Jinsi ya kudhibiti matumizi makubwa ya pesa wakati wa mapumziko ya wikiendi

December 20, 2019 4:38 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wikiendi usipoitumia vizuri inaweza kukuletea machungu na maumivu.
  • Tumia vizuri pesa yako wakati wa mtoko huku ukiwa umeipangilia vizuri ili isiharibu mipango mingine. 
  • Kama unaweza, kaa nyumbani na familia yako ili kuepuka gharama kubwa za mtoko. 

Dar es Salaam. Moja ya kanuni ya maisha ni kupata muda wa kupumzika baada ya shughuli nyingi za kuzalisha mali. Kupumzika siyo lazima alale au ukae bila kufanya kitu chochote.

Inaweza ikawa kubadilisha kazi au mambo ambayo umezoea kuyafanya kila siku. Ndiyo maana wengine hutumia kipindi cha mapumziko kutembelea ndugu na marafiki lakini wengine hutembelea vivutio vya utalii.

Ikiwa leo ndiyo tunaianza wikiendi na huenda umepanga kutoka na kwenda maeneo mbalimbali kujumuika na marafiki au na familia yako, usisahu jambo moja kuwa yote hayo ili yafanikiwe ni lazima utumie pesa.

Unawezaje kudhibiti matumizi ya pesa zako wakati ukiwa kwenye mapumziko ya mwisho wa wiki na kuhakikisha unatumia kulingana na unene wa mfuko wako? Jaribu dondoo hizi huenda zikakusaidia:

Kumbuka malengo yako

Matumizi yako ya pesa ni muhimu yaende sambamba na malengo uliyojiwekea; yawe ya muda mfupi au mrefu. Wakati ukijiandaa kwa mtoko leo au kesho, fikiria zaidi jinsi utakavyotumia pesa zako ili kuhakikisha kile ulichokipanga hakiathiriwi na matumizi yako wakati wa mapumziko. 

Wakati mwingine unaweza kujisahau na kutumia pesa uliyopanga kutekeleza jambo fulani la muhimu. Ni vema kukumbuka hilo hata kama mtoko utakuwa mzuri kiasi gani. Hii itakufanya kuwa mtu mwenye nidhamu katika matumizi. 

Lakini kabla hujaanza mapumziko, panga jinsi utakavyotumia pesa zako na utazielekeza wapi ili kukupa furaha uliyoikusudia. 

Panga ni kiasi gani cha pesa utatumia kabla ya mtoko. Picha|Mtandao.

Kunywa kwa kiasi

Kama kutumia vinywaji kwa wingi hasa soda na pombe na ndiyo tabia yako, jitahidi sana kunywa kwa kiasi ili kuepuka kutumia pesa nyingi kwa muda mfupi. 

Ulevi uliopitiliza unaweza kukuletea umaskini na kuifanya “weekend” yako iwe chungu. Ni vyema upange kabisa ni kiasi gani cha pesa kitatumika kwenye vinywaji na uhakikishe unatumia kiasi hicho bila kuzidisha. 

Tafuta eneo lenye gharama ndogo

Wakati ukiwaza ni wapi utapata mapumziko yako, basi tumia simu au hata matangazo kuangalia sehemu yenye kutoa huduma zinazoendana na mfuko wako. 

Eneo hilo linaweza kuwa mgahawa, fukwe, baa au hata maduka unayotaka kutembelea. Kufahamu bei ya vyakula, vinywaji na bidhaa nyingine kabla ya kununua kutakurahisishia kupanga vizuri bajeti yako. 

Tumia kulingana na uwezo wako, usinie makuu, maisha hayataki haraka. 


Soma zaidi: 


Tumia usafiri wa umma

Kama una gari binafsi au unatumia gari la kukodi, unaweza kuliacha nyumbani. Jumuika na watu wengine kwa kutumia usafiri wa umma ili ujifunze vitu vingi kutoka kwa wengine. 

Hii inaweza kukupunguzia gharama za mafuta ya gari na unaweza kufika unakokwenda kwa urahisi kwa sababu foleni inakuwa ndogo siku za mwisho wa juma. 

Pia itakupa fursa ya kutembea kwa miguu na kuupa mwili hali tofauti uliyozoea. Ni sehemu ya mazoezi, kama unaweza na una muda wa kutosha tembea umbali mrefu tu ili kujionea fahari ya dunia na vitu vilivyomo ndani yake. 

Changa pesa na wenzako

Kama una mpango wa kutoka na marafiki zako, ni vema mkachanga pesa kwa pamoja ili mtumie kwa pamoja. Itakusaidia kupunguza matumizi, kwa sababu pesa itakayotumika ni ile mliyokubaliana.

Pia itaimarisha uhusiano na marafiki zako au kukupunguzia mzigo wa kuwalipia bili za chakula na vinywaji. Mnaweza kutumia gari moja ili kupunguza gharama za kila mtu kutumia gari lake. 

Marafiki wa kweli watajali kipato chako na kukushauri kuwa na matumizi mazuri ya pesa. 

Ipe kipaumbele familia yako, onyesha upendo. Hapa mnaweza kununua mahitaji yote mnayotaka na mkapika kwa pamoja na kufurahia chakula cha pamoja. Picha|Mtandao. 

Tumia mapumziko yako ukiwa nyumbani

Kama hakuna haja ya kufanya mtoko, kwa nini usikae nyumbani na ufurahie na familia yako? Yapo mengi unayoweza kufanya ukiwa nyumbani ikiwemo kucheza na watoto wako na hata kutathmini mlikotoka na wapi mnakwenda.

Ipe kipaumbele familia yako, onyesha upendo. Hapa mnaweza kununua mahitaji yote mnayotaka na mkapika kwa pamoja na kufurahia chakula cha pamoja. 

Waswahili wanasema maisha ni kutumia, lakini kutumia lazima kuwe na mipaka. Nakutakia wikiendi njema yenye mapumziko mema kukuandaa kwa ajili ya wiki ijayo. 

Enable Notifications OK No thanks