Kigamboni, Temeke kutumia mfumo wa kielektroniki utoaji hatimiliki ardhi kuanzia Julai 1
Hatua hizo zimesaidia kuondoa malalamiko yaliyokuwepo awali ya ucheleweshaji na upatikanaji wa hati miliki za ardhi. Picha|Mtandao.
- Mfumo huo utasaidia kuharakisha na kupunguza gharama za utoaji huduma za ardhi ikiwemo utoaji wa hatimiliki za ardhi.
- Manispaa za Ubungo na Kinondoni tayari zinatumia mfumo huo.
- Serikali inaendelea na taratibu za kusimika mfumo huo katika halmashauri zote nchini kwa awamu.
Dar es Salaam. Huenda wananchi wa Manispaa za Kigamboni, Ilala na Temeke Jijini Dar es Salaam wakaondokana na usumbufu wa kupata hatimiliki za ardhi kwa wakati, baada ya Serikali kutangaza kua itaanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa kutoa hati hizo katika wilaya hizo ifikapo Julai mwaka huu.
Mfumo huo unganishi wa kutunza kumbukumbu za ardhi (Integrated land management information system) kwa sasa, unatumika katika Manispaa za Kinondoni na Ubungo.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula aliyekuwa akizungumza Bungeni leo (Juni 21, 2019) amesema mfumo huo umejengwa na wizara yake kwa ajili kuharakisha na kupunguza gharama za utoaji huduma za ardhi ikiwemo utoaji wa hati miliki za ardhi.
“Kwa sasa tayari mfumo huo umeanza kutoa hatimiliki za ardhi katika Manispaa za Kinondoni na Ubungo. Aidha, Serikali imekamilisha ufungaji wa mfumo huo katika Manispaa za Ilala, Kigamboni na Temeke na utaanza kutumika Julai 1, 2019,” amesema Mabula.
Soma zaidi:
- Mgogoro wa ardhi unavyosababisha wanafunzi 200 wabanane darasa moja Mbeya
- Kigoma kinara usajili mashamba Tanzania bara
- Nusu ya Watanzania hawana nyaraka muhimu za kumuliki ardhi
Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea na taratibu za kusimika mfumo huo katika halmashauri zote nchini kwa awamu.
Naibu Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Ilemela alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Lyimo aliyetaka kujua Serikali inasema nini kuhusu ucheleweshaji wa utoaji wa hatimiliki za ardhi.
Licha ya kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki, Mabula amesema tangu mwaka 2008, wizara yake imefanikiwa kuanzisha kanda nane za ardhi nchi nzima kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali ikiwemo utoaji wa hatimiliki za ardhi.
Hatua hizo zimesaidia kuondoa malalamiko yaliyokuwepo awali ya ucheleweshaji na upatikanaji wa hati miliki za ardhi.
“Sababu kubwa iliyosababisha kuwepo kwa changamoto hiyo ni kuwepo kwa Kaminshna mmoja nchi nzima aliyeruhusiwa kutia saini hati kwa nchi nzima,” amesema Mabula.