Kasri za kifalme zinavyovutia watalii Ufaransa
- Nchi hiyo ya Ulaya ina kasri nyingi za kifahari zilizojengwa miaka mingi iliyopita.
- Zimekuwa kivutio cha watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Dar es salaam. Kasri ni jumba la kifahari ambapo wafalme na malkia huishi. Katika jumba hilo unaweza kukuta vyumba vingi vikiwa vimenakishiwa kwa mitindo mbalimbali ya rangi na kuta.
Ufaransa ni miongoni mwa nchi barani Ulaya yenye kasri nyingi za kifalme na malkia katika pande zote ya nchi hiyo.
Hili nililithibitisha baada ya kukaa katika nchi hiyo kwa mwezi mmoja wakati nilipoitembelea ili kujifunza utamaduni, sanaa na desturi za nchi hiyo zinavyohusiana na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.
Usanifu na ujenzi wa kasri hizo ni wa kipekee na wakuvutia, na hilo utagundua pale tu utakapotazama kuta za kasri hizo zenye upana na urefu tofauti.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa, mwaka 2019 takribani watu milioni 90 kutoka mataifa mbalimbali walitembelea nchi hiyo ambapo moja ya vivutio walivyotembelea ni kasri hizo zilizojengwa miaka mingi iliyopita.
Zifahamu baadhi ya kasri katika ukanda wa Bourgogne nchini Ufaransa ambazo nilifanikiwa kuzitembelea Julai mwaka huu:
1. Kasri la Clos de Vougeot
Kasri hili lilijengwa katika karne ya 12 na watawa kutoka Abbey Cîteaux nchini Ufaransa ambapo eneo lililokuwa liikikaliwa na kanisa katoliki. Usanifu na ujenzi wa kasri hilo uliendelezwa katika karne ya 16 katika mashamba ya mizabibu ya eneo hilo la Burgundy nchini Ufaransa.
Kasri hili limezungukwa na mashamba ya mizabibu pande zote. Awali mahali hapo lilikuwa shamba la mvinyo lakini kwa sasa kasri la Clos de Vougeot halitengenezi mvinyo bali linasalia kuwa historia ya eneo la Burgundy mashariki mwa Ufaransa na kuvutia watalii mbalimbali kuja kutembelea.
Novemba 2021, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alimualika aliyekuwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa chakula cha pamoja katika moja ya chumba maalumu cha kasri hilo.
Kasri la Clos de Vougeot limekuwa kivutio kikubwa kwa watalii wanaotembelea Ufaransa. Picha| David Mselewa.
2.Kasri la Montbéliard
Kasri hili ambayo ujenzi wake ulianza katika karne ya 13 na kumalizika katika karne ya 19 linapatikana mashariki mwa Ufaransa ambapo ni kilometa 15 tu kufika nchi ya Uswizi.
Kati ya 1769 na 1792 Kasri ya Montbéliard ilikuwa ni makazi ya Princess Friederike wa Brandenburg-Schwedt. Binti huyo wa kifalme ni chimbuko la baadhi ya wafalme na malkia katika bara la Ulaya wa karne ya 19 na 20, kati yao ni Malkia wa Uingereza Elizabeth II na mumewe Prince Philip.
Kasri hilo limejengwa juu ya jiwe kati ya mito miwili. Leo kasri hilo limefanywa kuwa ni jumba la makumbusho lenye mkusanyiko wa mabaki ya wanyama na mijusi iliyogunduliwa na Georges Cuvier, mwanaakiolojia wa Ufaransa.
Muonekano wa nje wa Kasri la Montbéliard ambalo lilitumiwa na wafalme wa nchi ya Ufaransa kwa nyakati tofauti. Licha ya kuwa lilijengwa miaka mingi iliyopita bado lipo mpaka leo. Picha| David Mselewa.
3. Kasri la Bussy – Rabutin
Kasri ya Bussy-Rabutin ilianza karne ya 12 ilijengwa na Renaudin de Bussy. Kasri hilo lilikaliwa na watawala akiwemo Henri II (1547-1559) na Louis XIII (1610-1643).
Katika muendelezo wa ujenzi wa kasri hilo liliongezewa nakshi mbalimbali za sanaa kama vile picha. Hata hivyo, kasri hilo limerekebishwa mara kadhaa na kwa sasa linamilikiwa na Serikali ya Ufaransa na kufanywa kama sehemu ya makumbusho huku bustani nzuri ambayo inapatikana kwenye kasri hilo ikiwavutia watu wengi kuja kuitembelea.
Kwa utunzaji wa kasri mbalimbali nchini Ufaransa, Serikali inaendelea kukusanya mapato kupitia watalii wa mataifa mbalimbali na kuifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi zinazotembelewa na watu wengi duniani.
Kama wewe ni mdau wa masuala ya utalii wa kimataifa, basi mwaka huu unaweza kupanga safari kuitembelea nchi hiyo ya Ulaya ili kujionea kasri hizo zenye muonekano wa kipekee.

Kasri la Bussy – Rabutin limepambwa kwa nakshi mbalimbali za rangi muundo wa ujenzi unaovutia. Picha| David Mselewa.
Latest
