wa kipandauso amesema ugonjwa huo umeathiri kwa namna kubwa hali yake ya kiuchumi kwani zipo siku ambazo anashindwa kwenda kazini.
“Niliwahi kupata barua ya onyo kutoka kwa bosi wangu kwa sababu ya kipandauso,” amesema Baijun.
Baadhi ya washiriki waliohudhuria uzinduzi wa kitabu cha Rahma Bajun ambacho kinaelezea kwa undani ugonjwa wa kipandauso na athari kwa jamii. Picha| Jalilu Zaid
Kupoteza marafiki
Ugonjwa huo ambao humfanya mtu kujitenga, hujikuta akipoteza mahusiano ya kindugu na marafiki wa karibu ili kupata ahueni ya kupona haraka.
“Kipandauso kitafukuzia marafiki zako baada ya kuona kuwa hauchangii katika kukuza mahusiano hayo lakini kitakupatia marafiki wengine ambao mara nyingi ni wagonjwa wenzio ambao mtakua mnaongelea hali ya ugonjwa,” ameeleza Bajun.
Kujengeka kwa picha mbaya katika jamii
Ugonjwa wa kipandauso huwalazimisha wengine kujitenga na kelele na hivyo kushindwa kushiriki katika masuala ya kijamii kwa sababu wagonjwa wa kipandauso huitaji utulivu.
Hali hiyo huwaweka katika wakati mgumu wagonjwa kwa sababu baadhi ya watu huwahukumu bila kujua wanachopita.
Mbunge wa jimbo la Ileje mkoani Songwe, Janeth Mbene amesema amewahi kupata changamoto ya kipandauso na mara nyingi huwa kinamtokea pale anapokuwa na mawazo ya safari na vikao au mikutano.
Mbene amesema wakati akiwa binti mdogo hakuchangamana na watu na hivyo wengi walisema anaringa.
“Nikisikia muziki kwa muda mrefu, hapo hapo naumwa. Kijamii walianza kusema naringa, najifanya mzuri,” amesema Mbene ambaye kipandauso kilimpata akiwa na miaka 13, darasa la sita.
Changamoto zingine ni pamoja na wanafunzi kukosa masomo baada ya kulazimika kubaki nyumbani wakijiuguza na wengine wakilazimika kuwakosesha amani wanafamilia wenzao kwa kuwalazimu kufanya vitu kwa kujifikiria kila mara.
“Kutokana na kipandauso, imebidi nyumbani wajifunze kuishi na mimi. Watoto wangu kila muda wanajiuliza mara mbili wanapotaka kufunga mlango, wanapotaka kuwasha taa, wanapotaka kifanya chochote lazima wafikirie kuwa mama ana kipandauso,” amesema Rahma.
Mtaalam wa afya kutoka kituo cha afya cha TMH kilichopo Mwenge jijini Dar es Salaam, Dk Isaac Maro ameshauri watu wenye dalili za kipandauso kuonana na wataalamu wa afya mapema. Picha| Jalilu Zaid.
Ni nini cha kufanya?
Ili kuhakikisha kuwa wagonjwa wa kipandauso wanapata ahueni kutokana na tatizo hilo, wadau wameshauri Wizara ya Afya kuwekeza katika kutengeneza dawa za kutuliza maumivu ambazo watakuwa wanakaa nazo na kuzitumia pale hali inapowapata katika maeneo yao.
Dk Isaac Maro amesema dawa hizo katika nchi zingine zinauzwa katika maduka ya madawa na kwa Tanzania hazipatikani kirahisi na hivyo wagonjwa kulazimika kuagiza nje ya nchi.
“Wafamasia wetu wafanye kazi ya kutafuta dawa ambazo zitawasaidia watu hawa na ziuzwe dukani ili kila anayejua ana shida hiyo aweze kuwa nazo,” amesema Dk Maro.
Hata hivyo, wagonjwa wanaohisi kupata dalili za ugonjwa huo wametakiwa kufika hospitalini ili kupata ushauri wa daktari na tiba itakayowawezesha kurejea katika hali ya kawaida.
Latest
