Kigogo mwingine ateuliwa kuiongoza Vodacom Tanzania

September 6, 2018 7:39 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  • Uteuzi huo unakuja wakati kitendawili cha upatikanaji wa kibali cha kufanya kazi nchini cha Sylivia Mulinge aliyetakiwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji kuanzia Juni mosi kikiwa hakijatatuliwa.
  • Ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara, Hisham Hendi mwenye uzoefu wa miaka 15 katika sekta ya mawasiliano duniani na atakaimu nafasi ya Ian Ferrao aliyemaliza muda wake.  
  • Hendi ana kazi kubwa ya kuifanya Vodacom Tanzania kuendelea kutoa ushindani kwa kampuni zingine za mawasiliano nchini.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania, Hashim Hendi akizungumza katika moja ya mikutano pindi alipokuwa Mkurugenzi Kitengo cha Biashara. Picha| Michuzi Blog.

Dar es Salaam. Kampuni ya Vodacom Tanzania imemteua Hisham Hendi kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo kuanzia Septemba 1, 2018 mpaka mchakato wa kumpata Mkurugenzi mpya utakapokamilika.

Hendi amekuwa na kampuni ya Vodacom Tanzania tangu mwaka 2016 kama Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara ambapo ana uzoefu wa miaka 15 katika sekta ya mawasiliano na amewahi kushika nafasi mbalimbali katika kampuni ya Vodafone na kampuni mama ya Vodacom Group companies.

Uteuzi huo wa Hendi unakuja ikiwa imepita miezi minne tangu kigogo wa kampuni ya Safaricom, Sylvia Mulinge, raia wa Kenya ambaye alitakiwa kuchukua mikoba ya Mkurugenzi Mtendaji wa wakati huo, Ian Ferrao kukosa kibali cha kufanya kazi nchini.

Huenda Hendi atakakabiliwa na kibarua kigumu cha kuendeleza majukumu ya Vodacom Tanzania pale ilipoishia Ferrao aliyefanya kazi kwa miaka mitatu kutoka 2015 hadi Aprili 2018.


Zinazohusiana:  Kigogo wa Safaricom kuiongoza Vodacom Tanzania


Ferrao ambaye  aliondoka akiwa ameifanya Vodacom Tanzania, kuwa kampuni ya kwanza nchini kujiorodhesha katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) mwaka 2017 na kufanya vizuri katika ugawaji wa gawio la 28.5 bilioni.

 Kwa mujibu wa ripoti ya mawasiliano ya robo ya pili ya mwaka 2018 (Aprili-Juni), hadi kufika Juni mwaka mwaka, Vodacom Tanzania ilikuwa inaongoza kwa kuwa na watumiaji wengi wa simu za mkononi wanaofikia 13.3 milioni sawa na asilimia 32 ya mitandao yote ya simu nchini.

Uteuzi wa Hendi unaweza kuwa chachu kwa wafanyakazi, wakati wakisubiri kupata kigogo atakayeshikilia usukani wa kamapuni hiyo ya mawasiliano nchini.

Enable Notifications OK No thanks