Kicheko kwa wakulima, TMA akitoa mwelekeo mvua za msimu

October 18, 2019 3:27 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wakulima wametakiwa kujiandaa kuongeza uzalishaji na kupanua soko la mazao watakayolima.
  • Yasema hali ya unyevunyevu wa udongo kwa ustawi wa mazao vinatarajiwa kuimarika katika maeneo mengi.
  • Uharibifu na magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza hususan katika maeneo yenye miundombinu hafifu ya maji taka.

Dar es Salaam. Wakulima wa mikoa inayopata mvua mara moja kwa mwaka ikiwemo Mbeya na Iringa wametakiwa kujiandaa kuongeza uzalishaji na kupanua soko la mazao watakayolima, kutokana na ujio wa mvua nyingi za msimu. 

Mikoa inayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka  ni pamoja na mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa na Ruvuma. 

Pia maeneo ya Kusini mwa mkoa wa Morogoro, Lindi na Mtwara na maeneo yaliyosalia ya Mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa. 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agnes Kijazi aliyekuwa akitoa mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (Novemba, 2019 – Aprili, 2020) jana amesema hali ya unyevunyevu wa udongo kwa ustawi wa mazao vinatarajiwa kuimarika katika maeneo mengi.

Kutokana na mvua zinazotegemewa kunyesha katika maeneo hayo, Dk Kijazi amewashauri wakulima kujiandaa ili kuzalisha mazao hasa yanayokomaa muda mrefu yatakayoongeza tija katika familia na Taifa.

“Maghala ya hifadhi za chakula yaimarishwe katika ngazi mbalimbali ili kuwa na nafasi ya kutosha kuhifadhi ziada ya chakula kitakachozalishwa. Kuandaa na kusambaza viwatilifu vya kutosha kwa wakati ili kukabiliana na ongezeko la wadudu waharibifu mashambani na kwenye maghala ya hifadhi za chakula,” amesema Dk Kijazi. 


Soma zaidi: 


Mtawanyiko wa mvua

Mvua za Msimu ni mahususi katika maeneo ya magharibi mwa nchi, kanda ya kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro.

Katika mkoa wa Tabora mvua inatarajia kunyesha juu ya wastani hadi wastani huku mkoa wa Kigoma na Katavi inatarajia kunyesha mvua za wastani hadi juu ya wastani. 

Mvua katika maeneo hayo zitaanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba 2019 katika mkoa wa Kigoma na kusambaa Kwa mikoa ya Katavi na Tabora katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba.

“Mvua katika maeneo ya Singida na Dodoma zinatarajia kuanza katika wiki ya Kwanza hadi wiki ya pili ya mwezi Novemba 2019 na maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani hadi wastani,” amesema Dk Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO). 

Katika mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro mvua zinatarajia kuanza kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba 2019 na kutarajia kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi.

Aidha, amesema katika mikoa ya Lindi na Mtwara mvua zinatarajia kunyesha kati ya wiki ya kwanza na wiki ya pili ya mwezi Novemba 2019 na zinatarajia kuwa za juu ya wastani hadi wastani.

MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU (NOVEMBA, 2019 – APRILI, 2020)

                               

Matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani.

Ujio wa mvua hizo za msimu ni matokeo ya migandamizo midogo ya hewa pamoja na vimbunga katika eneo la kusini magharibi mwa bahari ya Hindi ambayo inatarajiwa kuvuta upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo na hivyo kusababisha mvua katika maeneo mengi hapa nchini. 

Katika eneo la mashariki mwa bahari ya Atlantiki, joto la bahari linatarajiwa kuwa la juu ya wastani na hivyo kuwa na mchango mdogo kwa mifumo na mwenendo wa mvua katika maeneo ya magharibi mwa nchi. 

Ushauri na tahadhari 

Dk Kijazi amesema magonjwa ya wanyama na uharibifu wa miundombinu ya kilimo vinaweza kujitokeza kutokana na mvua zinazotarajiwa. 

“Kwa upande mwingine, malisho na upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo na wanyama pori vinatarajiwa kuwa vya kuridhisha katika maeneo mengi,” amesema na kushauri kuwa teknolojia ya uvunaji maji ya mvua iimarishwe ili kuhifadhi maji  kwa matumizi katika kipindi cha baadaye. 

Wadau katika sekta ya uvuvi wanashauriwa kuandaa miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya Uvuvi  yakiwemo  maghala ya baridi kwa sababu kutakuwa  na maji ya kutosha na ziada katika maziwa, mito na mabwawa na hali hiyo inatarajiwa kuchangia kuongezeka  kwa chakula cha samaki.

Katika hatua nyingine, Dk Kijazi amesema mvua za msimu zinazotarajiwa zinaweza kusabibisha magonjwa ya mlipuko yanayohusiana na maji . Hivyo sekta husika zinashauriwa kuchukua hatua stahiki ikiwa pamoja na kutibu maji ya kunywa, kuzuia na kuharibu mazalia ya mbu na kudumisha usafi wa mazingira. 

TMA inawashauri watumiaji wote wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, mamlaka za wanyamapori, sekta za maji na afya kuendelea kufuatilia na kutumia ushauri wa kitaalam katika shughuli zao za kila siku.

Enable Notifications OK No thanks