Jinsi ya kudhibiti manunuzi mabaya ya nguo

February 16, 2019 5:23 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Usikimbizane na kila mtindo unaoingia sokoni, fanya manunuzi kulingana na ukubwa wa mfuko wako. 
  • Fanya manunuzi kulingana na wakati huku ukizingatia rangi chache zinazokuvutia.

Wewe ni miongoni mwa watu ambao hawapitwi na mitindo ya mavazi kila inapotoka na unapenda wakati wote kuwa na mwonekano mzuri kwa jamii inayokuzunguka? Lakini hujui ni jinsi gani unaweza kudhibiti matumizi makubwa ya pesa unazotumia kununua nguo wakati huohuo ukafanya mambo mengine ya maendeleo?

Kuvaa nguo nzuri au kila mtindo unaoingia sokoni sio jambo baya lakini ni kwa kiasi gani unaweza kutumia fedha zako vizuri ili bajeti yako isivurigike kisa tu kuwapendeza watu kwa mavazi.

Nukta inakuletea njia muhimu zinazoweza kukusaidia kutumia vizuri pesa na bado ukabaki na muonekano mzuri kwa mavazi yako.

Kagua kabati la nguo

Baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kutunza nguo kwa muda mrefu kiasi kwamba wanasahau idadi ya nguo walizonazo katika makabati au masanduku yao. Tenga muda wa kutosha kulifungua kabati lako ili kujua ni nguo gani hujavaa muda mrefu ambazo bado ziko katika fasheni ya sasa. 

Hii itakusaidia kupunguza gharama ya kununua nguo mpya mara kwa mara kwa sababu zipo kwenye kabati lako. Utakachotakiwa tu kizifanyia marekebisho madogo ili ziendane na mwonekano wa mwili wako.

Wakati mwingine tunalazimika kununua nguo mpya kwasababu hatupati muda wa kukagua nguo kwenye makabati yetu. Picha|Mtandao.

Tafuta mtindo unaokufaa zaidi

Changamoto inayowakuta watu wengi ni kununua nguo kwa mihemko na ushawishi ya watu kwa kila mtindo unaoingia sokoni. Kila mtu ana nguo zake ambazo akivaa zinamtoa na kuwa na mwonekano mzuri. 

Usipozingatia hilo utajikuta unanunua nguo nyingi ambazo hutazivaa kwa sababu haziendani na mwonekano wako. Kwanini utumie pesa nyingi kununua nguo nyingi ambazo unajua fika hutazivaa bali zitakaa kwenye kabati na kupigwa na vumbi? Ni heri ukawa na nguo chache lakini zinaenda na wakati.


Zinazohusiana:


Fanya manunuzi kulingana na wakati

Kila nguo zina wakati wake, fanya manunuzi kulingana na mahitaji ya nguo ya wakati huo. Mathalani kwa wanaoishi mikoa yenye joto kama Dar es Salaam, ukinunua nguo nzito utajikuta huvai na utaziweka kabatini. 

Katika kanuni za uchumi, bei ya bidhaa inakuwa kubwa kama kuna mahitaji makubwa ya bidhaa husika. Ili kuokoa gharama  unaweza kusubiri bei za nguo zishuke ambapo watu wameacha kuzichangamkia nguo za aina fulani. 

Lengo kubwa la nguo ni kusitiri mwili lakini unasaidia kukupa mwonekano mzuri mbele ya watu. Picha|Eyevine.

Usifue nguo mara kwa mara

Hapa haimaanishi kuwa uvae nguo zinazonuka hapana. Unatakiwa kufahamu kuwa kama nguo iko katika hali nzuri na haijachafuka sana haina haja ya kuifua. 

Kwa mfano jeans na masweta ya uzi yanaweza kuvaliwa mara nyingi kabla ya kufuliwa. Kutokufua nguo mara kwa mara pia  kunasaidia nguo zisichakae haraka lakini kunapunguza gharama za kufua au kupeleka kwa dobi. Hapa sisitizi uchafu la hasha. Nasisitiza matunzo bora ya nguo yanayoweza kusaidia kupunguza gharama zisizo za ziada kwenye mavazi. 


Chagua rangi ya nguo inayokufaa

Kila mtu ana rangi yake ya nguo ambayo akivaa anapata burudiko la moyo. Ili kuepuka kununua nguo mara kwa mara, chagua rangi chache zinazokuvutia. 

Kama huna uchaguzi wa rangi, utajikuta kila rangi ya nguo au unayoshauriwa na watu utaiona nzuri, jambo litakalokufanya kutumia gharama kubwa katika manunuzi.  

Kama huwezi kabisa kuhimili ushawishi wa rangi, hakikisha unanunua nguo zitakazoongeza thamani ya nguo ulizonazo nyumbani.

Chagua rangi chache za nguo ili kukutambulisha kwa muonekano uliotofauti na wengine. Picha|Mtandao.

Unaweza kuazima nguo 

Kama una mpango wa kuhudhuria tukio muhimu linalohitaji uvae mavazi ya aina fulani lakini huna mfuko wa kutosha kununua nguo hiyo ni vema kwenda katika maduka yanoyoazimisha nguo ukachukua halafu ukarudisha. 

Lakini yapo mavazi ambayo ukivaa mara moja huwezi tena kuvaa kwa sababu yamewekwa maalum kwa shughuli fulani. Mfano mzuri ni nguo za harusi hasa za wanawake ambapo baada ya tukio huwezi tena kuivaa katika mazingira ya kawaida. Nenda kaazime ili kupunguza gharama.


Nunua nguo kulingana na hadhi yako

Maduka ya nguo yana ushawishi mkubwa wa kutufanya tukimbizane na kila mtindo unaoingia sokoni. Angalia maisha uliyonayo yanaruhusu kufanya manunuzi ya nguo za gharama kubwa? 

Kumbuka nguo zimewekwa kusitiri mwili. Fasheni na mitindo ni vitu vya kupita. Nguo zisikufanye ukaharibu bajeti ya familia kwasababu tu ya kutafuta mwonekano mzuri mbele za watu.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW