Kenya, Tanzania kumaliza mgogoro mipakani kwa mazungumzo

May 20, 2020 3:18 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Rais John Magufuli aagiza viongozi wa Tanzania kuzungumza na wenzao wa Kenya ili kumaliza sintofahamu katika mipaka.
  • Amesema nchi hizo zinataka kufanya biashara kwa utulivu. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema wamekubaliana na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kuwa mawaziri wa uchukuzi na wakuu wa mikoa wa mipakani wa nchi hizo wakutane ili kumaliza tatizo la kuzuiwa kwa madereva wa malori kupita katika mipaka ya nchi hizo kulikosababishwa jitihada za kudhibiti janga la Corona. 

Madereva wa malori wa nchi hizo mbili wamekuwa wakitakiwa kupimwa kwanza Corona kabla ya kuendelea na safari zao, jambo ambalo limetatiza shughuli za biashara baina ya pande pili kwa kuchelewesha mizigo na kuzuiwa madereva wanaokutwa na corona.  

Dk Magufuli amesema leo (Mei 20, 2020) mkoani Singida akiwa njiani kutoka Chato wa Mkoa wa Geita kuwa amewasiliana na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kwa simu na wamekubaliana kumaliza mgogoro huo wa mipakani ulioibuka hivi karibuni. 

“Tumekubaliana na Mhe Rais Kenyatta (Rais wa Kenya) kwamba mawaziri wetu wa uchukuzi pamoja wakuu wa mikoa, kwetu sisi Tanzania; Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mara, Arusha, Kilimanjaro na wa Tanga watakutana na wenzao wa Kenya mpakani wajadili hili suala walimalize,” amesema Magufuli. 

Amesema mlipuko wa virusi vya Corona isiwe chanzo cha migogoro na kutokuelewana baina ya nchi hizo mbili na kwamba Kenya na Tanzania wote wanahitaji kufanya biashara.

Amesema raia wa hizo mbili wanatakiwa kuwa watulivu wakati viongozi wakitafuta suluhu ya sintofahamu iliyoibuka wakati wa utekelezaji tahadhari ya kujikinga na Corona.


Soma zaidi: 


Amesema  kitenda cha malori na madereva kuzuiwa katika mipaka ya nchi hizo kwa muda mrefu hakikubaliki kwa sababu bidhaa zinachelewa kufika mahali husika na kuwakosesha wananchi mahitaji muhimu. 

“Nilikuwa naambiwa kuna magari kule yamekwamishwa ya Wakenya. Haiwezekani tukawakwamisha wanakuja kufanya biashara hata magari ya Tanzania hayawezi yakakwamishwa kwenda Kenya,” amesema Dk Magufuli na kuagiza viongozi hao wafanye mkutano huo haraka iwezekanavyo hata wiki hii.

Aidha, amewataka viongozi walioko katika mikoa inayopakana na nchi ya Kenya na Tanzania wasitatue matatizo  kwa jazba bali waweke Utanzania na Ukenya mbele huku wakizingatia kujenga uchumi wa nchi zote mbili. 

Mei 17, Rais Kenyatta alitangaza kufunga mpaka wa Kenyatta na Tanzania kwa siku 30 na kuwa ni malori tu ya mizigo ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia nchini humo baada ya madereva wake kupimwa na kukutwa hawana maambukizi ya Corona.

Hata hivyo, siku chache zilizofuata baadhi ya viongozi wa Tanzania walizuia malori ya Kenya kuingia Tanzania, jambo lililoibua sintofahamu pande zote mbili. 

Leo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amedai madereva wa Tanzania waliokutwa na corona Kenya hivi karibuni wamekutwa hawana ugonjwa huo baada ya kupimwa tena nyumbani.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW