Kenya yarudisha mzigo wa dhahabu, mamilioni ya fedha yaliyoibwa Tanzania miaka 15 iliyopita
- Dhahabu hiyo ni kilo 35.34 iliyotoroshwa kupitia uwanja wa ndege wa KIA kabla ya kumatwa Nairobi Kenya Februari 15, 2018.
- Fedha hizo zinajumuisha Sh170 milioni zilizoibwa katika benki ya NBS tawi la Moshi, Kilimanjaro mwaka 2004.
- Rais Magufuli avipongeza vyombo vya ulinzi vya Kenya kwa kazi viliyofanya.
- Wahalifu wengine waambiwa wakae chonjo.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli leo amepokea kilo 35.34 ya dhahabu na fedha zilizokamatwa baada ya kutoroshwa na wahalifu kutoka Tanzania.
Zoezi la makabidhiano ya dhahabu na kiasi cha fedha kilichokamatwa yamefanyika leo (Julai 24, 2019) baina ya maafisa wa Serikali ya Kenya na Tanzania na kushuhudiwa na Rais Magufuli aliyevisifu vyombo vya dola vya nchi hiyo jirani kwa kazi nzuri waliyoifanya.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga amesema mtuhumiwa Baraka Chaulo aliyekuwa akisafirishwa dhahabu hiyo alikamatwa Februari 15, 2018 katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyata wakati akiajiandaa kuipeleka Dubai.
Amesema dhahabu hiyo ilitoka uwanja wa ndege wa Mwanz kisha ikapelekwa hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA) na baadaye ilisafirishwa hadi Nairobi Kenya ambako ilikamatwa.
Mbali na mzigo wa dhahabu hiyo, Biswalo amesema Serikali ya Kenya imerejesha fedha ambazo ziliibwa Tanzania mwaka Mei 21, 2004 katika benki ya NBC tawi la NBC.
“Mshtakiwa aliyekamatwa na hizo fedha amerejeshwa Tanzania na kesi ipo Moshi tunasubiri ushahidi wa vielelezo alivyokamatwa navyo ambavyo ni Sh 170 milioni, Dola za Kimarekani 77,500 (Sh178.2 milioni) na Ksh171.6 milioni…vyote naamini wameturudishia ili kesi iendelee,” amesema Mganga.
Soma zaidi:
- Uzalishaji wa dhahabu Acacia washuka
- Rais Kenyatta kuzuru Chato kwa mwaliko wa Magufuli
- Tanzania, Kenya zinavyochuana ujenzi wa bandari kavu
Amesema kurejeshwa kwa dhahabu hiyo kunatokana na mazungumzo kati ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais Magufuli yaliyofanyika katika Wilaya ya Chato mkoani Geita Julai 5 mwaka huu.
“Siku ya leo si kwamba tunashuhudia urudishwaji wa dhahabu tu bali pia urudishwaji wa fedha zetu zilizokamatwa Kenya baada ya kuibiwa Tanzania mwaka 2004 ambapo Benki yetu ya NBC tawi la Moshi ilivamiwa na watu wakaiba Sh170 milioni,” amesema Mganga.
Akizungumza mara baada ya kupokea dhahabu na fedha hizo, Rais Magufuli amevipongeza vyombo vya ulinzi vya Kenya kwa kazi kubwa viliyofanya ya kuhakikisha mali hiyo haisafirishwi hadi Dubai.
Pia amemshukuru Rais Kenyatta kwa moyo wa uzalendo na uaminifu wake wa kukubali kurejesha dhahabu na fedha hizo, licha ya kuwa alikuwa na uwezo kuzitumia atakavyo.
“Wa kupongezwa hapa kwenye hii mali ni vyombo vya ulinzi vya Kenya, najua wakuu wa vyombo vya ulinzi mko hapa lazima niwatandike hapa mbele ya watu kwa sababu imetoka Mwanza, Tanzania ikaenda KIA ilipofika Kenya vile vyombo kabla ya ile mali haijasafirishwa kwenda Dubai ikashikwa,” amesema Rais Magufuli.
Maafisa wa Kenya wakiwa wamebeba dhahabu na fedha zilizokamatwa nchini mwao wakiwasili Tanzania. Picha|Mtandao.
Kutokana na weledi wa vyombo vya ulinzi vya Kenya, Rais amewataka wakuu wa vyombo vya ulinzi nchini wajitafakari ni kwanini wahalifu hao walifanikiwa kupita vizuizi vyote vilivyopo nchini mpaka Kenya. Hata hivyo, amevitaka vyombo hivyo kuongeza ufanisi wa kazi katika kushughulikia uhalifu ikiwemo kuimarisha ushirikiano ili kuhakikisha Watanzania hawaendelei kuibiwa tena rasilimali zao.
Tanzania ni miongoni mwa nchi chache za Afrika zenye uzalishaji mkubwa wa dhahabu lakini wananchi wake wamekuwa hawafaidiki na rasirimali hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo usimamizi mbovu na ukosefu wa uwazi katika shughuli za uchimbaji madini.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Monica Juma ambaye alimwakilisha Rais Kenyatta katika makabidhiano hayo, amesema zoezi lilifanyika leo ni ishara ya mshikamano kati ya Tanzania na Kenya ambao ukiendelezwa unaweza kusaidia katika kupanua fursa za kibiashara na ukuaji wa uchumi wa nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amewasihi Watanzania kuepuka kujiingiza kwenye uhalifu ambao unaweza kuwagharimu hata wakikimbilia katika nchi za jirani.
“Ndugu zangu Watanzania na wale wote wanaodhani wakifanya uhalifu wanawaweza kukimbilia nchi nyingine, leo wameuona mwisho wao. Ni vema tukawa raia wema ambao hatujiingizi katika uhalifu,” amesema Kabudi.