Jinsi ya kutengeneza, kuhariri picha kwa kutumia Gemini AI
- Gemini ni miongoni mwa akili bandia zinazotumia lugha (Language model) iliyozinduliwa mwaka 2023 na kampuni ya Google.
- Licha ya ufanisi wake inaweza kupotosha au kutengeneza uhalisia usiokuwepo.
Arusha. Katika ulimwengu wa kidijitali, picha zenye ubora zimekuwa miongoni mwa mbinu za kuvutia hadhira na kuwasilisha ujumbe kwa ufanisi hususani katika biashara, mitandao ya kijamii au kazi za ubunifu.
Mara kadhaa nyenzo hiyo hutumiwa kuvutia na kushawishi wateja kununua bidhaa fulani huku makampuni na watu binafsi wakitumia kama njia ya kuongeza ushawishi wao kwa jamii.
Kutokana na umuhimu huo, hivi karibuni kumekuwa na bunifu za teknolojia mbalimbali zinaweza kuunda, na kuhariri picha kwa ubora na viwango mbalimbali ikiwemo akili unde (AI) ya Gemini.
Gemini ni miongoni mwa akili bandia zinazotumia lugha (Language model) iliyozinduliwa mwaka 2023 na kampuni ya Google ikiwa na maelfu ya watumiaji kutoka duniani kote.

Gemini AI hutegemea zaidi maelezo utakayoyatoa ili kutengenza picha, video au infografia.Picha/Gemini AI.
Mbali na kutengeneza picha Gemini AI ina uwezo wa kutoa majibu ya maswali, kufupisha nyaraka ndefu, kuunda maudhui ya ubunifu kama insha, mashairi, kufanya utafsiri wa lugha nyingi, pia kuunganishwa na zana za Google kama Gmail na ramani ili kutoa usaidizi wa kazi mbalimbali za kidijitali.
Pamoja na matumizi mengi ya Gemini, katika makala hii tutaangazia jinsi ya kuitumia kuunda na kuhariri picha.
Kuunda picha mpya
Gemini AI inaweza kukusaidia kuunda picha, logo au infografia kupitia maelezo utakayoyatoa.
Unachotakiwa kufanya ni kufungua AI ya Gemini kupita simu au kompyuta kisha chagua sehemu ya ‘image generation’ na uandike maelezo ya picha unayotaka kutengeneza mfano “Mtoto anacheza katika bustani yenye maua mekundu wakati wa jioni.
Baada ya kuandiika maelezo hayo ruhusu mchakato wa kutengeneza picha uanze kwa kubonyeza kitufe kilichoandikwa ‘Generate’ na baada ya sekunde kadhaa Gemini itaunda picha sawa na maelezo uliyotoa.
Ili uweze kupata matokeo bora unapaswa kuzingatia kutumia maelezo ya kutosha ikiwemo umbo, vipimo halisi, hisia unazotaka picha iwe nazo na mtindo mahususi (cartoon, realistic, 3D) ili kupata matokeo tarajiwa.
Katika hatua hii unaweza kpia kutumia akili bandia nyingine ikiwemo Chart GPT ili kupata maelezo yatakayokusaidia kutengeneza picha mpya kupitia Gemini AI.

Gemini AI inaweza kuwasaidia wabunifu, kutengeneza kazi za kipekee zaidi.Picha/Gemini AI.
Kuhariri picha
Pamoja na kuunda picha mpya Gemini AI ina uwezo wa kuhariri picha zilizokwisha kupigwa ikiwemo kuongeza au kuondoa vitu au watu,kurekebisha mwanga (brightness), rangi au saizi, kuboresha ubora wa picha na staili (kuwa katuni,michoro).
Ili kuhariri picha hizo unatakiwa kupakia picha unayotaka kuifanyia maboresho pamja na maelezo ya kile unachotaka kifanyike, mfano ondoa mtu aliye nyuma upande wa kushoto au geuza hii picha iwe katuni.
Ukishaweka maelezo hayo ruhusu Gemini AI ihariri kwa kubonyeza sehemu iliyoandikwa generate.
Baada ya sekunde chache Gemini itakupa matokeo kadhaa,unaweza kuchagua au kuomba maboresho zaidi kupitia picha mpya zilizundwa
Aidha, Gemini AI pia ina uwezo wa kuandika maandishi kwenye picha, kuchagua aina ya mwandiko ( font style) na miundo mingine mbalimbali.

Mbali na picha, Gemini AI pia inauwezo wa kutengeneza video kwa kadri ya maelezo utakayotoa.Picha/Lucy Samson.
Mambo ya kuzingatia
Licha ya AI hiyo kutumiwa na kuaminiwa na mamilioni inaweza kupotosha au kutengeneza uhalisia usiokuwepo hivyo ni vyema kutumiwa kwa uangalizi huku ikihusisha akili za kibinadamu (Human intelligence.)
Gemini pia imetoa onyo kwa watumiaji kuwa hawapaswi kuitumia kutoa maelekezo yanayoweza kusababisha madhara, ikijumuisha ushauri wa kujidhuru. pia haiwezi kusaidia katika shughuli hatarishi kama kununua dawa za kulevya au kutengeneza silaha.
Latest