KANUNI 2: Thamani ya mwanga wa jua kwenye ngozi yako
- Huongeza uwezo wa mishipa kubeba oksijeni na kuipeleka kwenye tishu zako tofauti mwilini.
- Husaidia upumuaji na kiwango cha mapigo ya moyo kwenda kama yanavyotakiwa.
- Kiwango cha jua sahihi kwa ngozi yako huongeza uwezo wa misuli na kupunguza mkazo lakini huimarisha uwezo wa kujifunza mambo mapya.
Wiki iliyopita tuliangalia kanuni ya kwanza katika mfululizo wa makala ya kanuni nane za afya ambazo tunashauriwa tuzingatie ili afya zetu ziwe kutuwezesha kutimiza shughuli za maendeleo na kufurahia maisha.
Leo tunaendelea na kanuni ya pili tukiangazia mwanga wa jua na umuhimu wake mwilini.
Kila kiumbe hai duniani hutegemea mwangaza wa jua kwa namna moja au nyingine. Mwaka 1877 watafiti wawili Arthur Downes na Thomas Blunt katika utafiti wao wa madhara ya jua kwa bakteria, waligundua kuwa mwanga wa jua unaweza kuharibu bakteria wabaya na kutibu maambukizi kadhaa ya magonjwa mwilini.
Miale ya jua inapozigusa chembe chembe za mwili ziitwazo “Ergosterols” hubadilishwa na kua vitamini D ambayo husafirishwa na damu kuelekea kila sehemu ya mwili ikisaidia kuimarisha mifupa na meno.
Mwanga wa jua unasaidia pia kushusha kiwango chako cha upumuaji na kukuwezesha kuwa na upumuaji na kasi ya mapigo ya moyo ya kawaida. Mwanga wa jua huongeza uwezo wa mishipa kubeba oksijeni na kuipeleka kwenye tishu zako tofauti mwilini.
Kiwango cha jua sahihi kwa ngozi yako huongeza uwezo wa misuli na kupunguza mkazo lakini huimarisha uwezo wa kujifunza mambo mapya.
Soma zaidi:
- Namna waathirika wa ajali ya Mv Nyerere wanavyoweza kusaidiwa kisaikolojia.
- Jinsi unavyoweza kuishinda sonona isiharibu maisha binafsi, kazi.
Lakini kujianika katika mwanga wa jua mkali, unakuweka katika hatari ya kupata saratani ya ngozi lakini siyo wakati wote kutegemeana na kiwango cha jua kinachoingia mwilini.
Jinsi ya kupata kiwango sahihi cha juu kwenye mwili wako
Kwa afya bora ya ngozi yako, ruhusu mwanga wa jua uingie ndani ya nyumba yako. Fungua madirisha ili mwanga na hewa viingie ndani.
Pia tumia vikinga jua (sunscreens) kwa wenye ngozi laini. Viwango vya jua kupita kiasi husababisha ngozi kukauka na kuwa kavu. Pata mwanga wa jua pale linapokuwa siyo kali.
Kiwango cha jua sahihi kwa ngozi yako huongeza uwezo wa misuli na kupunguza mkazo lakini huimarisha uwezo wa kujifunza mambo mapya. Picha| Helena Lopes on Unsplash.
Kwa hali ya kawaida ukipata dakika tano hadi kumi za kukaa katika mwanga wa jua la asubuhi hadi saa nne unaimarisha ngozi yako na uimara wa mwili wako kwa ujumla.
Baadhi ya watu wana ngozi ambazo ni rahisi kuathiriwa na mwanga wa jua, hasa watu wenye ulemavu wa ngozi, wenye ngozi laini na watu weupe kutokana na kiwango kidogo cha melanini kwenye ngozi zao. Anza kwa kuangalia mazingira uliyopo.
Kama jua ni kali basi hakikisha unaenda kukaa katika eneo ambapo jua siyo kali. Anza kwa kukaa walau dakika mbili.
Kisha unaweza kuongeza hadi dakika nane kulingana na namna unavyoona ngozi yako inavumilia. Usikae juani muda mrefu. Jinyooshe na endelea na majukumu yako ya kila siku.
Iwapo utaona mabadiliko yoyote yasiyo ya kawaida katika ngozi ya mwili wako baada ya kukaa juani, pata ushauri wa kitabibu .
Mwanga wa jua pekee hautoshi lakini zingatia kupata lishe bora hasa matunda na mboga mboga zinaweza kukukinga na matokeo hasi yatokanayo na mwanga wa jua.
Tukutane tena wakati mwingine tukiangazia kanuni ya tatu ya afya.