Kilio, kicheko: Viwango vipya vya ushuru wa forodha vifaa vya ujenzi

June 18, 2020 1:00 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Wadua wa ujenzi wamesema zitapunguza ushindani huku zikiongeza masoko kwa bidhaa zinazotengenzwa nchini.
  • Wengine wamesema watakaoumia ni wale wanaopenda vifaa vya nje. 

Dar es Salaam. Siku chache baada ya kupitishwa kwa viwango vipya vya ushuru wa forodha katika baadhi ya vifaa vya ujenzi zikiwemo nondo, wauzaji na watumiaji wa vifaa hivyo wametoa maoni mchanganyiko huku baadhi yao wakisema itasaidia kuimarisha viwanda ndani. 

Viwango hivyo vya ushuru wa forodha vitatozwa kwenye nondo, mabati na marumaru zinazoagizwa kutoka nje ya nchi vitatumika katika mwaka wa fedha wa 2020/21. 

Ushuru wa forodha umeongezwa kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za marumaru huku Serikali ikitoza Dola za Marekani 250 (Sh578,700) badala ya Dola za Marekani 200 (Sh462,997) kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye nondo. 

Pia Dk Mpango alisema Serikali iendelee kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 10 au Dola za Marekani 250 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za mabati badala ya ushuru wa asilimia 10 pekee. 

Mabadiliko hayo ya ushuru wa forodha yataanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2020/21 ambao unaanza Julai mosi mwaka huu. 

Mabati ya nchi zingine huingizwa kwa gharama nafuu na hivyo kuuzwa kwa bei ambayo ni tishio kwa mabati yanayozalishwa nchini. Picha| IPP Media.

Hiyo inamaanisha nini?

Afisa Masoko kutoka kampuni ya Mabati Quality ya jijini Dar es Salaam ambao wanatengeneza mabati ya kuezekea nyumba, Godfrey Paul amesema kuwepo kwa kodi hizo itakuwa ni jambo la neema kwa wazalishaji wa ndani kwa sababu litapunguza ushindani sokoni.

Paul ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa kumekuwepo na ushindani mkubwa sokoni na mara nyingi mabati yanayozalishwa nchini yanapigwa kikumbo na mabati yanayoagizwa kutoka mataifa mengine ikiwemo China.

Mdau huyo wa masoko amesema mabati ya nchi zingine huingizwa kwa gharama nafuu na hivyo kuuzwa kwa bei ambayo ni tishio kwa mabati yanayozalishwa nchini.

“Mabati ya nje yamekuwa tabu. Nimeongea hivi karibuni na mtu wa hard ware (duka la vifaa vya ujenzi) akasema wameingiza bati nyingi tu kutoka China na kwa bei ya chini,” amesema Paul.

Paul amesema huenda maamuzi yaliyochukuliwa ya kuongeza kodi kwa bidhaa zinazoingia, yatawasaidia kupata muda wa kupumua.

Mdau huyo amesema mara nyingi watu wanakosa imani na bidhaa za Tanzania kwa sababu hawaangalii uthabiti garantii ya bidhaa wanazonunua.

“Zipo bidhaa zinazotoa garantii ya miaka mitano. Hata sisi tunatoa miaka mitano na ni rahisi ukinunua bidhaa za Tanzania kwani hata zikiharibika, una garantii yako unaweza kwenda kiwandani kurudisha. Ukinunua ya nchi zingine utazirudisha?” amehoji Paul.


Zinazohusiana


Amesema mabadiliko hayo ya ushuru siyo tu yatavifaidisha viwanda vya ndani lakini hata wanunuzi kuwa na uhakika na bidhaa wanazonunua. 

Vifaa hivyo vimekuwa vikitumiwa na wananchi katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa majengo ya nyumba za kuishi na biashara. 

Naye Fundi wa marumaru za majumbani Salum Njaji ameiambia Nukta kuwa ongezeko la kodi hiyo huenda ikawapatia ugumu mafundi kwa sababu bidhaa hizo zinazotoka nje zina ubora wa juu na zinapendelewa na watu wengi. 

“Mimi ni mdau wa tiles (marumaru), tiles zinazotengenezwa nchini zinakuwa na changamoto. Mara nyingi zinakosa ulingano na hivyo kulazimu kutumia muda mwingi kuzilinganisha na unaweza kujikuta unazipasua kwani zinapasuka kwa urahisi.” amesema Njaji.

Viwango vipya vya ushuru wa forodha vimetokana na mabadiliko yaliyofanywa katika Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kwa mwaka wa fedha 2020/21. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW