Jinsi waathirika wa ajali ya moto soko la Karume wanavyoweza kusaidiwa kisaikolojia
- Wataalam wa kisaikolojia washauri wafanyabiashara kukubaliana na hali halisi na kuchukulia kama changamoto.
- Wanapaswa kufarijiwa na wakubali matokeo yaliyotokea.
- Washauriwa kukaa mbali na soko lilipoteketea.
Dar es Salaam. Kutokana na athari walizopata wafanyabiashara baada ya soko la Karume kuteketea kwa moto jijini Dar es Salaam, watalaam wa masuala ya saikolojia wamependekeza wahanga hao kupatiwa tiba ya kisaikolojia ili kuwarejesha katika hali ya kawaida.
Soko hilo liliteketea kwa moto usiku wa kuamkia Januari 16 mwaka huu kuwaharibu vibanda na bidhaa za wafanyabiashara zaidi ya 3,500.
Serikali inaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo ambayo imewaachia maumivu wafanyabiashara wa soko hilo ikiwemo kupoteza mitaji, wengine kupata mshtuko na kukata tamaa ya maisha.
Majanga makubwa kama hayo ya ajali za moto, vimbunga, matetemeko ya ardhi au mafuriko yanapotokea huja na athari mbalimbali kwa wahanga wa ajali hizo kuanzia ngazi ya kifamilia, kijamii na Taifa.
Kwa mujibu wa taasisi ya Brooken Haven retreat inayojihusisha na masuala ya kisaikolojia inaeleza kuwa kwa kawaida mtu ambaye hupatwa na majanga kama hayo huwa anahisi uoga, hofu, kutengwa, kujirudia rudia kwa tukio lililompata akilini, kukosa usalama, upweke, sonona, kusalitiwa, kujilaumu, kushindwa kupata umakini na utulivu wa kufikiri.
Hali hii huwa ni ya muda mfupi baada ya mtu kupatwa na tukio la kushtua na la kusikitisha na kama litaendelea kutokea kwa muda mrefu zaidi basi mtu huyo atahitaji kupatiwa msaada wa kitaaalam ili kuweza kukabiliana na hali hiyo.
Sehemu ya soko la Karume lililoteketea kwa moto hivi karibuni na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara. Picha| Mtandao.
Kazi kubwa ya kuwaepusha wahanga hawa ni kuwafariji pamoja na kuwa nao karibu na kuwatafutia maeneo ya utulivu ili waweze kurudi katika hali ya kawaida.
Mtaalam wa saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Erick Bunono amesema kuna njia mbalimbali za kuwasaidia wahanga wa ajali ya katika soko la Karume lililoteketea kwa moto.
Bunono amesema wanatakiwa wasikate tamaa na pia wawe wepesi kupokea matokeo ya kilichotokea licha ya kuwa wengi wao ni tegemezi pengine kwa familia zao au ndugu zao.
“Akili zao zipokee hilo tatizo kama changamoto tu za biashara ili waweze kuziruhusu akili zao kuwapa masuluhisho ya namna gani wanaweza kuamka na kusonga mbele tena au hata kuanza upya,” amesema Bunono na kusema wanapokata tamaa watazidi kuanguka zaidi kimaisha.
Bunono amesisitiza kuwa siku zote akili ikipokea jambo kama kitu kigumu sana basi jambo hilo litabaki kuwa mzigo mkubwa, lakini ukiruhusu akili kulipokea jambo kama changamoto basi njia zitafunguka taratibu na njia hizo zitakua suluhu za kukurejesha ulipokuwa.
“Katika maisha kuna vitu ambavyo vinatokea tu bila kupangwa na wakati vinatokea pengine ndio nafasi nzuri ya kujifunza kwamba hapa kuna kitu huwa kinatokea hivi.
“Hivyo wasimame upya bila woga waanze upya lakini katika kuanza huko basi wachukue tahadhari ya vitu vya muhimu vitakavyoweza kuwasaidia baadae kama kitu kama hicho kitajirudia tena,” ameongeza Bunono.
Bunono amewashauri wafanya biashara wa soko hilo wasiweke mawazo mengi sana juu ya hilo lililotokea bali wachukue muda huu kuwaza ni kwa namna gani wataweza kusimama upya ili waweze kujitoa kwenye msongo wa mawazo wa hasara kubwa waliyoipata kutokana na soko hilo kuungua.
Soma zaidi:
-
Wafanyabiashara wasota na soko liloungua miaka saba Dar
-
Wafanyabiashara wana la kujifunza kuungua soko la Kariakoo?
-
Suluhu ya kudumu majanga ya moto masoko ya Tanzania
Hatua za kukabiliana na matokeo ya janga hilo
Katika kukabiliana na matokeo ya majanga mbalimbali kama hili la wafanyabiashara wa soko la Karume kupoteza mapato, zipo hatua mbalimbali ambazo zinaweza kuwasaidia kutoka katika msongo wa mawazo waliyonayo.
Mwanasaikolojia kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii Tanzania, Dk Zainabu Rashid amesema kwanza kabisa wao wafanyabiashara wanatakiwa wakubali kwamba tayari eneo la kazi limeungua na waambiwe ukweli unaouma kuwa tayari limetokea na wamepoteza vyanzo vyao vya kujiingizia kipato.
“Katika kuwaambia ukweli wahanga wa jambo lolote lile mara nyingi wapo ambao wanakataa kabisa kuupokea ukweli lakini pia hiyo siyo mbaya kwa sababu ni miongoni mwa hatua za kukubaliana na kilichotokea,” amesema Dk Rashid.
Dk Rashid amesema kuwa wanasaikolojia wana nafasi ya kuwaelimisha wahanga hao ili waweze kukubaliana na kuelewa hali halisi na katika kumuelewesha mtu lazima apitie katika hatua zote hizo za aidha kukubaliana na matokeo ya tukio hilo au kukataa kabisa.
Mbali na hayo Dk Rashid amewashauri wafanyabiashara hao kuacha tabia ya kwenda katika maeneo yao ya biashara yaliyoteketea kwani itawasaidia sana katika kuondokana na msongo wa mawazo na kuwafanya waweze kufikiri juu ya namna gani wataweza kusimama na kuanza upya.
Katika kuanza upya wafanyabiashara wanaweza kuanza na hatua mbalimbali kama kuchukua mikopo midogo midogo ili kupata mitaji na kutafuta wafadhili watakaowasaidia kwa hali na mali waweze kuendelea na shughuli zao kama kawaida.